Na Meleka Kulwa – Dodoma
Mkurugenzi wa Miradi wa Habitat for Humanity Tanzania, John Massenza, amesema ujenzi wa vyumba vya vyoo vya kisasa katika minada ya Bahi na Kigwe utakapokamilika, utaimarisha mazingira ya biashara, afya, na usafi kwa wafanyabiashara pamoja na wananchi wanaotumia minada hiyo wilayani Bahi, jijini Dodoma.
Ziara ya kukagua na kukabidhi maeneo ya ujenzi ilifanyika Desemba 16, 2025, ambapo John Massenza amekabidhi rasmi maeneo ya miradi hiyo kwa wahandisi watakaotekeleza ujenzi wa vyumba vya vyoo katika minada ya Bahi na Kigwe.
Amesema kuwa katika mradi huo, kutajengwa majengo ya vyoo pamoja na miundombinu rafiki kwa wanawake, ikiwemo jengo maalumu litakalowawezesha wakina mama kujisitiri wanapokuwa na mahitaji maalumu.
Aidha, amesema kuwa katika minada ya Bahi na Kigwe kutajengwa jumla ya vyumba 26 vya vyoo, vikiwemo vyumba 10 kwa wanaume na 16 kwa wanawake, pamoja na tanki la maji kwa kila mradi. Miradi hiyo pia itajumuisha chumba maalumu cha mahitaji ya wanawake, bafu, chumba cha wakina mama wanaonyonyesha, pamoja na ofisi ya wasimamizi wa huduma.
Amebainisha pia kuwa vyumba viwili kwa kila mradi vitajengwa kwa ajili ya watu wenye ulemavu katika minada ya Bahi na Kigwe.
Aidha, amebainisha kuwa mradi wa ujenzi wa vyumba vya vyoo katika Mnada wa Bahi utagharimu shilingi milioni 60, huku mradi wa Mnada wa Kigwe ukigharimu shilingi milioni 60 pia. Miradi hiyo inatarajiwa kunufaisha zaidi ya watu 4,000 pindi itakapokamilika.
Katika mpango wa uendeshaji wa huduma hizo, amesema kuwa watumiaji wa vyoo watalipia huduma hiyo kwa lengo la kugharamia matengenezo, uendeshaji wa mradi pamoja na kuboresha makazi ya wananchi na kuinua vipato vyao.
Amebainisha kuwa utekelezaji wa miradi hiyo unalenga kuboresha afya na ustawi wa jamii, kuongeza kipato, na kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja kupitia mazingira bora ya biashara na huduma.
Habitat for Humanity inafanya kazi katika nchi 70 duniani, huku makao makuu yake yakiwa nchini Marekani. Aidha, Massenza amesema kuwa mradi huo ni sehemu ya jitihada za taasisi hiyo katika kuboresha huduma za vyoo na usafi wa mazingira katika maeneo ya minada na jamii kwa ujumla.
Katika ziara hiyo, Mkurugenzi wa Habitat for Humanity Tanzania, John Massenza, aliambatana na viongozi wa serikali ya kijiji na mtaa pamoja na maafisa mazingira kutoka Wilaya ya Bahi.
Awali, mhandisi wa mradi alisema kuwa tanki la maji litakuwa na ujazo wa lita 3,000, kwa Kila tank litakalokuwepo kwenye miradi hio, huku akibainisha kuwa ujenzi wa majengo hayo ukitarajiwa kuchukua wiki 8 hadi 10, na kwamba mradi mzima unatarajiwa kukamilika ndani ya siku 90.
No comments:
Post a Comment