NAIBU Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) amesema ili kutatua changamoto ya ukosefu wa miundombinu ya kusafisha na kutibu maji katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu Mkoani Kigoma, Serikali tayari imekamilisha ukarabati wa chujio la maji la Kabanga ambalo limeanza kufanya kazi.
Mhandisi Mahundi ameyasema hayo leo Februari 1 2024, bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la mbunge wa viti maalum Josephine Gezabuke aliyeuliza ni lini Halmashauri ya Mji wa Kasulu itaondokana na matumizi ya maji machafu kutokana na ukosefu wa chujio.
Mhandisi Mahundi amesema Chujio hilo la maji la Kabanga lina uwezo wa kuchuja maji jumla ya lita 1,000,000 kwa siku.
"Ujenzi wa machujio ya maji kutoka vyanzo vya Mto Chai na Miseno umeanza na unatarajiwa kukamilika ifikapo Mwezi Aprili, 2024, Machujio haya yatakuwa na uwezo wa kuchuja maji jumla ya lita 3,000,000 kwa siku.
"Kwa sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 15. Serikali kupitia mradi wa Miji 28 imeanza ujenzi wa chujio la maji kutoka Chanzo cha Maji cha Mto Ruchugi na kwa sasa mradi huo utekelezaji wake umefikia asilimia 5 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Aprili, 2025 ambapo Chujio hilo litakuwa na uwezo wa kuchuja maji jumla ya lita 15,000,000 kwa siku"amesema
Mwisho
No comments:
Post a Comment