Kumezuka
maandamano ya watu walio na hasira katika maeneo ya mji wa Charlotte
nchini Marekani, baada ya polisi kumpiga risasi mwanaume mmoja mweusi,
huku kukiwa na maelezo yanayotofautiana juu ya tukio hilo.
Mkesha wa
maombi uliokuwa wa amani, ghafla uligeuka kuwa maandamo ya watu
waliokuwa na hasira, na baadae ukawa usiku wa vurugu kubwa baada ya mtu
huyo kupigwa risasi na kuachwa na majeraha mabaya sana, huku
waandamanaji wakiwavamia polisi waliokuwa wakijaribu kuwatawanya.
Kumekuwa
na maelezo yanayotafautiana juu ya tukio hilo. Mkuu wa polisi wa mji wa
Charlotte , Kerr Putney, awali aliripoti kuwa mtu mmoja aliyepigwa
risasi wakati wa maandamano hayo ameuawa, lakini maafisa wa mji baadae
waliandika katika ukurasa wao wa Twitter kwamba mtu huyo amepelekwa
hospitali na yupo katika hali mbaya saa.
Maafisa
hao pia wamesema mtu huyo alipigwa risasi na raia mwenzake na si polisi.
Aidha, afisa mmoja wa polisi ameripotiwa kuwa anapata matibabu
hospitali baada ya kupata majeraha wakati wa maandamano hayo ya jana
usiku.
Mmoja wa
waandamanaji Braxton Winston amerekodiwa akizungumza kwa hasira huku
akiwa amezungukwa na waandamanaji wenzake akimtaka Mkuu wa polisi atoke
nje ya jengo aje azungumza nao.
“Daima
mnatuambia yale tusioruhusiwa kufanya. Haturuhusiwi kupiga magoti.
Haturuhusiwi kuandamana. Haturuhusiwi kusimama. Hatuna ruhusa ya kuimba.
Kitu gani tunachoruhusiwa kufanya. Chifu Kerr Putney, toka nje uje
utueleze kile tunachoruhusiwa kufanya, ” amesema Braxton Winston.
Gavana wa
jimbo la North Carolina, Pat McCrory ametangaza hali ya hatari jana
usiku katika mji mkubwa wa jimbo hilo wa Charlotte, na baadae kuita
kikosi cha ulinzi wa taifa baada ya Mkuu wa polisi wa Charlotte kusema
wanahitaji msaada.
Waandamanaji waharibu majengo ya biashara
Jana
usiku, mamia ya waandamanaji waliokuwa wakipiga mayowe "Maisha ya watu
weusi yana thamani" pamoja na "mikono juu, usifyatuwe risasi"
walitawanyika baada ya polisi kuanza kuwarushia mabomu ya kutoa machozi.
Lakini
makundi kadhaa ya waandamanaji yalibaki, na kushambulia raia, wakiwamo
maripota, walivunja vioo vya madirisha ya mahoteli, majengo ya maofisi,
migahawa huku wakiwasha moto mdogo katika maeneo tofauti.
Vurugu
ziliibuka watu walipoanza kuuliza masuali mengi kuhusu tukio la Jumanne
la kifo cha Keith Lamont Scott, menye umri wa miaka 43 aliyepigwa risasi
karibu na jengo analoishi. Polisi wamekataa kutoa mkanda wa video wa
ushahidi wa tukio hilo lakini wamesema Scott alikuwa amebeba bunduki na
alikataa mara kadhaa kufuata amri za polisi za kuweka silaha chini. Hata
hivyo, familia ya Scott pamoja na majirani zake wanasema hakuwa amebeba
bunduki bali kilikuwa ni kitabu.
Vurugu za
Charlotte zimewastaajabisha wengi, mji huo unaojulikana kwa biashara za
mabenki Kusini mwa Marekani, hauna kawaida ya kutokea vurugu
zinazohusiana na ubaguzi wa rangi wa polisi. Mji wa Charlotte una idadi
ya watu wapatao 830,000 na asilimia 35 miongoni mwao ni watu weusi.
DW
No comments:
Post a Comment