Na Saida Issa,Dodoma
Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia TANAPA kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Mbeya imepanga kuweka vigingi kwenye mpaka wa hifadhi kwa umbali wa kilometa 82 katika Mwaka wa Fedha 2024/2025 ili kurahisisha utambuzi wa mipaka ya Hifadhi na Vijiji.
Haya yamebainishwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula alipokuwa akijibu swali la Mhe. Oran Manase Njeza(Mb) aliyataka kujua Serikali itamaliza lini mgogoro wa muda mrefu wa ardhi kati ya TANAPA, Kitulo/TFS na Wananchi wa Kata za Ilungu, Igoma na Inyala.
Mhe. Kitandula aliongeza kuwa Serikali kupitia Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Mbeya Vijijini na Uongozi wa Kata zinazopakana na Hifadhi ya Taifa Kitulo imefanya mikutano 15 kati ya tarehe 17 Mei, 2023 na 9 Novemba, 2023.
“Mikutano hiyo ililenga kutoa elimu kwa Wananchi juu ya umuhimu wa uhifadhi, dhana ya ujirani mwema na kuwashirikisha Wananchi katika juhudi za pamoja za kutambua mipaka ya Hifadhi kwa faida za hifadhi, jamii na Taifa kwa ujumla. Kufuatia mikutano hiyo, mgogoro huu umemalizika” alisema Mhe. Kitandula
No comments:
Post a Comment