Wednesday, November 8, 2023

REA YATENGA BILIONI 10 KUSAMBAZA MITUNGI YA GESI VIJIJINI

 Na Veronica Simba – REA

Wakala wa Nishati Vijijini (REA), katika Mwaka huu wa Fedha (2023/24), umetenga shilingi bilioni 10 kwa ajili ya kusambaza mitungi ya gesi ya LPG, majiko na vifaa vyake katika maeneo ya vijijini kwa njia ya ruzuku.

Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy ameyasema hayo wakati akiwasilisha Taarifa ya Wakala kwa Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, Novemba 7, 2023.

Alisema kuwa, kiasi cha mitungi kati ya 200,000 hadi 500,000 inatarajiwa kusambazwa katika maeneo ya vijijini kutegemea kiwango cha ruzuku kitakachotolewa.

Akielezea Mradi wa usambazaji gesi ya kupikia kwa ujumla, Mhandisi Saidy alisema unategemewa kusambaza mitungi ya gesi 70,020 ambapo hadi kufikia Agosti 15 mwaka huu, mitungi 23,806 (sawa na asilimia 34) ilikuwa imeshasambazwa kwa wananchi mbalimbali kupitia kwa Wabunge ambao ni wawakilishi wao.

“Lengo la Serikali kupitia REA katika utekelezaji wa Mradi huo ni kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia katika maeneo yao,” alifafanua.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu alieleza kuwa, katika hatua nyingine, REA inatekeleza Mradi wa usambazaji gesi asilia kwa ajili ya kupikia katika mikoa ya Lindi na Pwani kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), ambapo alisema Mkataba umesainiwa na maombi ya fedha za awali, yapo Wizara ya Fedha kwa ajili ya uhakiki.

“Mkataba huu una jumla ya shilingi bilioni 6.8 ambapo unatarajiwa kuunganisha wananchi 980 na nishati ya kupikia katika maeneo ya Mnazi Mmoja mkoani Lindi na Mkuranga mkoani Pwani.”

Alisema kuwa, katika Mwaka huu wa Fedha (2023/24), REA imetenga shilingi bilioni 18.5 kwa ajili ya kuiwezesha TPDC kujenga miundombinu ya kusambaza gesi asilia katika maeneo yaliyopo pembezoni mwa Mkuza wa Bomba Kuu la kusafirisha gesi asilia linalopita katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani ili wananchi wanaoishi kwenye maeneo hayo waweze kutumia gesi asilia kwa ajili ya kupikia.

Mkurugenzi Mkuu pia alieleza kuhusu Mradi wa ufungaji mifumo ya kupikia katika taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 300 ambapo alisema Wakala unalenga kujenga mifumo hiyo kwa Taasisi 100.

Akifafanua, alisema kuwa Mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa wakati akifungua Kongamano la Nishati ya Kupikia jijini Dar es Salaam, Novemba 2022.

Kuhusu usambazaji wa majiko banifu, alieleza kuwa kupitia ruzuku ya Dola za Marekani milioni sita iliyotolewa na Benki ya Dunia, Serikali kupitia REA inatarajia kusambaza majiko banifu 70,000 yaliyotengenezwa kwa teknolojia yenye ubunifu wa kupunguza matumizi ya kuni na mkaa pamoja na kupunguza uharibifu wa mazingira.

Naibu Waziri Kapinga alitembelea Makao Makuu REA jijini Dodoma na kuzungumza na Menejimenti yake ikiwa ni mara ya kwanza tangu ateuliwe kushika wadhifa huo.

No comments:

Post a Comment