Saturday, March 12, 2016

RC Wa Dar es Salaam Ampa ONYO Meya wa Manispaa ya Kinondoni


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, amemtaka Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Boniphace Jacob, kuacha malumbano ya kisiasa na badala yake ajikite kufanya kazi.

Onyo hilo Sadiki limekuja baada ya Meya Jacob kukaririwa akisema manispaa hiyo ina uwezo wa kukabiliana na uamuzi wa serikali wa kutoa elimu ya bure bila kuhitaji fedha zinazotolewa na utawala wa Rais John Magufuli.

Halmashauri ya wilaya ya Kinondoni inaongozwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao ni mwamvuli unaojumuisha wabunge na madiwani kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha Wananchi (CUF).

Sadiki alisema hahitaji malumbano na kiongozi huyo ambayo hayana tija.

"Mimi sipendi malumbano yasiyo na tija baina ya viongozi," alisema Mkuu wa Mkoa na kuongeza; "unapokataa msaada kama huo wa kupunguza mapungufu katika sekta ya elimu, wanaoathirika ni watu waliowachagua."

Serikali imepanga kutumia Sh. Bilioni 137 kugharamia elimu bure katika miezi sita ya kwanza ya Rais wa tano, Magufuli.

Kiasi cha Sh. bilioni 18.77 kilitumwa kwenye akaunti za shule za Msingi na Sekondari za halmashauri zote hapa nchini na vyombo vya usimamizi wa mitihani kwa kila mwezi wa Januari na Februari, kwa ajili ya wanafunzi kusoma bure.

Pesa zilizogawanywa kwenye akaunti za shule za Msingi na Sekondari katika halmashauri zote ni Sh. bilioni 15.7 kila mwezi na Sh. bilioni 3 kila mwezi kwenye akaunti vyombo vya usimamizi wa mitihani katika Halmashauri zote hapa nchini.

Mkuu wa Mkoa alisema fedha hizo zitapelekwa katika Manispaa zote na ametoa agizo kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni kutumia fedha hizo katika matumizi yaliyokusudiwa na si vinginevyo.

Sadiki alisema kwa sababu Rais Magufuli ni kiongozi wa wote, ana haki ya kutoa kwa wote bila kuzuia wala mipango yake kukataliwa.

"Yule ni mkuu wa nchi, hata kama wanakusanya fedha za kutosha, zipo taratibu za matumizi ya fedha hizo," alisema Sadiki.

Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mipango wakati akitoa taarifa ya kuanza kwa utumaji wa fedha za elimu bure Januari 6, mwaka huu, walimu wakuu wa shule zote za Msingi na Sekondari katika halmashauri zote hapa nchini wanatakiwa kuweka wazi matumizi ya fedha hizo katika mbao za matangazo kwa kila shule, ili kila mzazi aweze kujua kiasi gani kimetumika.

Sadiki alikuwa akizungumza wakati akipokea msaada wa ahadi ya ujenzi wa madarasa 12 katika mkoa wa Dar es Salaam kutoka kwa Wamiliki wa Malori Tanzaznia(Tatoa), yenye thamani ya Sh. milioni 300.

Mkoa wa Dar es Salaam, alisema Sadiki, una upungufu wa vyumba vya madarasa 7,223, lakini pia uhitaji wa madawati 66,000.

"Yapo maeneo mengi ya kujenga shule, nawaomba wadau wetu muendelee kuhamasisha kupata shule nzima kwani shule nzima inahitaji madarasa kuanzia 22," alisema.

No comments:

Post a Comment