Serikali kupitia wizara ya madini imeweka mkakati wa kuhakikisha inatatua mgogoro wa muda mrefu uliodumu zaidi ya miaka 20 tangu kuanza kwa shughuli za uchimbaji madini kati ya wananchi na mgodi unaomilikiwa na Kampuni ya Geita Gold Mine (*GGM*).
Hayo yamesemwa leo tarehe 12 Oktoba, 2023 na Waziri wa Madini, *Mheshimiwa Anthony Peter Mavunde (Mb)* Mkoani Geita alipofanya ziara ya kikazi kutembelea maeneo yenye mgogoro wa vigingi na mipasuko baina ya wananchi na mgodi wa GGM.
"Lazima tukiri kwamba mgogoro huu umedumu kwa muda mrefu, na ndo maana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu* Hassan ambaye ndiye msingi wa mimi kuja hapa amenielekeza kufika hapa kutembelea maeneo yenu na kuwasikiliza ili kupata uhalisia wa mgogoro huu"
"Kipekee kabisa, naomba nimshukuru kwa dhati mtangulizi wangu ambaye kwa sasa ni *Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko (Mb)* kwa kazi nzuri ambayo alishaianza katika jambo hili. Kupitia kazi yake, imenifanya mimi kupata mahali pa kuanzia na kazi yangu kuwa nyepesi kuelekea kupata ufumbuzi wa mgogoro huu" alieleza Mhe. Mavunde.
Katika maeneo yote ya Nyakabale, Nyamilembo,Samina na Katoma alikotembelea, Mheshimiwa Mavunde alibainisha kwamba amepata fursa ya kuona hali halisi ya mgogoro huo, na kuahidi kwamba *Mheshimiwa Rais* amemuagiza kwamba anataka kuona mgogoro huo unafika mwisho.
Vilevile, Mavunde alipongeza jitihada na kazi nzuri iliyofanywa na *Mkuu wa Mkoa wa Geita*, *Mbunge wa Geita Mjini* na *Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Geita* kwa namna wanavyoendelea kutoa ushauri na kupigania ili kuhakikisha mgogoro huo unatatuliwa. Aidha, alisisitiza kwamba kwa kuwa maoni ya Kamati ya Wataalam, Kamati ya wananchi na GGM alikwisha yaona, aliona ni jambo jema yeye mwenyewe kufika kujionea hali halisi kabla ya kufanya maamuzi ya mwisho.
Akihitimisha maelezo yake, Mheshimiwa Mavunde aliwashukuru wananchi kwa ushirikiano wao na kutoa maoni yao kwa uwazi na kuahidi kwamba anakwenda kuhakikisha ndani ya *Mwezi mmoja* kuanzia tarehe ya leo mgogoro huo unakwenda kupata utatuzi wa kudumu baada ya kikao cha mwisho kati ya Wabunge, Uongozi wa Mkoa, Wananchi na GGM.
Akieleza kwa niaba ya wananchi wake, Mbunge wa Geita Mjini, *Mheshimiwa Constantine Kanyasu* alionesha namna Serikali inavyoendelea kusikiliza kilio cha wananchi hao na kupongeza hatua iliyofikiwa kwa sasa ambayo anaona ni muhimu katika kumaliza mgogoro.
Naye *Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mheshimiwa Martine Shigela* aliwashukuru wananchi kwa kuwa wavumilivu wakati wote ambao Serikali inafuatilia mgogoro huo, na kuwaomba wananchi kuiamini Serikali kwani inakwenda kutatua mgogoro huo kwa ueledi mkubwa.
No comments:
Post a Comment