Saturday, December 23, 2023

BASHUNGWA AWANYOOSHEA KIDOLE VIONGOZI WAORUDISHA NYUMA MAENDELEO KAGERA


Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa ameendelea kuwanyooshea kidole baadhi ya Viongozi wanaochangia kurudisha nyuma maendeleo ya mkoa wa Kagera na kutoa wito kwa Wananchi wa mkoa huo kusimama kidete katika umoja kwa kuhakikisha wanabadilisha historia iliyopo katika mkoa.

Ameyasema hayo mjini Bukoba wakati hafla ya Chakula cha jioni ya “Ijuka Omuka” iliyoandaliwa na Mkuu wa Mkoa Kagera, Hajjat Fatma Mwassa iliyolenga kuwakutanisha Wanakagera wanaoishi ndani na nje ya nchi.

“Nakushukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuandaa jukwaa hili la kujikosoa na kujisahihisha. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuwa mkoa wa Kagera alituelekeza kufanya hili tunalolifanya leo la kujadili mustakabali wa mkoa wetu” - amesema Bashungwa.

Bashungwa ameeleza kuwa maendeleo ya mkoa wa Kagera yamekuwa yakirudishwa nyuma na baadhi ya viongozi na wanasiasa  ambao wamekuwa wakipambania maslahi yao binafsi na kukwamisha maendeleo ya mkoa.

“Viongozi wamekuwa wakija ndani ya mkoa wetu na kutoa nafasi ya kutusikiliza, lakini kuna baadhi ya viongozi wanatoa hoja binafsi na sio hoja za kuleta maendeleo katika mkoa, ikiwa ni pamoja na mambo yao binafsi na kesi zinazorudisha maendeleo yetu nyuma”- amesisitiza Bashungwa.

Aidha, Bashungwa amesema pamoja na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoa fedha za kutekeleza miradi katika mkoa wa Kagera kama Ujenzi wa barabara ya njia nne, stendi ya kisasa na upanuzi wa bandari, bado kumekuwepo na viongozi wanaoendelea kukwamisha utekelezaji huo.

Ameeleza baadhi ya matukio yaliyochangia kudumaza maendeleo ya mkoa kiuchumi, kijamii na kisiasa ni pamoja na Vita, milipuko ya magojwa, majanga ya asili kama tetemeko na mabadiliko ya tabianchi.

Kadhalika, Bashungwa ameeleza kuwa kumekuwepo na tafiti zinazoendelea kuudidimiza mkoa wa Kagera kwa kuutafsiri Mkoa huo katika dhana isiyo sahihi na hali halisi iliyopo.

Kwa Upande wake, Mkuu wa Mkoa Kagera Fatma Mwassa amesema Mkoa huo hauwezi kuendelea bila ushirikiano kwa kupingana kwa kila jambo, kuwekeana figisu na mikingamo bali mkoa utafanikiwa kwa kuwa na umoja madhubuti.

No comments:

Post a Comment