Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, Dodoma13/09/2016
Serikali imeendelea kupokea na kuhakiki madai ya watumishi wa umma yanayohusu mshahara na kuyalipa kadri ya uwezo wake kifedha.
Hayo
yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora Angellah Kairuki alipokuwa akijibu swali la
Mbunge wa Singida Mjini Mhe. Mussa Sima lililohusu mpango wa Serikali
kulipa madeni ya watumishi.
Waziri
Kairuki amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2014/2015 Serikali ililipa
madai ya malimbikizo ya mshahara wa shilingi 56,293,372,627.37 ambapo
yalilipwa kwa watumishi 55,688 waliokuwa na madai yatokanayo na
kupandishwa vyeo, ajira mpya na sababu nyinginezo.
Aidha,
Waziri Kairuki amesema kuwa kwa mwaka 2015/2016 Serikali imeendelea
kulipa madai ya malimbikizo ya mshahara wa watumishi wa umma ambapo hadi
kufika mwezi Juni, 2016 watumishi 31,032 walilipwa jumla ya shilingi
28,929,095,373.89.
Pia
ameongeza kuwa madai ya mishahara ya watumishi 7,871 yenye jumla ya
shilingi 13,754,462,429.29 yameshahakikiwa na kuingizwa kwenye mfumo wa
taarifa za kitumishi za mshahara yakisubiri kulipwa na madai ya
watumishi 8,776 yanaendelea kuhakikiwa ili yaingizwe kwenye mfumo tayari
kwa kulipwa.
Akijibu
swali la Mhe. Zubeda Sakuru (Viti Maalum) lililohusu changamoto ya
maslahi kwa watumishi wa sekta ya afya Waziri Kairuki amesema kuwa
Serikali inatambua na kudhamini mchango unaotolewa na madaktari,
matabibu na wauguzi nchini.
Hivyo,
Serikali imeendelea na jitihada za kuboresha mishahara ya watumishi wake
mwaka hadi mwaka ikiwemo ya wataalamu wa sekta hiyo kwa kuzingatia
uwezo wa Serikali wa kulipa.
Waziri
Kairuki amesema kuwa Serikali inaendelea na utafiti wa tathmini ya kazi,
punde itakapokamilika itapanga mishahara na motisha upya kwa watumishi
wote wa umma wakiwemo wa sekta ya afya.
Aidha,
amebainisha kuwa Serikali itaendelea kuboresha maslahi ya watumishi
kadri ya uwezo wake wa kulipa utakavyoimarika ambapo katika shughuli za
kila siku madeni huzalishwa lakini ni azma yake kuhakikisha madeni hayo
yanalipwa mara yanapojitokea.
No comments:
Post a Comment