Mbunge wa Segerea, Dk Makongoro Mahanga akionyesha karatasi za kura zinazodaiwa kuwa zilikwishapigwa zilizokamatwa wakati wa upigaji wa kura za maoni CCM juzi. Dk Makongoro alitangaza kujivua uanachama wa chama hicho na kujiunga Chadema kwa kile alichodaia ni uvunjifu wa sheria na hujuma dhidi yake. Picha na Venance Nestory
Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Makongoro Mahanga ametangaza kuihama CCM na kujiunga na Chadema baada ya kushindwa katika kura za maoni kwa nafasi ya ubunge katika Jimbo la Segerea.
Dk
Mahanga amechukua uamuzi huo ikiwa ni wiki moja tangu Waziri Mkuu wa
zamani, Edward Lowassa ahamie katika chama hicho kikuu cha upinzani
baada ya kukosa nafasi ya kugombea urais kwa tiketi ya CCM.
Dk
Mahanga ambaye amedumu kwenye nafasi ya unaibu waziri kwa kipindi chote
cha Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, alisema jana kuwa amejitoa katika
chama hicho kwa sababu utaratibu uliotumika katika uchaguzi wa Segerea
ulitawaliwa na vitendo vya rushwa na njama zilizofanywa na viongozi wa
kitaifa wa CCM ili kuhakikisha anaondolewa.
Akizungumza
na waandishi wa habari nyumbani kwake jana, Dk Mahanga alidai kuwa
baadhi ya wagombea katika jimbo hilo walianza kampeni mwaka 2013 jambo
ambalo ni kinyume cha sheria za chama.
“Nimetoa
malalamiko yangu mara kadhaa kwa uongozi wa CCM wilaya, mkoa na Taifa
lakini viongozi hao hawakuchukua hatua yoyote. Hii inaonyesha wazi kuwa
nao walikuwa ni sehemu ya mpango huo,” alisema Dk Mahanga.
Alisisitiza
kuwa hakubaliani na mchakato uliotumika katika kumpata mshindi kwa
sababu viongozi wa kata zote za Jimbo la Segerea walimbeba mgombea mmoja
na kuzunguka naye kwenye matawi kinyume cha matakwa ya kanuni za CCM.
Dk
Mahanga alisema fedha ziligawiwa kwa muda mrefu na siku ya kupiga kura,
baadhi ya maeneo wapigakura walipewa Sh10, 000 na kadi mpya zenye
majina feki zilizowawezesha kushiriki.
Alisema
operesheni ya kuhakikisha kwamba anaondoka kwenye jimbo hilo ilianza
muda mrefu, lakini ilishika kasi zaidi baada ya vikao vya CCM Taifa vya
kusaka mgombea urais, mjini Dodoma.
“Familia ya kigogo
mmoja wa CCM Taifa iliyokuwa inaishi jirani na mimi kule Dodoma iliamua
kuwasakama wanafamilia wangu ikiwaeleza kwamba baada ya Lowassa ni zamu
ya baba yao (mimi), lazima niondoke ubunge Segerea kwa gharama yoyote,”
alisema.
Alisema hata baada ya hapo, kauli kama hizo
ziliendelea wakati wote wa kampeni za ubunge na fedha nyingi ziliingizwa
jimboni na kufikia mikononi mwa mmoja wa wagombea ambaye alianza
kuzigawa kwa wingi na jeuri.
Dk Makongoro alisema
sababu nyingine ya kupigwa vita na CCM ni urafiki wake na Lowassa ambaye
tayari amehamia Chadema na kudai kwamba, mara kadhaa aliwahi kuonywa
juu ya urafiki wao.
Unaibu waziri
Alisema
kigogo mmoja serikalini aliwahi kumwambia kwamba kama ataendelea kuwa
karibu na Lowassa hatapanda cheo na ataendelea kuwa naibu waziri siku
zote. Alisema ulifika wakati alikata tamaa na kutaka kuacha unaibu
waziri lakini alishauriwa asifanye hivyo.
“Mimi ndiye
naibu waziri pekee ambaye nimekaa miaka 10. Wamekuja vijana wadogo ambao
hawana uzoefu na wakapewa uwaziri, mimi nikiendelea kuwa naibu waziri,
inakatisha tamaa sana,” alisema.
Dk Mahanga alisema
uhusiano wake na Lowassa ni wa muda mrefu na amekuwa rafiki wa familia.
Alisema alipokuwa kijana alikuwa anavutiwa na Rais Jakaya Kikwete na
Edward Lowassa, lakini baada ya Lowassa kujiuzulu mwaka 2008 walikuwa
karibu zaidi.
“Nampenda Lowassa kutokana na utendaji
kazi wake, akipewa majukumu ya kiserikali anayatekeleza kikamilifu,”
alisema na kusisitiza kuwa uongozi wa juu wa CCM unafinyanga demokrasia
na kuwanyima wananchi fursa ya kuchagua viongozi wao.
“Ninatangaza
kuanzia leo (jana) ninahamia Chadema na unaibu waziri wangu unakoma
kuanzia sasa. Nimeshamwagiza dereva wangu arejeshe gari la Serikali,”
alisema mbunge huyo wa Segerea.
Mtatiro amkaribisha Ukawa
Mara
baada ya Dk Mahanga kutangaza uamuzi huo, Julius Mtatiro anayewania
ubunge katika jimbo la Segerea kupitia CUF, aliandika kwenye ukurasa
wake wa Facebook: “Comrade Makongoro Mahanga! Karibu sana Ukawa. Kama
unalitaka Jimbo la Segerea njoo tushindanishwe kwa sifa, uwezo na
vigezo.
“Natambua utakuwa na mchango mkubwa sana kwa
ushindi wa Ukawa lakini lazima uwe tayari kumuunga mkono mgombea wa
Ukawa ambaye atapitishwa ikiwa si wewe. Huku Ukawa hakuna kususia, kuna
kushirikiana na kupambana tu.”
No comments:
Post a Comment