Sunday, August 7, 2016

Polisi Waendelea Kumsaka Dr. Mwaka


Mmiliki wa kituo cha Foreplan Clinic, Juma Mwaka, maarufu Dk Mwaka’ bado hajauepuka mkono wa Serikali na sasa Jeshi la Polisi limesema linataka limtie mikononi mwake ndani ya saa 24. 
Tangu Baraza la Mawaziri la Serikali ya Awamu ya Tano liapishwe mapema mwaka huu, Dk Mwaka, ambaye ni tabibu wa tiba mbadala amekuwa kwenye hali ngumu. 
Sakata lake lilianza baada ya Naibu Waziri wa Afya, Dk Hamisi Kigwangalla kufanya ziara ya kushtukiza kwenye kituo chake kilichoko Buguruni, lakini hakumkuta na kuamua kuagiza awasilishe nyaraka zake wizarani. 
Siku chache baadaye kituo hicho kiliendelea na shughuli zake za tiba, kikijitangaza kwenye vituo vya redio na televisheni na kudhamini mashindano, lakini Serikali ilitangaza kukifunga takriban wiki mbili zilizopita. 
Juzi, Dk Kigwangalla alifanya tena ziara ya kushtukiza na kukuta lundo la dawa za asili, kitu kilichomfanya aamini kuwa kituo hicho kinaendelea na shughuli zake kinyume na agizo la Serikali na hivyo kuagiza tabibu huyo akamatwe. 
Jana, Kamanda wa Polisi wa Ilala, Salum Hamdan alisema jeshi lake linaendelea kumsaka Dk Mwaka kama lilivyoagizwa na Waziri Kigwangalla. 
 “Vijana wangu wapo kazini kuhakikisha wanampata ndani ya saa 24,” alisema Kamanda Hamdan. 

“Nia ni kumfikisha mahakamani, lakini tutafanya hivyo endapo tutakuwa na ushahidi wa kutosha kuhusu madai dhidi yake, kama kudanganya umma kwa kujiita daktari, kuvaa mavazi na kutumia vifaa vinavyopaswa kutumiwa na madaktari na si waganga wa tiba mbadala. 
“Kosa jingine kama yalivyoainishwa ni pamoja na kukiuka agizo la kufungiwa na kuendelea kutoa tiba ndani ya jiji na nje kama vitabu vilivyokutwa ofisini kwake.” 

Baada ya kupata kibali cha Jeshi la Polisi juzi, Dk Kigwangalla aliingia ndani ya jengo kukagua na kukuta wateja wakiendelea kumiminika kufuata huduma, wengi wao wakiwa kina mama. 

Mara baada ya kufanya upekuzi na kukuta ndani ya jengo hilo kuna dawa, Dk Kigwangalla alizungumza na wateja hao. 
“Nimekuja kufuata huduma na hata juzi nilikuwa hapa. Taarifa kuwa kituo hiki kimefungiwa ninazo, lakini naona kila siku kwenye matangazo anayotoa kuwa bado anatoa huduma na kweli nikija hapa napata,” alisema mwanamama aliyejitambulisha kwa jina moja la Agnes na kukataa kutaja jina la pili.

No comments:

Post a Comment