Na Mathias Canal, Singida
Wiki 16, Miezi minne itatosha kuwakutanisha pamoja vijana wa kata mbalimbali Wilayani Ikungi kwa pamoja wakipatiwa mafunzo ya Mgambo hususani kujifunza uzalendo, Mbinu za medani za kupambana na uhalifu, Kuimarisha nidhamu na kujituma.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu wakati akifungua rasmi mafunzo hayo yatakayojikita pia katika kuimarisha utu na uadilifu.
Mtaturu amesema kuwa vijana wote walioamua kujitolea katika mafunzo hayo kwa ridhaa yao watapaswa kuwekwa katika kumbukumbu ya vijana ambao baada ya kumaliza mafunzo wataanzishiwa vikundi vya ujasiriamali ambavyo vitasimamiwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
"Tanzania ina wimbi la vijana wengi ambao wanajiamulia maisha wenyewe kutokana na wazazi wao kuyakimbia majukumu yao ya kuwalea watoto wao katika maadili mema ya kumjua Mungu na nidhamu kwa kila mtu kwenye jamii hivyo sisi kama serikali ngazi ya Wilaya tutahakikisha Vijana hawa wanaimarika katika maadili mema" Alisema Mtaturu
Dc Mtaturu amesema kuwa mara baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo vijana hao watapaswa kuamua wanataka kujishughulisha na nini kati ya ufugaji na kilimo cha kisasa ambapo ofisi ya mkuu wa Wilaya itasimamia kuhakikisha wanafanikiwa katika malengo yao.
Sambamba na hayo amewaeleza vijana hao kuwa serikali ina mamlaka ya kuwasaidia watanzania kujikwamua katika wimbi kubwa la umasikini lakini pia vijana na watanzania kwa ujumla wanapaswa kutumia muda wao mwingi kujishughulisha na shughuli za uzalishaji mali kwa kufanya kazi sio kucheza bao, kujihusisha na vikundi ovu, kunywa pombe, Ngono zembe ama kucheza Pool Table wakati wa kazi.
Dc Mtaturu amewapongeza vijana hao kwa kujitolea kwa moyo mmoja kushiriki katika mafunzo hayo ambapo amesema kuwa mafunzo wanayoyapata sio mateso ila ni sehemu ya kuwaimarisha kimwili na kiakili, Kujifunza maadili mema, ili kuwa na uchungu na nchi yetu.
Mafunzo ya mgambo yaliyofunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu yanahusisha Tarafa mbili ya Ikungi na Sepuka ambapo katika Tarafa ya Ikungi vijana wa kiume waliojitokeza ni 138 huku wanawake wakiwa 6.
Kwa upande wa Tarafa ya Sepuka kuna jumla ya vijana 210 ambapo vijana wa kiume ni 206 na wanawake ni wa 4.
Katika ufunguzi wa Mafunzo hayo katika Tarafa hizo mbili Mkuu huyo wa Wilaya ya Ikungi aliambatana na Wajumbe wa kamati ya Ulinzi na usalama ya Wilaya.
Dc Mtaturu amesisitiza kuwa mgambo wanajulikana kama jeshi la akiba ambapo wajibu wao Mkubwa ni kushirikiana na jeshi la polisi na Jamii katika kuimarisha ulinzi wa watu na Mali zao.
No comments:
Post a Comment