Friday, December 1, 2023

BASHUNGWA ATOA SIKU 7 KWA CRG7 KUJA NA MPANGO KAZI WA KUKAMALISHA MIRADI

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ametoa siku saba kwa Mkandarasi Kutoka China, China Railway Seventh Group Ltd (CRG7) kuwasilisha Wizarani mpango kazi wa miradi mitano anayoitekeleza hapa nchini kutokana na utekelezaji wa miradi yote kusua sua na ipo nyuma ya muda kulingana na mikataba.

Ametoa maelekezo hayo leo tarehe 01 Disemba 2023 wakati alipokutana na Uongozi wa juu wa Kampuni hiyo, ulioongozwa na Mkurugenzi mkuu Msaidizi wa Kamapuni ya CRG7 Kutoka China, ndugu Xianyang Dong.

Bashungwa amemtaka Mkurugenzi mkuu huyo wa CRG7 kuhakikisha anawasilisha kwake Mpango kazi wa kila Mradi na namna alivyojipanga kukamilisha, kutokana na kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi yote mitano waliyopewa kujenga hapa nchini.

Ameeleza kuwa Mkandarasi CRG7 anatekeleza miradi mitano ambayo ni Ujenzi wa Kiwango cha lami barabara ya Amanimakoro - Ruanda km 35 iliyopo mkoani Ruvuma ambapo utekelezaji wake ulitakiwa kuwa asilimia 92 lakini sasa umefikia asilimia 24.

Bashungwa ameeleza mradi mwingine ni ujenzi wa Kiwango cha lami barabara ya Sanzate - Natta km 40 iliyopo mkoani Mara ambapo walitakiwa kuwa asilimia 99 lakini sasa hivi wamefikia asilimia 41.

Aidha, Ameeleza Ujenzi wa Kiwango cha lami barabara ya Kibaoni - Mlele junction km 50 iliyopo mkoani Katavi ambapo walitakiwa kuwa asilimia 26 lakini sasa wamefikia asilimia 12.

Amebainisha miradi mingine ambayo utekeleaji wake haujaanza ni barabara ya Nyamwage - Utete km 33.7 mkoani Pwani, Ujenzi wa Daraja la mpiji chini na barabara unganishi ya km 2.3 vilivyopo mkoa Dar es Salaam.

Kadhalika, Bashungwa amemuagiza Mtendaji Mkuu wa TANROADS kuondokana na hali ya kutoa miradi mingi ya ujenzi kwa Mkandarasi mmoja, jambo linalosababisha miradi kushindwa kutekelezwa kwa wakati kulingana na mikataba.

Bashungwa ameeleza kuwa Serikali inayongozwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan haitamvumilia Mkandarasi yoyote anayeshindwa kuteleleza miradi kwa wakati, Kutoka na sababu zozote ambazo zinakwamisha Utekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

1 comment:

  1. Sehemi nyingi kunasababishwa na wizi wa mafuta na vipuri vinavyofanywa na baadhi ya madereva wazawa wasio waminifu. Ulazima wa wakandarasi kutoa ajira kwa wazawa kunaathiri Kasi na hatimae yubora wa miradi hii

    ReplyDelete