KAMATI
ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imeitaka Wizara ya
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuwasimamisha kazi
watumishi watatu wa Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, akiwemo
Mwanasheria wa Manispaa hiyo, Barton Mahenge kutokana na matumizi mabaya
ya ofisi.
Watumishi
wengine waliotakiwa kusimamishwa kazi kutokana na matumizi hayo mabaya
ya ofisi na kushindwa kuishauri manispaa hiyo kuhusu mkataba wake na
Kampuni ya Oysterbay Villa ni Mchumi Mwandamizi, Ando Mwankuga na
Mratibu wa Uwekezaji na Mthamini wa Manispaa hiyo, Einhard Chidaga.
Pamoja
na hayo, Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene pamoja na kuahidi
kutekeleza maagizo hayo, pia ameapa kuwa atahakikisha watendaji wengine
waliohusika katika mkataba huo hata kama wamestaafu au kuacha kazi,
wanapatikana na kuwajibishwa.
Akizungumza
na uongozi wa manispaa hiyo, Mwenyekiti wa LAAC, Kangi Lugola alisema
watumishi hao pamoja na kuwepo kwenye madaraka yao kwa muda mrefu,
wameshindwa kushauri namna ya kufikia malengo ya mkataba huo ambayo ni
kuongeza mapato na ajira.
Alisema
kamati hiyo imebaini kuwa mkataba huo unaohusisha vitalu viwili
vilivyopo eneo la Oysterbay namba 277 na 322 vimekuwa vikimnufaisha
mwekezaji huyo pekee kwa muda wa miaka sita tangu ujenzi wa majengo ya
makazi ukamilike mwaka 2011.
“Kamati
hii imetafakari na kuamua kuwa mwanasheria, mchumi na mthamini wa
manispaa wasimamishwe kazi ili kupisha uchunguzi dhidi ya mkataba huu.
Kamati yangu pia itaunda kamati ndogo itakayoshirikiana na Sekretarieti
ya Sheria ya Bunge ili kuupitia kwa kina mkataba huu na kutoa ushauri
utakaosaidia manispaa hii,” alisisitiza Lugola.
Alisema
baada ya LAAC kupitia mkataba huo imebaini kuwa pamoja na manispaa hiyo
kutopata mapato kwa muda wa miaka sita huku majengo yakiwa matupu bila
wapangaji kwa kipindi chote, pia uwekezaji wa mradi huo unaojumuisha
ardhi, alipatiwa mwekezaji raia wa nje jambo ambalo ni kinyume cha
sheria za uwekezaji nchini.
Aidha,
alisema mkataba huo umebainisha mgawanyo wa mapato baina ya pande zote
mbili zilizoingia ubia ambao hauendani na kiwango cha uwekezaji kwani
Manispaa ya Kinondoni iliwekeza kwa kutumia ardhi kupitia vitalu viwili
vyenye thamani ya Sh bilioni sita wakati mwekezaji huyo alijenga majengo
hayo kwa gharama ya Sh bilioni 11.
“Mkataba
unaonesha mgawanyo wa mapato kwa kila upande na upande wa manispaa
unapata asilimia 25 kupitia vyumba vyake 17 vya mradi huo, wakati
kampuni ya Oysterbay Villa inapata asilimia 75 kupitia vyumba vyake 51,”
alisema Lugola katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na Naibu Spika Dk Tulia Ackson.
Alisema
mkataba huo pia unaonesha kuwa katika kitalu 377 mwekezaji anatakiwa
kujenga jengo la ghorofa lenye vyumba 40, lakini katika uhalisia
alijenga jengo lenye vyumba 44 huku mgawanyo ukibakia vilevile kama
mkataba wa awali ulivyotaka asilimia 25 na 75.
“Hili
ndio eneo lenye changa la macho, huu mgawanyo haueleweki na kama kweli
mnapata asilimia 25, mbona tangu mwaka 2011 manispaa haijapata hata
senti tano ya faida ya mradi huu zaidi ya kudai kuwa mnamdai mwekezaji
shilingi bilioni 3.5 tena za miaka hiyo…”
Pamoja
na maagizo hayo, pia kamati hiyo, iliitaka Wizara ya Tamisemi
ihakikishe inampatia Mwanasheria Mkuu (AG) wa Serikali mkataba huo ili
aupitie na kutoa ushauri wake.
No comments:
Post a Comment