Monday, October 23, 2023

MKURUGENZI REA ABAINISHA MIKAKATI UTEKELEZAJI MIRADI YA UMEME VIJIJINI, RAIS SAMIA APONGEZA




Na Dotto Mwaibale, Singida

NISHATI ya Umeme kwa wanadamu ni muhimu katika maendeleo ya nchi na taifa kwa ujumla na ni hitaji la kuaminika  hasa pale bei yake inapokuwa nafuu.

Nishati hiyo inaweza kuboresha na hata kuokoa maisha, nishati ya kuaminika inasaidia tasnia iliyopanuliwa kama kilimo cha kisasa, kuongezeka kwa biashara na uboreshaji wa usafirishaji.

Matumizi ya nishati ya umeme yamegawanyika katika sekta nne za kiuchumi ambazo ni makazi, biashara, usafirishaji na viwanda.

Kazi nyingine ya nishati ya umeme ni kupasha joto na kuweka ubaridi katika nyumba, kuwasha majengo ya ofisi, kuendesha magari na mizigo inayosonga, na kutengeneza bidhaa tunazozitegemea katika maisha yetu ya kila siku.

Nikutokana na umuhimu wa nishati hiyo hapa nchini  Oktoba 17, 2023 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan aliridhia ombi la kuzindua uwashaji umeme katika vijiji takribani 131 mkoani Singida kupitia mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili katika Kata ya  Shelui Wilaya ya Iramba uliotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Rais Samia aliipongeza REA na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kazi kubwa ya kusambaza umeme mkoani hapa ambapo alisema hadi ifikapo Mwezi Juni, 2024 Mkoa wote wa Singida utakuwa umemepata umeme katika maeneo yote.

Katika uzinduzi huo Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy alipata fursa ya kuelezea mikakati mbalimbali ya utekelezaji wa miradi hiyo ambapo kwa niaba ya Bodi ya Nishati Vijijini na watumishi wenzake wa REA walimkushukuru Rais Dkt.Samia kuridhia ombi la kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo.

Mhandisi Saidy anaanza kwa kusema Wakala wa Nishati Vijijini ni taasisi ya umma iliyo chini ya Wizara ya Nishati yenye jukumu la kuwezesha upatikanaji wa Nishati Bora maeneo ya vijijini ikiwemo Nishati ya Umeme. Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007, Wakala wa Nishati Vijijini kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) umesaidia kuongeza hali ya upatikanaji umeme vijijini kwa upande wa Tanzania Bara kutoka asilimia 5% mwaka 2007 hadi 70% mwaka 2020 (ambapo tathmini ya mwisho ilifanyika).

Anasema kupitia miradi mbalimbali ya umeme vijijini, Serikali kupitia Wakala wa Nishati imeweza kufikisha huduma za umeme katika vijiji 10,987 sawa na asilimia 89 ya vijiji vyote 12,318 vilivyopo Tanzania Bara.

“Kwa upande wa vitongoji, kati ya vitongoji 64,760 vilivyopo nchini, vitongoji 28,659 sawa na asilimia 44 vishafikiwa na huduma ya umeme. Serikali inaendelea na mipango ya kuongeza mafungu katika Mfuko wa Nishati Vijijini ili kuongeza kasi ya kufikisha umeme katika vitongoji 36,101 vilivyobaki kupitia Mpango wa Kufikisha Umeme Vitongoji Vyote (Hemlet Electrification Project-HEP),” anasema Saidy.

Aidha, Saidy anasema Tanzania chini ya Serikali inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imeendelea kupiga hatua kubwa katika kufikisha nishati bora vijijini kama njia ya kuboresha maisha ya wananchi, kuwezesha shughuli za uzalishaji mali zikiwemo biashara, viwanda na kilimo pamoja na kuboresha huduma za jamii zikiwemo afya, elimu, maji, mawasiliano.

Anasema zaidi ya shughuli za uchumi na huduma za jamii, umeme vijijini umesaidia; kuboresha ulinzi, kuhifadhi mazingira, kuimarisha usawa wa kijinsia pamoja na kuchangia azma ya serikali katika kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) ambapo upatikanaji wa Nishati bora utasaidia kufikia malengo 13 kati ya malengo 17.

“ Hivi tunavyoongea Serikali inatekeleza miradi mikubwa Saba (7) ya kupeleka umeme maeneo ya vijijini kupitia kandarasi 112 (Contract/Lots) ambayo kwa ujumla wake itapeleka umeme katika vijiji na vitongoji takribani 11,000 kwa gharama ya Sh.Bilioni 2,768. Miradi hiyo ni pamoja na:

  1. Miradi wa Ujazilizi Awamu ya Pili A (mioa 9), 2B (Mikoa 9) na 2C (Mikoa 7) ambayo itafikisha huduma za umeme katika vitongoji 4,895 katika mikoa 25 ya Tanzania bara kwa gharama za Sh.Bilioni 654.
  2. Mradi wa kusambaza umeme katika maeneo 808 (mitaa na vitongoji) yaliyopo pembezoni mwa miji (vijiji miji) ambayo inatekelezwa katika mikoa 13 kwa gharama ya Sh.Bilioni 189.4.
  3. Ujenzi wa Vituo Vya Kupoza Umeme eneo la Ifakara (Ifakara Substation) na Mtera (mtera Substation) vyenye uwezo wa 20MVA kila kimoja pamoja na mifumo ya kusambaza Umeme Vijijini kwa wilaya za Kilombero na Ulanga mkoani Morogoro na mikoa ya Iringa, Dodoma, Shinyanga na Tabora ambapo vijiji 136 vimefikishiwa huduma kwa gharama ya Sh. Bilioni 82.
  4. Mradi wa Kusambaza Umeme Katika Migodi Midogo, Maeneo ya Kilimo na Viwanda; 336 yaliyopo maeneo mbalimbali hapa nchini kwa gharama ya Sh.Bilioni 115
  5. Mradi wa Kusambaza Umeme Katika Vituo vya Afya na Pampu za Maji 460 maeneo mbalimbali katika mikoa yote kwa gharama ya Sh.Bilioni 34.5
  6. Mradi wa Kupeleka Umeme katika Vitongoji 654 Katika Mikoa ya Songwe na Kigoma (Hamlet Electrification Project I - HEP I) kwa gharama ya Sh. bilioni 100
  7. Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya III Mzunguko wa II (Turkey Phase III – Round II) unaotekelezwa kwa mafungu 39 ambapo vijiji 4071 katika mikoa 24 vitafikishiwa umeme kwa gharama ya Sh.1,593,” anasema Mhandisi Saidy.

Mhandisi Saidy anasema mradi huo Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya 3 Mzunguko wa 2 ndio unaenda kuhitimisha safari ya kufikisha miundombinu ya umeme katika vijiji vyote 12,318 Tanzania Bara kama ambavyo imeelekezwa katika Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 kuwa ifikapo mwaka 2025 vijiji vyote viwe vimefikiwa na huduma za umeme.

Anasema kati ya vijiji 4071 katika mradi huu, vijiji 2,740 vishafikiwa na huduma za umeme na vijiji 1,331 vilivyobaki, wakandarasi wanaendelea na shughuli za ujenzi ambao mpaka kufikia mwezi Juni 2024 mradi huo utakuwa umekamilika kwa mafungu yote 39 na hivyo kufanya vijiji vyote kufikiwa na huduma ya umeme kabla ya mwaka 2025.

Baada ya kukamilisha safari ya kufikisha umeme katika kila kijiji, na kwa kutambua kuwa ndani ya vijiji kuna vitongoji ambavyo havijafikiwa na huduma, Wakala unajipanga kutekeleza mpango mkubwa wa kufikisha umeme katika vijiji 10,000 ndani ya miaka 5 ambapo kwa kuanza, ndani ya mwaka huu wa fedha, serikali itatangaza zabuni ili kupata wakandarsi watakaojenga miundombinu ya kusambaza umeme katika vitongoji 3060 ambavyo ni wastani wa vitongoji 15 kwa majimbo yote 204 yaliyo maeneo ya vijijini.

Anasema Mkoa wa Singida una jumla ya vijiji 441. kati ya vijiji hivyo,  vijiji 397 sawa na asilimia 90% ya vijiji vyote katika mkoa huu vimeshapatiwa umeme kupitia miradi mbalimbali ya umeme vijijini.

Mhandisi Saidy anasema katika kuhakikisha vijiji vyote vinapata huduma za umeme, Serikali kupitia mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya 3 Mzunguko wa Pili imetenga Shilingi bilioni 71.6 ili kufikisha umeme katika vijiji 175 mkoani Singida.  Mradi huo unatekelezwa na wakandarasi wawili; kampuni ya Central Electricals International Ltd inatekeleza mradi kwa wilaya za Singida DC na Ikungi (amepewa vijiji 94 ambapo amewasha vijiji 70, vijiji 2 keshakamilisha kazi vinasubiri kukaguliwa na anaendelea na kazi katika 22), na CRJE-CTCE CONSORTIUM kwa wilaya za Iramba, Manyoni, Mkalama  (amepewa vijiji 81 ambapo amewasha vijiji 61, vijiji 3 kesha maliza kazi vinasubiri kukaguliwa na anaendelea na kazi katika 17) ambapo hadi kufikia Oktoba 15.2023 vijiji 131 vishafikishiwa huduma za umeme ambavyo leo unazindua rasmi uwashwaji wake na kuwa vijiji 5 kazi ishakamilika vinasubiri ukaguzi na 39 vilivyobaki vitafikiwa kabla ya kuisha mwezi Disemba mwaka huu (2023).

Mhandisi Saidy anasema  pamoja na mradi huo, Serikali pia inatekeleza miradi mingine Mitatu (3) katika mkoa wa Singida ambayo ni:

  • Mradi wa Kupeleka umeme Pembezoni mwa Miji (Peri-Urban III) ambapo maeneo 34 yatafikishiwa huduma za umeme (Sh.Bilioni 7.1)
  • Mradi wa Kupeleka umeme kwenye migodi midogo 22 (Sh.Bilioni 5.5)
  • Mradi wa kupeleka umeme kwenye Vituo vya Afya 5 na Pampu za Maji 23 kwa lengo la kuboresha huduma hizo pamoja na kuunga mkono jitihada za serikali katika kupambana na magonjwa ya kuambukiza (Sh.Bilioni 1.6) na jumla ya gharama ya miradi yote ni Sh. Bilioni 85.8.


Mhandisi Saidy  kwa niaba ya Bodi na Watumishi wenzake wa Wakala wa Nishati Vijijini alitumia nafasi hiyo kutoa shukrani kwa serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za kuwezesha utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini ambayo kama nilivyosema awali miradi ya takriban Sh. Trilioni 2.8 inatekelezwa nchi mzima.

Aidha, alimpongeza Rais Samia kwa, azma, maamuzi na jitihada zake za kuhakikisha nchi yetu inaondokana na matumizi ya Nishati isiyo salama na kuhamia katika Nishati Bora ya Kupika.

“Tunatambua jitihada zako hizo zimejengwa na dhamira yako ya dhati katika; kulinda afya za watanzania, kulinda misitu yetu, kuzuia mabadiliko ya tabia nchi, kuepusha unyanyasaji wa kijinsia, na kuwapa unafuu wa maisha, wananchi waishio vijijini hasa kina mama na watoto,” anasema  Saidy.

Anasema Wakala wa Nishati Vijijini zaidi ya miradi ya umeme, unawezesha pia upatikanaji wa Nishati Bora ya Kupikia Vijijini ambapo kwa mwaka huu wa fedha tunatekeleza miradi minne (4) ikiwemo; usambazaji wa mitungi ya gesi ya kupikia (LPG), usambazaji majiko banifu, ufungaji wa mifumo bora ya kupikia katika taasisi zaidi ya 100 zinazohudumia watu zaidi ya 300 pamoja na usambazaji wa gesi asilia kwa ajili ya kupikia katika mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara. Miradi hii ni endelevu na Wakala utaendelea kupanua wigo wa utekelezaji pamoja na aina za nishati kila mwaka kutegemea na upatikanaji wa fedha.

Mhandisi Saidy anasema  mwisho ila sio kwa umuhimu, wana mkushuru  tena Rais kwa kuendelea kuwaupa dhamana ya kuongoza taasisi hiyo muhimu ambapo pamoja na watumishi wenzake wa Wakala, wanafahamu ukubwa na umuhimu wa jukumu walilopewa na wanaahidi kuendelea kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na uadilifu ili kutimiza matamanio na azma yake ya kuona kila mtanzania hasa wa vijijini anafikiwa na huduma za nishati bora.

Anasema kwa kuzingatia hilo, Wakala wa nishati vijijni (REA) na kwa uongozi mzuri uliopo katika Wizara ya Nishati, wanamuhakikishia Rais Samia kuwa wataendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya nishati vijijini pamoja na kuwasimamia kwa karibu wakandarasi wote waliopewa zabuni ya kutekeleza miradi hiyo ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na wa ubora unaotakiwa ili iweze kuwanufaisha wananchi pamoja na taifa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment