Monday, July 20, 2015

BALOZI DK MAIGA ALIYEKUWA MUWANIA URAIS SASA KUGOMBEA UBUNGE IRINGA MJINI


BALOZI Mstaafu wa Umoja wa Mataifa (UN), Dk Agustine Maiga ameingia katika kinyang’anyiro cha kutafuta ridhaa ya wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ili agombee ubunge katika jimbo la Iringa Mjini.
Kabla ya kuingia katika kinyang’anyiro hicho, Dk Maiga alikuwa mmoja kati ya wana CCM 38 waliokuwa wakitafuta ridhaa ya chama hicho ili awanie urais; mchakato huo ulihitimishwa kwa kumchagua Dk John Pombe Magufuli kupeperusha bendera ya chama hicho.
Dk Magufuli, Dk Maiga na Jaji Augustino Ramadhani ni baadhi ya wana CCM waliotajwa mara baada ya sherehe za miaka 38 ya kuzaliwa kwa CCM zilizofanyika mwaka huu mjini Songea, kwamba uadilifu walionao unawabeba kurithi nafasi hiyo kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete.
Mbali na Dk Maiga, wana CCM wengine 12  wametajwa na Katibu wa CCM wa wilaya ya Iringa Elisha Mwampashi kuchukua fomu za kuwania kugombea nafasi hiyo.
Wana CCM hao ni pamoja na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa Jesca Msambatavangu, Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe Frederick Mwakalebala na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mahamudu Madenge.
Katika orodha hiyo yupo pia Dk Yahaya Msigwa, Nuru Hepautwa, Addo Mwasongwe,  Adestino Mwilinge, Frank Kibiki, Aidani Kiponda, Peter Mwanilwa, Fales Kibasa na Michael Mlowe.
Akizungumza na wanahabari mara baada ya kurejesha fomu zake, Dk Maiga alisema; “mimi nimerudi hapa nchini kuja kulitumikia Taifa langu katika ngazi yoyote ile ya uongozi.”
Alisema baada ya kufikiri na kupata ushauri kutoka katika makundi mbalimbali ya jamii, ameamua kuingia katika mchakato huo akiwa na dhamira ile ile iliyomsukuma kugombea urais ili ashirikiane na wana Iringa kuleta maendeleo.
Alisema endapo atachaguliwa vipaumbele vyake vitakuwa ni kuzingatia mambo yanayojikita katika biashara, uwekezaji, ujasiriamali, ajira kwa vijana, ustawi wa jamii pamoja na kuboresha yale ambayo yamefanyika.
Alisema mji wa Iringa una nafasi ya pekee katika uwekezaji kwani ni kiungo cha barabara kuu zinazounganisha baadhi ya barabara kuu nchini na zile zinazokwenda nchi za nje.
Kwa kufungua barabara hizo alisema, Iringa itakuwa kiungo cha kuendeleza utalii kusini mwa Tanzania ili ufikie kiwango cha ukanda wa kaskazini.
“Kama miji yoyote inavyopanuka kwa haraka, Iringa itapanuka kwa haraka na moja kati ya vipaumbele vyake itakuwa ni kujenga makazi ya kisasa,” alisema.
 Dk Maiga alisema kuingia katika kinyang’anyiro hicho, kwake yeye hiyo ni fursa ya pekee kwa kuzingatia kwamba jimbo la Iringa Mjini limekuwa katika mikono ya upinzani kwa miaka mitano sasa.
Alisema kwa kupitia jitihada mpya za kurudisha jimbo hilo mikononi mwa CCM, chama hicho kina haja ya kuingiza mawazo mapya, uongozi mpya na kutathimini nini kilichotokea ili yaliyotokea yasitokee tena.

Alisema katika siasa umoja ni ushidi na akaonya siasa isitumike kwa uhasama na rushwa ikataliwe kwani inadharirisha utu.

Alisema heshima CCM na wafuasi wa kutosha watarudi endapo makundi yaliyojengeka huko nyuma na kugawa chama yatamalizwa.

No comments:

Post a Comment