Kumekuwa na tuhuma kwamba usafirishaji wa mizigo na abiria kwa njia ya Reli ya Kati na Tazara umekuwa ukihujumiwa kwa makusudi ili wamiliki binafsi wa malori na mabasi wachume fedha kwa kufanya biashara hiyo.
Matokeo yake ni uharibifu wa
barabara na miundombinu mingine, huku wananchi wakiteseka kwa kukosa
huduma ya vyombo vya usafirishaji vyenye unafuu na uhakika.
Bado
kila siku inashuhudiwa magari makubwa ya kubebea mizigo na abiria
yakiwa yamejaza kupita kiasi, huku ikifahamika kwamba pindi yanapopita
kwenye barabara ni lazima kutatokea uharibifu wa miundombinu hiyo.
Ni
vyema kupita kwenye barabara zenye lami, kwani safari yako inakuwa na
uhakika wa kufika salama, lakini inaweza kugeuka shubiri pale
utakapokutana na barabara mbovu.
Inafahamika kwamba ujazo wa magari kupita kiasi pia ni sababu ya uharibifu wa barabara nchini.
Kwa
kuyatoza ushuru wa petroli, magari ya kigeni na yanayozidisha uzito
kwenye mizani, Mfuko wa Barabara(RF), umekusanya Sh293 bilioni.
Meneja
mfuko huo, Joseph Haule anasema upatikanaji wa ushuru huo kupitia
vyanzo hivyo vitatu umesaidia kwa kiasi kikubwa ujenzi wa barabara kwa
kiwango cha lami.
Anasema katika kipindi cha miaka 10
iliyopita, asilimia mbili ya mapato yote yalitokana na tozo ya magari
yanayozidisha uzito na kuongeza kuwa lengo ni kudhibiti magari ya mizigo
na abiria yasizidishe uzito.
“Tozo hii hukusanywa kwenye vituo vya mizani pale inapobainika kuwa gari limezidisha uzito kinyume cha sheria,’’ anasema Haule
Anaeleza
kwamba uzidishaji wa uzito ni chanzo kikubwa cha uharibifu wa barabara
nchini na kwamba kiwango hicho cha tozo hakiwezi kufidia uharibifu
unaofanywa na magari husika.
Haule anasema siku
wafanyabiashara watakapotimiza wajibu wao wa kutokuzidisha uzito,
kiwango hicho kitafutika na hakitachangia kitu chochote kwenye mfuko
huo.
Anasema tozo ya mafuta ni chanzo kikuu cha mapato
ya mfuko ambacho huchangia asilimia 97 ya mapato yote ya mfuko huo na
kupitia chanzo hicho, watumiaji wa barabara huchangia Sh263 kwa kila
lita ya petroli au dizeli wanayonunua. Kuhusu tozo ya magari ya kigeni
mipakani, Haule anasema yanachangia kwa asilimia moja kwenye mfuko
huo, kwani kiwango kinachotozwa ni Dola 16 za Marekani sawa na Sh33,600
kwa kilomita 100.
“Mchango wa chanzo hiki unategemea
ubora wa barabara zetu na ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam kuvutia
wafanyabiashara wa nchi za jirani kutumia miundombinu hiyo kusafirishia
mizigo,’’ anasema.
Meneja msaidizi wa mfuko huo, Ronald
Lwakatare anasema baada ya kukusanya ushuru huo wa Sh2,931 bilioni,
fedha hizo ziligawanywa kwenye idara husika zikiwamo Wakala wa Barabara
(Tanroads) iliyopatiwa Sh1,829 bilioni, Ofisi ya Waziri na Mkuu
(Tamisemi) Sh 874 bilioni na Wizara ya Ujenzi Sh200 bilioni na mfuko huo
ukabakiwa na 27.33 bilioni.
Lwakatare anasema barabara isipofanyiwa matengenezo ya mara kwa mara, huharibika kidogo kidogo.
Anasema:
“Utafiti uliofanywa Afrika Kusini na shirika la ‘The South African
National Road Agency,’ unaonyesha kuwa kama uharibifu mdogo
usipofanyiwa matengenezo kuna uwezekano wa barabara yote kuharibika
kabisa na kuhitajika kujengwa upya.’’
Anafafanua kuwa
ikiwa matengenezo yatafanywa baada ya miaka mitatu tangu uharibifu
utokee, gharamaza matengenezo hupanda mara sita zaidi na mara 18 ikiwa
matengenezo hayatafanywa katika miaka mitano.
Lwakatare
anasema ubora wa hali ya barabara huchangia kupanda au kushuka kwa
kiwango cha nauli kinachotozwa kwa abiria na mizigo, pia muda unaotumika
kusafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
“Idadi ya magari yanayotoa huduma katika njia yoyote hutegemea ubora wa barabara,” anasema.
Utafiti
uliofanywa mwaka 2006 na Tanroads kwa pamoja na Jumuiya ya Ulaya
kupitia mradi wa Rusrim ulibaini kuwa gharama ya nauli kati ya Mbamba
Bay na Songea Mjini ilishuka kutoka 10,000 hadi 5,000 baada ya
matengenezo ya barabara kukamilika.
Anasema kutokana na
mtandao wa barabara kufanyiwa matengenezo mara kwa mara, nchi jirani za
Malawi, Zambia, Burundi, DRC, Rwanda na Uganda hutumia barabara za
Tanzania kwa kupitisha mizigo Bandari ya Dar es Salaam, hivyo kuchangia
kuinua uchumi wa Taifa.
Amesema Bodi ya Barabara
ilifanya tafiti mbalimbali kwa lengo la kupanua wigo wa mapato na kuziba
mianya ya uvujaji wa mapato na matokeo yake yametumika kuishauri
Serikali namna ya kuziba mianya ya ukwepaji kodi ikiwamo suala la
uchakachuaji na uuzaji wa mafuta ambayo hayajalipiwa kodi kutoka nchi
jirani.
No comments:
Post a Comment