Sunday, January 28, 2024

MAKONDA AMUWEKA KIKAANGONI RPC SHINYANGA


Na Mwandishi Wetu, shinyanga

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo  Paul Makonda amemuweka kikaangoni Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi kueleza alipo kijana Issa Hamis Issa anayedaiwa kupotea tangu Novemba 2022.

Aidha, amemuagiza Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ambaye pia ni Mbunge wa Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi kumsaidia mama wa kijana huyo kuonana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi ndani ya wiki moja ili kupata majibu alipo kijana huyo.

Hatua hiyo ya Makonda imekuja baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa mama wa kijana huyo kwenye mkutano wa hadhara akidai kuwa Issa alikuwa ni rafiki wa kamanda huyo na siku moja kabla ya kupotea alikwenda kutengeneza gari la Kamanda huyo.


Mama huyo alidai kuwa yeye na familia yake wamekuwa wakifuatilia suala hilo na walishafika ofisini kwa kamanda huyo lakini hakuna jibu lililopatikana na badala yake  alimfukuza mama huyo na kumwambia  aache usumbufu wa kulisumbua jeshi. 

"Kwa kweli tunashangaa sana jeshi la polisi kushindwa hata kufuatilia namba zake za simu na kujua ni wapi mara ya mwisho zilisoma hii sio sahihi kwani tunajua kwa sasa tulipofikia dunia ni kama kijiji jeshi linashindwa vipi kufuatilia mawasiliano na kupata suluhu kwa muda wote huo?,"alisema mama huyo. 

Aidha alisema kuwa anaimani na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kuwa ndio itakuwa mkombozi wake kwa kuwa amehangaika mwa muda mrefu kumtafuta mwanae na mpaka kupotea matumaini ya kumpata.

"Naomba leo RPC aseme mwanangu yupo wapi kama amekufa tuambiwe na kama yupo hai yupo wapi,"alisema.

Hata hivyo, Kamanda Magomi alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu suala hilo, alikiri kuwa na taarifa nalo huku akidai hamjui Issa na wala hakuwa rafiki yake.

Baada ya majibu hayo, Makonda alitoa maagizo hayo kwa Wizara na jeshi la polisi na kwamba CCM itahakikisha  inafuatilia suala hilo ili kujua nini kilitokea mpaka kupotea kwa kijana huyo kwa muda mrefu na familia bila kujua ukweli wowote wa chanzo cha kupotea ndugu yao.

"Nampatia mama huyu kiasi cha fedha kama nauli na kujikimu kwa kipindi watakachokuwa Dodoma kumtafuta Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge Katambi atahakikisha anawasaidia kumpata Waziri ili tujue suluhu na sisi chama lazima tutaendelea kulifuatilia hili ili tujue muafaka wake,"alisema Makonda.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment