📌 Shule mpya 30 za msingi zajengwa
📌 Kila Kata wilayani Bukombe sasa ina Shule ya Sekondari
📌 Barabara mpya zajengwa, mtandao wafikia kilometa 1400
📌 Bukombe sasa ina hospitali mbili, vituo vya afya sita, zahanati 18
📌 Apokea Wanachama wapya wa CCM, watokea CHADEMA
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Mhe. Dkt. Doto Biteko, amepongeza jitihada kubwa zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza kwa kasi miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani Bukombe ikiwemo Barabara, Shule na ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na hospitali.
Dkt. Biteko ametoa pongezi hizo wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara na Wananchi wa Kijiji cha Bukombe, Kata ya Bukombe, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita ikiwa ni sehemu ya ziara yake jimboni Bukombe. Viongozi mbalimbali walihudhuria mkutano huo wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella.
“Kama kuna mtu mmoja anatupenda Bukombe, ni Dkt. Samia Suluhu Hassan, na nitawaambieni kwa nini; sijawahi kwenda kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kumuomba suala lolote kuhusu maendeleo ya Bukombe akanikatalia, na leo nitawatajia baadhi ya mambo magumu ambayo tumehangaika nayo kwa miaka mingi, mnakumbuka kule Idoselo wananchi wenzetu walikuwa wakichapwa viboko wakiambiwa kuwa ni wavamizi wa Hifadhi, lakini Mama ndani ya mwaka mmoja akiwa madarakani, alilifanyia kazi suala hili kwa kuwarudisha wananchi Idoselo, akawajengea barabara na Shule, Mama huyu anatupenda na ametufanyia mambo makubwa sana.” Amesema, Dkt. Biteko
Dkt. Biteko pia amemshukuru Dkt.Samia kwa ujenzi wa Shule za elimu ya Sekondari ya Juu (High Schools) kutoka moja hadi tano, ujenzi wa shule za msingi kutoka 75 hadi 105 na kueleza kuwa, kila kata wilayani Bukombe sasa ina shule ya sekondari huku Chuo kikubwa cha Ufundi Stadi (VETA) kikiwa mbioni kujengwa.
Kuhusu mtandao wa barabara wilayani Bukombe, Dkt. Biteko amesema kuwa, kulikuwa na mtandao wa barabara kilometa 256, lakini Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha zilizowezesha kujengwa kwa barabara mpya na kwa sasa mtadao wa barabara wilayani humo umefikia kilometa 1,400.
Katika Sekta ya Afya, Dkt. Biteko amesema kuwa, jitihada mbalimbali zimefanyika kwani kulikuwa na hospitali moja ya wilaya, vituo vya afya viwili na zahanati nne pekeyake, lakini kwa sasa kuna hospitali mbili, vituo vya afya sita, zahanati 18 na ujenzi wa zahanati nyingine 57 unaendelea katika maeneo mbalimbali wilayani Bukombe.
Akiwa katika Kijiji cha Bukombe, Kata ya Bukombe, Dkt. Biteko ameahidi kuweka taa za barabarani, kujenga kisima cha maji katika Shule ya Sekondari kwenye Kata hiyo na kukamilisha hatua za mwisho za ujenzi wa zahanati kwenye Kata hiyo ili wananchi wapate huduma bora.
Ametoa wito kwa wananchi wa Bukombe kumuunga mkono Rais, Dkt. Samia na kumuombea ili aendelee kuiletea nchi maendeleo.
Katika hatua nyingine, Dkt. Doto Biteko amepokea Wanachama wapya wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakitokea Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambao walieleza kuwa wamefanya uamuzi huo kutokana na kujionea jitihada mbalimbali zinazofanywa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuwaletea maendeleo wananchi wilayani Bukombe ikiwemo ujenzi wa barabara, Shule, umeme n.k
Baada ya kupokea Wanachama hao, Dkt. Biteko amewakaribisha ndani ya CCM akieleza kuwa, Chama hicho ni cha watu wote, kinachowaangalia watanzania na kuwaza maendeleo yao, hivyo amewaasa kuwa wakiwa ndani ya CCM, wajifunze mila na desturi ikiwemo, kusikilizana, kuvumiliana, kuheshimiana na kupendana huku wakati wote mawazo yao yakiwa ni kuwapelekea wananchi maendeleo.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella, alitaja baadhi ya miradi iliyotekelezwa mkoani Geita chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambapo alieleza kuwa, madarasa mapya zaidi ya 2500 yamejengwa ambayo yamegharibu zaidi ya shilingi bilioni 65, ujenzi wa shule mpya zaidi ya 87 na katika suala la umeme amesema kuwa, katika vijiji 486 mkoani humo, vijiji 53 tu havina umeme huku kazi ya kupeleka umeme kwenye vijiji hivyo ikiendelea.
No comments:
Post a Comment