BAADA ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuusogeza mbele mchezo wa
Ligi Kuu kati ya Yanga na JKT Ruvu kocha msaidizi wa mabingwa hao
watetezi Juma Mwambusi amesema uamuzi huo umekuja wakati muafaka kwao
kwani wachezaji wao watapata muda wa kupumzika.
Yanga ilipangwa kucheza mechi ya kiporo ya ligi dhidi ya JKT Ruvu leo
Uwanja wa Taifa Dar es Salaam lakini TFF imesogeza mbele mchezo huo
mpaka utakapopangwa tena tarehe nyingine.
Taarifa ya TFF ilisema moja ya sababu za kuahirisha mchezo huo ni
kutokana na Yanga kuwa na wachezaji wengi kwenye kikosi cha timu ya
taifa, Taifa Stars kinachotarajiwa kwenda Nigeria kesho kwa ajili ya
mechi ya kuwania kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa Afrika Septemba
tatu.
Akizungumza na gazeti hili jana Mwambusi alisema hiyo ni nafasi nzuri
kwao kwani wataitumia kufanya mazoezi mepesi mepesi ili kuwapa muda wa
kupumzika wachezaji wao ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakitumika tangu
kumalizika kwa ligi ya msimu uliopita.
“Tunaishukuru TFF, kwa nafasi hii waliyotupa na sisi tutaitumia kwa
kufanya mazoezi mepesi ili wachezaji wetu waweze kupumzika na miili yao
iutamani mpira baada ya kufanya kazi mfululizo bila kupumzika lakini pia
nafasi hii itatusaidia kurudi kwenye kasi yetu tuliyokuwa nayo msimu
uliopita,” alisema Mwambusi.
Kocha huyo alisema mechi za michuano waliyokuwa wakishiriki zimewapa
uchovu mkubwa kutokana na ugumu, lakini hawakuwa na la kufanya zaidi ya
kufuata kile wanachotakiwa na TFF, ambao ndiyo waongozaji wa soka la
Tanzania.
Tayari ligi imeanza kwa timu 16 kushuka dimbani mara mbili kila moja
isipokuwa Yanga na JKT Ruvu ambazo zimecheza mchezo mmoja mmoja kutokana
na ratiba ya Yanga ilivyokuwa.
No comments:
Post a Comment