Naibu Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia, January Makamba amesema kuwa ana imani vikao vya kuwachuja wagombea wa urais vitafanya uamuzi kwa msingi wa kujiamini na siyo kwa hofu.
Makamba alisema hayo mjini Dodoma jana baada ya
kurejesha fomu za kuomba kuteuliwa na CCM kugombea urais katika Uchaguzi
Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
“Kama chama tumepata nafasi ya kupitia michakato
mingi migumu kuliko hata huu, tumefanya uamuzi katika mambo mengi na
makubwa na bado tumeendelea kubaki kuwa wamoja. Nina imani hata katika
hili pia tutavuka salama,” alisema Makamba.
Alisema wananchi wengi hasa vijana wanaangalia CCM
itamteua mgombea wa aina gani na wanataka aina mpya ya uongozi ambao
unaangalia mbele na unaoakisi matarajio yao.
Makamba alisema wana-CCM, kama walivyo wananchi
wote, wanachukizwa na rushwa na matumizi mabaya ya madaraka na
wanachukizwa na chama chao kuhusishwa na masuala hayo.
Alisema CCM wanataka wagombea kwa nafasi za ngazi
zote ambao wana mvuto kwa watu na ambao itakuwa rahisi kuwanadi bila
kuwatolea maelezo au utetezi kwanza.
Alisema katika kuomba nafasi hiyo ni vyema
kutosahau kwamba bado yupo Rais ambaye amefanya kazi nzuri na anaendelea
kuifanya iwe nzuri zaidi.
“Tusizungumze kana kwamba hakuna kilichofanyika.
Yeyote atakayepata heshima ya kuliongoza Taifa letu ataanzia alipoishia
Rais Jakaya Kikwete,” alisisitiza.
Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli, alisema
nafasi ya urais ni ya hadhi, heshima na dhamana kubwa hivyo ni muhimu
kujitafakari kwa kina kabla ya kuiomba.
Lakini pia ni muhimu kuiomba kwa staha,
unyenyekevu na hekima na kwa namna inayoendana na hadhi, heshima na
dhamana ya nafasi yenyewe.
“Anayeiomba nafasi hii kwa namna tofauti
hastahili. Binafsi nimejitafakari kwa kina. Nimejiandaa na nimeandaliwa
vizuri kiuongozi na kimaadili kwenye chama chetu, Serikali, bungeni na
kwenye utumishi wangu ndani ya Ikulu,” alisema.
No comments:
Post a Comment