Katibu
Mkuu wa Chama cha Ada Tadea, John Shibuda amesema Rais John Magufuli
“ni katili kwa wahujumu wa ustawi na maendeleo ya Taifa na rafiki kwa
waadilifu”, na kuwataka Watanzania kumuunga mkono kwa ukatili huo ambao
amesema unabezwa na baadhi ya watu.
Shibuda,
ambaye alikuwa mbunge wa Maswa Magharibi kwa tiketi ya Chadema na CCM
kwa vipindi tofauti, alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi
wa habari mjini Shinyanga.
Alisema
wanaodai Rais Magufuli ni dikteta hawajui viwango vya ubora wao katika
kutoa hukumu hiyo na kuwataka kuchagua kupendezesha waadilifu ili kwenda
peponi au waovu waliojipanga kwenda jehanamu.
“Ndugu
zangu ukweli haulogeki. Mahimizo ya Rais si udikteta, bali ni dhamira
ya kuibua msisimko wa uhuru na maendeleo na uhuru ni kazi na asiyefanya
kazi asinufaike na jasho la Watanzania,” alisema Shibuda ambaye anasifika kwa uwezo wake wa kutumia vizuri lugha ya Kiswahili.
Shibuda
alisema kama Magufuli ni katili, basi dini zote ni katili kwa kuwa zina
amri za Mungu ambazo zinawakataza watu kufanya mambo wanayoyapenda.
Alisema ndiyo maana viongozi wa dini nao wamekuwa wakisisitiza uadilifu, jambo ambalo Rais Magufuli analifanya.
“Napongeza ukatili wa Rais kukemea maovu,” alisema Shibuda.
Alisema
Serikali ya Awamu ya Tano imekuja katika dunia ya mabadiliko ya mila,
jadi na utamaduni wa utendaji wa umma na kukomesha uzembe katika
uwajibikaji, ufisadi na kuleta msisimko unaoshangiliwa na jamii na
kuondoa zomeazomea dhidi ya Serikali.
Kiongozi huyo wa upinzani alisema ajenda ya vyama vya upinzani imenyauka na kuvitaka kuacha kutafuta mfereji wa kutorokea.
Badala yake, alivitaka vyama vya upinzani kujipanga upya ili viwe na mtazamo mpya wa utendaji wa shughuli za kisiasa.
Aliifananisha
Serikali ya Awamu ya Tano na mabadiliko ya tabianchi duniani, akisema
Taifa limepata Rais mwenye utumishi changamfu na kugusa hisia za jamii.
“Vyama
vya upinzani viache siasa za mipasho na vijembe. Siasa hizi hazitatui
kero za umaskini, ujinga, uchumi wa kaya na wananchi,” alisema Shibuda.
“Wanasayansi
walianza na dawa ya panado zakutuliza maumivu, lakini leo kuna dawa
tatu na mseto kwa kuwa walishindana kugundua dawa bora, basi na
wapinzani wawe na vikosi kazi vya kubuni tiba mbadala ya kutengua
utumishi wa Rais Magufuli,” alisema Shibuda.
Alisema
hakuna chama chochote cha kisiasa Tanzania ambacho kipo kwa masilahi ya
kukweza chama kingine, bali kila chama kipo kwa ajili ya kugombania
kushika hisia za jamii na kuwa na dola na wala chama hakilazimishwi
kufungamana na tafsiri ya chama kingine kwani kina sera zake zaidi ya
kufungamana siasa na itikadi ya chama chenyewe.
Alisema
vyama vinaweza kuwa na ushirikiano wenye dhamira sahihi ya kukuza
masilahi ya jamii, ndiyo maana chama chake cha Ada Tadea kinashirikiana
na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Shibuda aliwataka wanasiasa kuwa
na mawazo makini ya kunufaisha fikra za Watanzania.
No comments:
Post a Comment