Monday, April 27, 2026

USIMAMIZI WA WAHANDISI WAZAWA WAKOLEZA NURU YA BWAWA LA JNHPP KWA USTAWI WA WATANZANIA







Na Mathias Canal, Dodoma

 

Utangulizi:

 

Mradi wa kufua umeme kwa kutumika nguvu ya maji katika mto Rufuji uliopewa jina la ‘Julius Nyerere Hydropower Project’, ukiwa ni uwekezaji wa Serikali ya Tanzania kutokana na fedha za ndani wa takribani Shilingi za Kitanzania trilioni sita na nusu, ulipata hati rasmi ya kukamilika kwa asilimia mia moja na Mkandarasi kuukabidhi tarehe 26 Machi 2025.

 

Maneno rahisi ni kwamba ‘mgodi umetema’. Tangu tarehe 22 Februari 2024 mtambo wa kwanza kutoka JNHPP ulipounganishwa na gridi ya taifa, kisha mtambo wa tisa na wa mwisho kuungwa na gridi tarehe 28 Machi 2025, rekodi za tarehe 31 Mei 2025 zinasoma JNHPP kuingiza mega-watt-hour 5,747,683.722. Kutumia kikokotoo cha bei ya TZS 292 kwa kila kilo-watt-hour, uingizwaji na kutumika kwa nishati hiyo kwenye gridi kunatafsiri mapato ya TZS 1,678,323,646,824 (Trilioni 1.678). Endapo uingizwaji na utumikaji wa umeme kutoka JNHPP utazingatia mwanzo huu mzuri unaoendana na usanifu wa mradi wa wastani wa uhakika wa mega-watt-hour 6,307 kwa mwaka, JNHPP itarudisha uwekwzaji wake wa TZS 6.5 trilioni katika kipindi kati ya miaka mitatu hadi minne.

 

Kuweka kumbukumbu sawa ni kuwa mtambo wa kwanza, mtambo namba tisa, ulikamilika ujenzi na wenyewe peke yake ukaunganishwa na gridi tarehe 22 Februari 2024 kupata mega-watt 235 zilizohitajika sana kupunguza makali ya upungufu wa mega-watt 300 katika gridi ya taifa ambapo nchi ilikuwa katika dhahama ya giza lilitotokana na upungufu wa umeme unaozalishwa vituoni. 

 

Mradi huu ambao ni moja kati ya miradi mikubwa kuwahi kutekelezwa nchini unajumuisha miradi kumi inayojitegemea katika jina moja la ‘Julius Nyerere Hydropower Project’.

 

Wasifu wa miradi kumi inayojumuishwa katika mradi wa Julius Nyerere ni: Kingo kubwa ya kuzuia maji yenye urefu wa mita 1,036 ikibeba pia barabara inayotumika kuvuka kutoka kaskazini mwa mto Rufiji kwenda kingo ya kusini; Bwawa ama kwa ufasaha zaidi ni ziwa kubwa linalokalia eneo la kilomita za mraba 1,194 likiwa na uwezo wa ujazo wa mita za ujazo bilioni 32.78; Jumba la mitambo na vinu vya kufua umeme vikiwa tisa kila kimoja chenye uwezo wa kufua mega wati 235; Kituo kikubwa cha wazi cha kupoza umeme cha kilovoti 400; Daraja lenye urefu wa mita 250 na uwezo wa kupitisha mzigo wa tani 250; Barabara za ndani ya mradi zenye urefu wa kilomita 42; Kingo nne za kuzuia maji yasitoroke na hivyo kutengeneza bakuli la ziwa zenye jumla ya urefu wa kilomita 17.4; Mahandaki matatu ya kupitisha maji kuelekea kwenye vinu vya kufua umeme yenye kipenyo wastani wa mita 12 yakijengwa kwa zege; Handaki lenye kipenyo wastani wa mita 14 likijengwa kwa zege lililotumika kuchepusha mto; Kijiji cha makazi wa watumishi watakao hudumia mtambo wa kufua umeme kikiwa na huduma zote na majumba takribani 150.

 

Mradi huu ambao kwa kukamilika kwake una umuhimu katika kuboresha ustawi wa maisha ya mwanadamu kwa matokeo chanya katika nyanja za kijamii, kiuchumi na mazingira, unatimiza malengo saba ya nchi ya Tanzania, yanayoainishwa kuwa: Chanzo cha kuaminika cha nishati safi; uimarishaji wa upatikanaji nishati kwa bei wanayoimudu wananchi; upatikaji wa njia za kuvuka na kuunganisha kingo za kusini na kaskazini za mto Rufiji; Uwepo wa ziwa kubwa la maji ikiwa ni hazina ya hekta milioni 60 za ardhi zinazostahili kuendelezwa kwa umwagiliaji; Hazina ya maji safi kwa  mkoa na jiji la Dar es Salaam na mkoa wa Pwani; Kuboresha ikolojia ya mbuga za wanyama, hifadhi za taifa, uwepo wa visiwa sita unaonogesha ushoroba wa kanda ya kusini ya utalii ya Tanzania; Urekebu wa ukame na mafuriko kwa ardhi na maeneo yaliyo chini kuelekea baharini ya bonde la mto Rufiji ambayo mafuriko yamekuwa ni tishio.   

 

Mradi huu ni endelevu (sustainable) kwa kuwa umewezesha ustawi wa sasa pia ni endelevu pia kwa uwezo (ability) wa kizazi kijacho kukidhi mahitaji yake.      

 

Ni kutokana na umuhimu huu wa kipekee wa bwawa la Julius Nyerere na mchango wake kwa maendeleo ya nchi, makala hii itazama kwa kina kufuatilia na kuandika historia yake, ujenzi wake, usimamizi wake na mchango wake kwa ustawi wa maisha ya mwanadamu.

 

Historia na Asili:

 

Historia na dhamira ya nchi kutumia nguvu ya maji ta mto Rufiji kufua umeme inaanzia miaka ya nyuma sana. Makala hii inatambua mahojiano aliyofanyiwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere mwezi wa Julai 1960, ikiwa ni kabla ya uhuru wa Tanganyika, akitanabahisha umuhimu wa kuujenga mradi huu.

 

Mwalimu Nyerere katika mahojiano hayo anautaja mto Rufiji kuwa hazina ya nishati ambao itawakomboa waafrika kwa kuwapatia ustawi na umoja baada ya kupata uhuru. Mwalimu alioona Rufiji kunufaisha Afrika na siyo Tanganyika pekee.

 

Ni jambo la heri kuiweka bayana kuwa kuanzia awamu ya kwanza ya uongozi Tanzania hadi kufikia awamu ya sita ya uongozi ambayo imekamilisha ndoto ya Tanzania kutumia nguvu ya maji ya mto Rufiji kufua nishati safi kwa ustawi wa mwanadamu, awamu zote sita zilichukulia kwa uzito na kwa nafasi na mazingira yalivyoruhusu, kuhakikisha kufikiwa kwa ndoto hiyo.

 

Kumekuwepo tafiti na taarifa za washauri elekezi ukijumuisha upembuzi yakinifu wa bonde la mto Rufiji katika kufua nishati jadidifu ikianzia ya miaka ya awali ya 1970 iliyotekelezwa na kampuni ya Norplan International, kisha miaka ya 1980 iliyotekelezwa na A/S Hafslund, kampuni zote mbili zikitokea nchi ya Norway. Mwaka 2012 kampuni ya Odebrecht kutoka Brazil ilitekeleza utafiti na upembuzi kuendeleza kazi zilizofanyika miaka ya 1970 na 1980. Pia mwaka 2014 kampuni ya SinoHydro kutoka nchini China ilishiriki kupembua nishati jadidifu ipatikanayo kutoka bonde la mto Rufiji.

 

Hatua kubwa ilifanyika kuzigeuza tafiti, ripoti na pembuzi yakinifu kuwa kitu halisia mwaka 2017 wakati Rais wa awamu ya tano alipoelekeza kuanza kwa utekelezaji wa kufua umeme katika bonde la mto Rufiji ukiitwa Stiegler’s Gorge Hydroelectric Power Project na hatimaye kubadilishwa jina ukiitwa Rufiji Hydropower Project. Wizara ya Nishati na Madini, kwa wakati huo ambayo sasa imeitwa Wizara ya Nishati, ilipewa jukumu la kuunda timu ya wataalam watendaji kuanza kutekeleza mradi. Timu iliyoundwa ilijumuisha watumishi kutoka TANESCO, Wizara ya Nishati, Taasisi nyingine za Serikali, Hekima Wazee na TANROADS.

 

Timu hii ya wataalam ilikuwa na hadidu rejea ya kuishauri Serikali kuhusu mchakato na njia bora ya kupata zabuni na wazabuni ili kutekeleza mradi. Pia timu ilipitia na kuhuisha tafiti, taarifa na upembuzi yakinifu wa miaka ya 1970, 1980, 2012 na 2014.

 

Timu ya wataalam pia ilifanikiwa kuandaa nyaraka za zabuni na ainisho la uhitaji na viwango vya mradi. Kazi hii ilifanikishwa kwa ushirikishwaji wa kampuni ya kiserikali kutoka Ethiopia ya Ethiopian Construction Design and Supervision Works Corporation- ECDSWC ndani ya mwaka wa 2017.

 

Katika marejeo ya ainisho la uhitaji na viwango vya mradi, nyaraka zilielekeza kujengwa kwa vinu tisa vya kufua umeme kila kimoja kikiwa na uwezo wa kufua mega wati 235 hivyo kuufanya mradi kuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 2115, ikiwa ni kituo cha pili kwa uwezo wa kuzalisha umeme kwa Afrika baada ya Grand Ethiopian Renaissance Dam yenye uwezo wa kuzalisha megawati takribani 5000 itakapokamilika. Nafasi ya tatu ni bwawa la Aswan nchini Misri linalozalisha megawati 2100. Pia ilipendekeza uzalishaji wa uhakika kwa mwaka kwa wastani wa Giga-Watt-Hour 6,153. Kipimo hiki cha Giga Watt-Hour ndio msingi wa kukototoa mapato halisia yapatikanayo kutokana na uuzaji wa umeme.

 

Timu hii iliyoundwa na watu watano ikijumuisha wengine kumi na sita katika sekretarieti ndiyo iliyoshiriki katika majadiliano na wazabuni mwaka 2017 na 2018 hata kufikia kilele cha kusainiwa kwa mkataba wa kandarasi ya ujenzi ya mradi wa kufua umeme kwa nguvu ya maji wa mto Rufiji.

 

Makala hii inawatambua washiriki wa timu ya wataalam kuwa Mhandisi Daktari Leonard Chamuriho- Mweyekiti,  Mhandisi Leonard Masanja- Katibu, Mhandisi Daktari Tito Mwinuka, Mhandisi Patrick Mfugale na Mhandisi John Mageni.

 

Sekretarieti ya timu ya wataalam ikijumuisha watu 16 ambao ni: Mhandisi Harold Kitainda, Mhandisi Justus Mtolera, Mhandisi James Luchagulla, Mhandisi Lutengano Mwandambo, Mhandisi Pakaya Mtamakaya, Elias Kisamo, Stanslaus Kizzy, Said Kalunde, Hassan Rugwa, Glory Kombe, Beatrice Stephen, Edson Mweyunge, Jackson William, Mhandisi Mhina Kiondo, Yosepha Tamamu na Ally Hashim

 

Zabuni iliyotangazwa kimataifa na Wizara ya Nishati mwaka 2017, ikiitwa ‘TENDER NO. ME/008/2017-2018/HQ/W/3 FOR CONSTRUCTION OF RUFIJI HYDROPOWER PROJECT (RHPP) AT STIEGLER’S GORGE ALONG THE RUFIJI RIVER UNDER EPC CONTRACT MODALITY INCLUDING INSTALLATION, TESTING AND COMMISSIONING’ ilikamilika mwezi Novemba 2018 ikimtangaza Joint Venture of Arab Contractors and Elsewedy Electric (JV-ACEE) of Egypt kufanikiwa kuteuliwa.

 

TANESCO, iliyo chini ya Wizara ya Nishati, na iliyokasimiwa mamlaka ya kuusimamia mradi kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilisaini mkataba tarehe 12 Desemba 2018 na Mkandarasi Joint Venture (JV-ACEE) of M/S Arab Contractors “Osman A. Osman & Co.” (AC) and Elsewedy Electric (EE) katika hafla iliyofanyika Ikulu Dar es Salaam kwa kushudiwa na Rais wa Tanzania na Rais wa Misri

 

Mkataba uliosainiwa unatambulishwa na Jumuiko la Washauri Elekezi Kimataifa (International Federation of Consulting Engineers- FIDIC), kitabu kinachojulikana kuwa ni ‘Silver’ chapisho la mwaka 1999. Mkataba ulielekeza kuanza rasmi kwa utekelezaji wa mradi wa mega wati 2115 kuanzia tarehe 15 Desemba 2018, mradi utajengwa kwa miezi 42, ikijumuisha miezi 6 ya awali ya maandalizi. Hivyo mradi ulielekezwa kukamilika 15 Juni 2022. Gharama ya mradi ikiwa ni Shilingi za kitanzania 6,558,579,983,500.28. Pia majadiliano yalifanikisha kuongeza uzalishaji wa uhakika kwa mwaka kwa wastani wa Giga-Watt-Hour kutoka 6,153 hadi 6,307

 

Ikumbukwe kuwa tarehe 5 Novemba 2019 kwa kusaini nyongeza namba moja ya mkataba kubadili jina la mradi kuwa ‘JULIUS NYERERE HYDROPOWER PROJECT (JNHPP).

 

Usimamizi na Uendeshaji:

 

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Nishati ikiwa ndiye muwekezaji wa mradi, iligatua usimamizi wa mradi kwa TANESCO kama chombo mahsusi yaani ‘Special Purpose Vehicle’. Hivyo mkataba wa ujenzi wa JNHPP uliingiwa kati ta TANESCO na Mkandarasi.

 

Katika taratibu zilizofuata za uendeshaji wa miradi ya ujenzi na kihandisi, TANESCO ilifanya uteuzi wa TANROADS kuwa Mshauri Elekezi na msimamizi wa mkataba na ujenzi wa mradi. TANROADS ilielekeza ushauri elekezi na usimamizi wa mkataba na usimamizi wa ujenzi wa mradi utekelezwe na kitengo chake tanzu cha ushauri elekezi yaani TANROADS Engineering and Consulting Unit (TECU). Kwa kuzingatia ainisho ka kitabu cha FIDIC cha Silver, TECU ilikasimiwa jukumu la mwakilishi wa mwajiri yaani Employer’s Representative.

 

Makubaliano (Memorundum of Understanding) kati ta taasisi mbili za serikali, TANESCO na TANROADS yalisainiwa tarehe 17 Aprili 2019 hivyo timu ya wataalam wabobezi (Experts) 18 wakaanza kazi rasmi kusimamia mkataba na kusimamia ujenzi tarehe 18 Aprili 2019.

 

Historia kwa kina ya TECU kwenye mradi huu

 

Historia ya kina ya TECU iliyosimamia mradi huu inajipambanua na miradi mingine kuwa ni tofauti. Inabainishwa kuwa timu hii ya wabobezi ilikuwa ni mchujo na uteuzi maalum kutokana na watanzania wa nyanja zote waliounda timu ya taifa itakayoipigania nchi kizalendo kusimamia mradi mkubwa wenye maslahi mapana kwa taifa. Pia inabainishwa kuwa timu hii ya taifa ilitoa unafuu wa gharama za ushauri elekezi kwa kuwa ni takribani asilimia 12.51 ya gharama ambazo mzabuni wa chini aliwasilisha kwa kazi hiyo.

 

Wataalam wabobezi waliojumuika kuunda timu ya taifa kulipigania taifa kizalendo katika kuusimamia mradi walikuwa ni:  Mhandisi Chrispianus Bayo Ako; Mhandisi Mushubila L.Kamuhabwa; Mhandisi Lutengano Mwandambo; Mhandisi John Musobi  Mageni; Mhandisi Daktari Majige Mabulla; Mhandisi Pakaya Mtamakaya; Mhandisi Justus Mtolera; Joseph Kiyumbi; Mhandisi James Luchagullah; Mhandisi Stanslaus Kizzy; Mhandisi Kamugenyi Luteganya; Mhandisi John Samwel Masiko; Daktari Obeid Saitabau Lemna; Mhandisi Francis Mutabazi; Mhandisi David Munkyala, Enock Mabugo; Mhandisi Bahati K. Buzenganwa; na Mhandisi Daktari Robert Wendo Kabudi.

 

Mwaka 2020 timu ya usimamizi ya TECU iliongezeka na kuongeza wataalam wafuatao: Mr. Gabriel Thobias Mwita; Ms. Hawa Ismail Nassoro; Mhandisi Justine Kessy; Belingtone G. Mariki; Del’chance Nuru; Leviticus Bossa; Nuruanna Y. Lori; Ng’wandu Johnson; Dr. Bwire S. Ndazi.

 

Mwaka 2021 wafuatao waliongezwa: Didas Francis Urio; Kulwa M. Sylvester; Rodrick Pius Komu; Chrispin T. Mutagaywa; Denis Ngusa Lucas; Abdul Ayubu Samata; Ramadhan Said Hamza; Jessica Moses; Leonard Qoqona Mahu; Amiri Halifa Hida; Simon Leole; na Peter C. Romati.

 

Mwaka 2021 kwa umuhimu wa kuwafunda wataalam wa TANESCO, wafuatao walijumuishwa TECU wakitokea TANESCO kwa madhumuni ya kufundwa: Dennis Masini; Frank J. William; Emmanuel G. Nkembo; Anterius A. Ndyetabula; Johnson Godfather Mola; Michael Patrick Laurent; Innocent Abel Kafugugu; Justine Bernard Dominick; George Evarist Theophil; John Aliko Mwakarobo; na Leokadia Joseph Badi.

 

Mwaka 2022 timu iliongeza wafuatao: Augustino A. Christopher; Raymond J. Haule; Athumani A. Mchindu; Daktari Isack A. Legonda; Sylvester K. Mgina; Joackim Joseph Mrema.

 

Mwaka 2023 waliongezeka: Mwanahamisi John; Bakari Mahmoud; John C. Tchinyangile; Richard Mhongole; Stephen N. Lowoko; Elieza Tunze; Pilla H. Patrick; na Peter Y. Mangoma.

Mwaka 2024: Lilian George Kaskazi; Gift Alli Shoo; Tosta Jonas Hopaje; na Calvin Elias Mulungu. Jumla ya wataalam 67 wametumikia TECU katika kusimamia mradi wa JNHPP.

 

 

Taarifa ya kina kuhusu TECU/TANESCO ilivyoendesha na kusimamia bwawa, ikiwa ni pamoja na matengenezo, usalama, na matumizi ya nishati.

 

Ndani ya siku 2,293, kuanzia kuanza kuusimamia rasmi mkataba na ujenzi wa JNHPP tarehe 18 Aprili 2019 hadi kukamilika 26 Machi 2025, wataalam wabobezi wa TECU wametumia ubunifu na weledi wa kiwango kikubwa kuutafsiri mto Rufiji katika ustawi wa maisha bora ya wanadamu. Ujenzi wa tuta kuu la kukinga maji likiwa na urefu wa mita 1,036 na kina cha mita 133.5 kwa kutumia zege maalum lisilo hitaji nondo liitwalo ‘Roller Compacted Conrete’ (RCC) ulitimizwa katika muda muafaka kufuatia methodojia iliyoboreshwa. Uwepo wa mvua kubwa ulitishia kucheleweshwa kuanza ujenzi wa tuta kuu na handaki la kuchepusha maji kwa mwaka mzima. Wataalam walibuni methodolojia ya kuanza ujenzi kutokea kingo za pembeni (abutments) kuelekea mtoni badala ya kutokea mtoni kwenda kwenye kingo. Sambamba na ubunifu huo, iliamuliwa kujenga handaki moja tu la kuchepusha mto badala ya mawili ambayo ujenzi wake ungechelewesha kuanza ujenzi wa tuta kuu kwa miaka miwili. Ubunifu na umahiri mkubwa ulikuwa ni kutumia tuta kuu linalojengwa kufungua lango (notch) kupitisha maji ya mto pale mvua zinapoongezeka huku ujenzi wa tuta ukiendelea.

 

Sayansi hii ilisaidia sana kupunguza muda wa kukamilisha mradi na itabaki kuwa hazina ya maarifa katika tasnia ya ujenzi wa mabwawa ulimwenguni.

 

Kazi kubwa ya ubunifu pia ilihusisha upatikanaji wa mchanganyiko wa zege la RCC kwa kutumia mali ghafi inayopatikana nchini ya ‘pozzolana’ badala ya ‘fly ash’ ambayo ilikuwa inaagizwa kutoka nje ya nchi. Kulikuwa na upinzani mkubwa kutumia ‘pozzolana’, mikingamo (obstacles) ikionyesha kuwa majaribio ya kupata mchanganyiko unaotakiwa kwa kutumia ‘pozzolana’ ya Tanzania hayafikii viwango. Ilibidi ofisi ya TECU igeuzwe kuwa maabara na kusimamiwa na wataalam wenyewe wa TECU ndipo majaribio (trials) yalitoa majibu yaliyoonyesha ‘pozzolana’ ilikuwa na ufanisi mkubwa na viwango vinavyokubalika. Kazi hii ilisimamiwa kwa umahiri na weledi mkubwa hata ‘pozzolana’ kutoka Tanzania ikatumika katika mradi wa JNHPP.

 

Ubunifu mwingine wa kukumbukwa ni uwezeshaji wa kuvuka ng’ambo ya pili ya mto Rufiji kwa kutumia madaraja ya haraka. Wataalam waliharakisha ujenzi wa Daraja la kwanza lenye kina cha mita 80 ili kuanza ujenzi ng’ambo ya pili kwa kutambua kuwa mvua kubwa zitakaponyesha litasombwa na mto. Wakati yaliyotabiririwa yakitokea Daraja la kina cha mita 100 na ambalo lilikusudiwa kwa kazi hiyo lilikuwa limekamilika na kuanza kutumika ili hali manufaa ya Daraja lililosombwa na mto yakiwa ni dhahiri kwa kazi nyingi na kubwa ng’ambo ya pili ambazo zilikuwa zimeshamiri na kuendelea kwa kasi. Ubunifu uliendelea kwa Daraja la kina cha mita 100 ambalo liliongezewa kimo na kufikisha kina cha mita 120 hivyo kulifanya litumike muda wote hadi pale eneo hilo lilipozamishwa na kugezwa kuwa bwawa. Sayansi hii ya kuongeza kimo cha Daraja ambalo tayari limejengwa ni hazina katika tasnia ya barabara katika nyakati hizi na zijazo.

 

Pia kulikuwa na ubunifu katika ujenzi wa kuta za muda za kuzuia maji (cofferdams) ambapo zege la majaribio (trial mix) ndilo lilitumika na hivyo kupata uthibitisho katika ujenzi halisi. Sayansi hii ya kujifunza kwa kuzalisha kitu halisia ni hazina ya sasa na baadae katika nyanja ya uanagenzi (apprecentiship)

 

Lakini pia ujenzi wa kingo za kuzuia maji kutoroka (Saddle Dams) uligubikwa na changamoto ambazo zilihitaji ubunifu mkubwa. Kingo ya kwanza ilibadilishwa kuwa ni ya zege lisilokuwa na nondo ili litumike kuwa lango la dharura lisilo la mageti (un-gated emergency spill). Kingo tatu zilizosalia zilielekezwa kutumia mawe, udongo na chokaa ambavyo vinapatikana eneo la mradi badala ya pendekezo la kutumia mali ghafi itokayo nje ya nchi ya ‘membrane’.

 

Wataalam wa TECU walikuwa na kitengo cha usalama kazini. Changamoto ya kwanza ilikuwa ni ajali iliyosababisha kifo cha mtaalam kutoka China, kijana Mao, ambacho kilisababishwa na kuporomokewa na kupondwa na mawe makubwa wakati wa utegaji baruti kutoboa handaki la kuchepusha mto. Taratibu zote za usalama kazini zilikuwa zimefuatwa na kuzingatiwa. Tukio hili linaacha jambo la kujifunza katika tasnia hii kwani ripoti zinaonyesha kila kitu kuwa sawa lakini tukio lilitokea na kuchukua uhai wa binadamu mwenzetu.

 

Katika sura hii ya usimamizi na uendeshaji ni vema kuweka rekodi kuwa usimamizi ulishuhudia na kuheshimu ushauri wa wakandarasi na hasa kutoka China kuwa wakati wa kutoboa mahandaki ya kuchepusha mto na kupeleka maji kwenye mitambo, kuna jinsia ambayo inaruhusiwa kuingia pindi tu uchorongaji unapofikia upande wa pili. Lakini pia ulikuwapo utaratibu wa maombezi maalum kabla ya ukataji wa miti mikubwa ikyokuwa na umri mkubwa.

 

Mradi wa JNHPP uliajiri watu takribani 12,800 waliojihusisha moja kwa moja. Wataalam wa TECU walipitia (review) makabrasha 12,576 ya mawasihisho ya kiufundi (Technical Submissions), walifanya kaguzi  44,155 (Inspections) kuthibitisha ubora pia kaguzi na majaribio viwandani 376 (Factory Inspection Tests).

 

Faida za kuwa na shirika imara la usimamizi kama TECU.

 

Kuna faida za wazi kwa manufaa ya nchi kuwa na shirika imara la usimamizi na ushauri elekezi kama ilivyokuwa TECU katika mradi mkubwa wenye maslahi kwa nchi wa JNHPP.

 

Mradi wa JNHPP katika uwazi wake umedhihirisha uwepo wa uadilifu, umahiri na umakini wa kiwango cha juu. Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa mahesabu (NAOT & CAG), kwa kutekeleza mamlaka iliyokabidhiwa chini ya kifungu 29 cha Sheria ya Manununuzi ya Umma, iliwasilisha taarifa tatu za ukaguzi kwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na kupitia Bunge mara tatu. Ukaguzi (Technical Audit) uliwasilishwa Machi 2021, Machi 2023 na Machi 2025.

 

Ripoti ya kaguzi zote tatu imepongeza na kutambua kuwa kwa ushauri wa TECU kumekuwa na ushahidi wa dhati wa weledi, uadilifu na dhamira ya dhati kuhakikisha mradi unatimiza malengo yaliyokusudiwa na taifa.

 

Taasisi ya Kuzuia na Kupamabana na Rushwa (TAKUKURU), chombo cha Taifa, kilifanya kaguzi saba na kuutembelea mradi mara tisa. Pia Wizara ya Fedha na Mipango (August 2022) ilifanya ukaguzi maalum (special audit) kwa mradi wa JNHPP. Kaguzi hizi za taasisi mbili za serikali pia zilipongeza uwazi, uadilifu na uthubutu wa hali ya juu ambao haukukiuka misingi ya maadili na uwajibikaji wala matarajio ya umma.

 

Majina ya  kampuni au wakandarasi walioshiriki katika ujenzi kama TECU

 

Mfadhili (Donor): Serikali ya JMT kupitia Wizara ya Nishati

Chombo cha Utekelezaji (Special Purpose Vehicle): TANROADS

Mshauri Elekezi (Consultant/ Employer’s Representative): TANROADS Engineering and Consulting Unit (TECU)

Mkandarasi: JV Arab Contractors and ElSewedy Electric, Egypty.

 

Lakini pia kulikuwa na wakandarasi washiriki (subcontractors) wa kigeni na wazawa. makampuni ya kigeni yalikuwa 11 na ya wazawa 104 (Orodha ipo kwenye Ripoti za mwezi za TECU)

 

Mchango kwa Taifa:

 

Maelezo kuhusu bwawa linavyochangia uzalishaji wa umeme kwa ajili ya taifa, hasa katika mkoa wa nyanda za juu kusini na maeneo ya jirani. Association na maendeleo ya kiuchumi na kijamii, pamoja na ajira na maendeleo ya sekta nyingine.

 

Tanzania, tangu miaka ya 1970 na kwa muda wote na awamu zote sita za uongozi, ilijiwekea na imedumu kulenga kutafsiri maji tiririka ya mto Rufiji katika kuboresha, kunufaisha na kuongeza ustawi wa maisha ya wanadamu

 

Ndoto imetimia, kwani tarehe 26 Machi 2025 JNHPP ilikabidhiwa rasmi kwa nchi ikiwa imekamilika asilimia 100, ikizalisha mega-watt 2115 na wastani wa uhakika kwa mwaka wa giga-watt-hour 6,307. Wastani huu wa uhakika wa giga-watt-hour kwa mwaka ukitafsiriwa kwa kikotoo cha mauzo cha TZS 292 kilo-watt-hour ni mavuno ya TZS 1,841,644,000.

 

TANROADS-TECU, mshauri elekezi wa mradi inajivunia kutimiza wajibu wake kwa weledi na ufanisi kufanikisha kufikiwa kitaifa kwa malengo ya mradi. Mradi unaibadilisha ramani ya Tanzania kwa kuunda ziwa la tano kwa ukubwa Tanzania baada za maziwa Victoria, Tanganyika, Nyasa na Rukwa. Ziwa hili linaloitwa Bwawa la Julius Nyerere lina ukubwa wa kilomita za mraba 1,194

 

Mradi wa JNHPP una mchango wa kipekee kabisa kwa nchi katika Nyanja za kijamii, kiuchumi na mazingira ikiwa ni Chanya kuboresha ustawi wa maisha ya mwanadamu katika maeneo saba makuu (primary objectives):

 

Hiki ni chanzo cha kuaminika cha nishati safi; Ni nishati ambayo wananchi wanamudu; Mradi unaunganisha kingo za kusini na kaskazini za mto Rufiji kupitia Daraja na tuta kuu; Ni hifadhi yam aji lukuki kwa ajili ya ardhi ya hekta 60 milioni zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji; Ni hifadhi yam aji safi kwa jiji na mikoa ya Dar Es Salaam na Pwani; Ni ngome ya mbuga za taifa na game reserves na visiwa kwa ajili ya utalii kwa ushoroba wa kusini mwa Tanzania; Unarekebu ukame na mafuriko katika maeneo ya chini yam to Rufiji kuelekea Bahari ya Hindi ambayo ni muhanga wa majanga.

 

Mbali ya maeneo saba makuu (primary objectives) yaliyoanishiwa pia kuna maeneo kumi na tatu ya upili (secondary objectives) ambayo ni:

 

Sasa Tanzania inazalisha umeme unazidi uhitaji wa ndani na hivyo kuchangia katika kapu la nishati na Kusini mwa Jangwa la Sahara (power pool agreement pact for Africa South of Sahara; Uhakika wa uanagenzi (apprenticeship) na elimu ya viwango (quality education for hydro-energy professionals); Ushirikiano katika tasnia (partnership with industry players); Uangalizi wa vyanzo na maeneo yowevu (catchment area of about 158,420 square Kilometre) katika wilaya 29 zilizo ndani ya mikoa 10 ya Tanzania; Uhifadhi wa mazingira kwa kupunguza ukataji wa miti kama chanzo cha nishati; Uchochezi wa skimu za kilimo cha umwagiliaji na viwanda vya uchakataji chakula; Kutengeneza ajira kutokana na kilimo na uchakataji mazao ghafi; Kuchagiza mauzo ya nje yatokanayo na bidhaa za kilimo; Chanzo kipya cha mapatao ya nchi kutokana na bidhaa za kilimo; Kuundwa kwa mji na jamii wa kisasa wenye kituo cha afya na Barabara unaochagiza mzunguko wa fedha kwa mikoa ya Morogoro, Pwani na Lindi; Chanzo cha mapato kwa Halmashauri za Wilaya za Morogoro, Pwani  na Lindi; Huduma za afya kwa vijiji Jirani vya Kisaki na Mloka; Chanzo cha uhakika cha mapato ya Serikali.

 

JNHPP ni miongoni mwa mabwawa 70 makubwa duniani na miongoni mwa mabwawa 4 makubwa Afrika. Ni mradi wa pili barani Afrika kuzalisha umeme mwingi (MW 2115) baada ya GERD ya Ethiopia itakayozalisha takribani MW 5000.

 

Changamoto na Matarajio:

 

Mto Rufiji ndio chanzo pekee cha maji kwa bwawa hilo. Vyanzo vikuu vya Mto Rufiji ni mito mitatu. Wa kwanza ni Mto Kilombero, ambao una eneo la bonde la kilomita za mraba 40,389 sawa na asilimia 25 ya eneo lote la vyanzo vya maji la mradi wa JNHPP. Mto huu huchangia takribani mita za ujazo bilioni 13.8 za maji kwa mwaka, sawa na asilimia 65 ya maji yanayoingia kwenye Mto Rufiji.

 

Wa pili ni Mto Luwegu, ambao una eneo la bonde la kilomita za mraba 25,365, sawa na asilimia 16 ya eneo la vyanzo vya maji la JNHPP. Mto huu huchangia takribani mita za ujazo bilioni 4 za maji kwa mwaka, ambayo ni takribani asilimia 19 ya maji yanayoingia kwenye Mto Rufiji.

 

Wa tatu ni Mto Ruaha Mkuu (Great Ruaha River), ambao una eneo la bonde la kilomita za mraba 85,571, sawa na asilimia 54 ya eneo la vyanzo vya maji la JNHPP. Mto huu huchangia takribani mita za ujazo bilioni 3.3 za maji kwa mwaka, sawa na asilimia 15 ya maji yanayoingia kwenye Mto Rufiji. Asilimia 1 iliyosalia ya maji inatokana na vijito mbalimbali vya maji.

 

Eneo lote la vyanzo vya maji la mradi linakadiriwa kuwa kilomita za mraba 158,420, likihusisha mikoa kumi (10) ya Tanzania: Pwani, Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora, Mbeya, Njombe, Iringa, Ruvuma na Lindi. Pia linajumuisha wilaya ishirini na tisa (29): Chunya, Iringa Vijijini, Iringa Mjini, Njombe Mjini, Njombe, Tunduru, Mbeya, Mbeya Mjini, Mpwapwa, Bahi, Mufindi, Songea, Wanging’ombe, Makete, Manyoni, Chamwino, Kilolo, Liwale, Rungwe, Sikonge, Ulanga, Dodoma Mjini, Ikungi, Namtumbo, Rufiji, Mbarali, Morogoro, Kilombero na Kilosa.

 

Aidha, eneo hilo linahusisha hifadhi za wanyamapori na mbuga za taifa nane (8): Selous, JNNP, Mikumi, Udzungwa, Ruaha, Rungwa, Kizigo na Muhesi.

 

Kukamilika kwa Ujenzi wa Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ni ushahidi wa uwezo wa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Rais Dkt samia Suluhu Hassan kupitia Kazi kubwa ya kizalendo iliyofanywa na wasimamizi wazawa kwa shirika la umeme Tanzania -TANESCO kuiteua Wakala ya Barabara Tanzania -TANROADS kuwa Mshauri Elekezi na msimamizi wa mkataba na ujenzi wa mradi. Ambapo TANROADS ilielekeza ushauri elekezi na usimamizi wa mkataba na ujenzi wa mradi utekelezwe na kitengo chake tanzu cha ushauri elekezi yaani TANROADS Engineering and Consulting Unit (TECU).

 

Mradi huu ni miongoni mwa miradi mikubwa zaidi ya miundombinu kuwahi kutekelezwa nchini. Ikiwa ni pamoja na Kuongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme wa uhakika wa megawati 2,115, hivyo kuongeza uwezo wa taifa kufikia zaidi ya Megawati 3,500. Kuharakisha maendeleo ya viwanda utakaopelekea Uzalishaji wa bidhaa kwa gharama nafuu, Kupunguza utegemezi wa vyanzo vya gharama kubwa kwani Umeme wa maji ni rafiki kwa mazingira na wa gharama nafuu ukilinganishwa na umeme wa mafuta.

 

Pia mradi huu utapunguza matumizi ya jenereta na mafuta ya dizeli, na kupunguza kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa hewa na gharama za uendeshaji, Kukuza uchumi na kuvutia uwekezaji, kupatikana kwa Umeme wa uhakika, Kuimarika kwa sekta mbalimbali kama kilimo cha umwagiliaji, biashara, na TEHAMA lakini pia Kutoa ajira na kukuza ujuzi wa kitaifa.

 

Katika mradi huu utakumbuka kuwa Maelfu ya Watanzania walipata ajira za muda na za kudumu wakati wa ujenzi. Mafundi, wahandisi na wataalamu wa ndani walishiriki moja kwa moja, Mradi umeboresha miundombinu ya maeneo ya jirani kwa kuchangia Ujenzi wa barabara, daraja, na miundombinu ya kijamii katika maeneo ya karibu kama Morogoro, Lindi, na Pwani.

 

Huduma za kijamii kama shule, maji safi, na afya viliboreshwa kutokana na uwepo wa mradi lakini umethibitisha uwezo wa Tanzania kusimamia miradi mikubwa, Kuwezesha usambazaji wa umeme vijijini na Kuinua kipato cha wananchi kupitia shughuli za kiuchumi.

 

Serikali ya Tanzania inajivunia JNHPP kama alama ya maendeleo, urithi wa kizazi kijacho, na nguzo ya uchumi wa viwanda. Mradi huu ni mfano wa kujitegemea, uzalendo, na dira ya maendeleo ya Taifa kwa kutumia rasilimali za ndani.

 

Tanzania sasa imeandika historia. Kwa fedha zetu, kwa wataalamu wetu, na kwa moyo wetu

 

Kutoka maono ya jana hadi uhalisia wa leo – Huu ni ushindi wa watanzania

 

MWISHO

No comments:

Post a Comment