Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), wamezindua Tuzo ya SAMIA KALAMU AWARDS yenye kubeba kauli mbiu ya “UZALENDO NDIO UJANJA”.
Tuzo hizo zitatolewa kwa wanahabari watanzania kwa lengo la kuhamasisha, kuhimiza na kukuza wigo wa uchakataji, utangazaji na uchapishaji wa maudhui ya ndani kupitia vyombo vya habari.
Aidha, utoaji wa Tuzo hizi umelenga kuchochea uandishi wa makala zilizofanyiwa utafiti na uchambuzi kuhusu maendeleo, uwajibikaji, uzalendo na kujenga chapa na taswira ya nchi.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA Dkt. Rose Reuben leo tarehe 13 Octoba 2024 katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Serena Jijini Dar es salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari na kubainisha kuwa Tuzo hizo zitahusisha maudhui yaliyochapishwa kupitia magazeti, redio, televisheni, majukwaa ya mtandaoni, Tuzo maalumu kwa vyombo vya habari na maafisa habari wa Serikali.
Pia Dkt Rose Tuzo hizo zinahusisha habari zilizochapishwa kati ya Januari 01 hadi Oktoba 26, 2024 na kueleza kuwa Tuzo hizo zimepewa jina la SAMIA KALAMU AWARDS ili kutambua na kuenzi historia ya kuwa na Rais wa kwanza mwanamke nchini na zinatarajiwa kutolewa Novemba, 2024.
Ameeleza kuwa Kutokana na Maendeleo ya tekinolojia na utandawazi uandishi wa habari nchini umekua ukijikita kwenye kuburudisha, kuhabarisha huku uandishi wa makala za kuelimisha zikiwa kwa kiwango kidogo ambapo vyombo vyingi vya habari nchini vimekuwa vikitangaza maudhui ya nje yasiyokidhi mahitaji ya hadhira ya kitanzania.
Kwa muktadha huo, TAMWA kwa kushirikiana na TCRA tiliamua kutoa mafunzo maalumu kwa waandishi wa habari, watangazaji, wahariri, mameneja, maafisa habari, wamiliki wa vyombo vya habari, wahadhiri na watengeneza maudhui ya mitandaoni wapatao 2,054 kote nchini, kwa kipindi cha miezi mitatu.
Tuzo hizo zimegawanyika katika makundi matatu ambayo ni Tuzo Maalumu za Kitaifa, Tuzo kwa Vyombo vya Habari na, Tuzo za Kisekta ambapo amelezo ya kina yanapatikana kupitia tovuti ya https://samiaawards.tz
Dkt Rose amebainisha kuwa vigezo vitakavyotazamwa ni Makala ziwe zinahusu masuala ya maendeleo yanayogusa maisha ya wananchi na fursa zinazopatikana kutoka kwenye miradi mbalimbali.
Makala hizo ziwe zimechapishwa, kutangazwa au kurushwa kwa lugha ya Kiswahili au Kiingereza kwenye vyombo vya habari vya ndani au nje ya Tanzania. Aidha, mwandishi lazima awe Mtanzania na makala iwe imefanyiwa utafiti na uchambuzi wa kina. Vyanzo vya habari visipungue vinne na makala hazipaswi kuwa zimeshawahi kushindanishwa kwenye tuzo nyingine. Kwa kuzingatia ulinzi wa haki miliki, kazi zote zitakazowasilishwa kwa ajili ya mashindano ni lazima ziwe za kipekee na zifuate masharti ya haki-miliki ya mwandishi na kituo kilichozitangaza.
Mchakato wa upigaji kura utahusisha wananchi kwa asilimia 60 na majaji kwa asilimia 40. Kura zitapigwa kupitia SMS SHORT CODE namba 15200 kupitia simu, na kutumia tovuti ingia link hii https://samiaawards.tz
Meneja wa huduma za utangazaji-TCRA Mhandisi Andrew Kisaka akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania-TCRA Dkt. Jabiri Bakari amesema kuwa lengo la tuzo hizo pia ni kuhakikisha waandishi wa habari wanaandika makala zenye maudhui bora na zenye kuleta mabadiliko.
“Hizi ni tuzo za kipekee kwa sababu vyombo vya habari vyote vitashindishwa, maafisa habari nao watashindanishwa. Zitaleta matokeo chanya katika tasnia ya habari, Tunataka waandishi wa habari wanaoandika habari zenye kuleta mabadiliko “Quality local contents lengo ni kuongeza kiwango bora cha maudhui ya ndani", Amekaririwa Mhandisi Kisaka
MWISHO
No comments:
Post a Comment