Baada ya kupatikana na hatia katika kesi tatu za wizi wa Fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (Epa) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na hivyo kutumikia adhabu ya kifungo jela, hatimaye jana Kada wa CCM, Rajabu Maranda alipangua kesi mojawapo iliyokuwa ikimkabili.
Maranda alikuwa anakabiliwa na jumla ya kesi tano
za Epa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, pamoja na wenzake akiwamo
binamu yake na baadhi ya maofisa wa BoT.
Jana, Mahakama ya Kisutu ilitoa hukumu ya kesi ya
nne kati ya tano zinazomuhusisha Maranda na kwa mara ya kwanza alishinda
kesi hiyo na hivyo kuachiwa huru.
Maranda, ambaye hata hivyo alikuwa nje baada ya
kumaliza vifungo katika kesi tatu alizokuwa ametiwa hatiani, aliachiwa
huru jana baada ya Mahakama ya Kisutu kumuona hana hatia katika kesi
hiyo.
Hukumu hiyo ilisomwa jana mchana na Hakimu John
Utamwa kwa niaba ya jopo la mahakimu waliokuwa wakisikiliza kesi hiyo.
Mbali na Utamwa ambaye kwa sasa ni Jaji wa Mahakama Kuu, mahakimu
wengine katika jopo hilo ni Ignas Kitusi (sasa Msajili Mkuu wa Mahakama
Kuu) na Eva Nkya.
Katika kesi iliyotolewa hukumu jana, mbali na
Maranda washtakiwa wengine ambao pia waliachiwa huru ni pamoja na binamu
yake Farijala Hussein, mfanyabiashara Ajay Somani na maofisa watatu wa
BoT, Iman Mwakosya, Ester Komu na Bosco Kimela.
Washtakiwa hao walikuwa wakidaiwa kuiba Sh207.3
milioni kutoka katika akaunti hiyo kwa kutumia nyaraka za kughushi,
kuonyesha kuwa kampuni yao ya Rashaz imepewa jukumu la kukusanya madeni
kwa niaba ya Kampuni ya General Marketing ya India.
Walikuwa wakidaiwa kutenda makosa hayo kati ya Septemba 8, 2003 na Agosti 18, 2008.
Hata hivyo, katika hukumu yake jana, Mahakama ya
Kisutu iliwaachia huru washtakiwa wote baada ya kujiridhisha kuwa hawana
hatia kwa mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili. Akisoma hukumu hiyo,
Utamwa alisema, upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka
yaliyokuwa yakiwakabili bila kuacha mashaka yoyote.
No comments:
Post a Comment