Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imevifungia vituo viwili vya mafuta kwa muda wa miezi miezi sita kwa kosa la kuhodhi mafuta ili kujipatia maslahi haramu ya biashara ikiwemo faida kubwa kutokaba na ongezeko la bei za mafuta jambo ambalo ni kinyume na sheria, kanuni na miongozo inayosimamia biashara ya mafuta nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 10, 2023 Jijini Dar es Salaam, Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano EWURA Bw. Titus Kaguo, amesema kuwa vituo vilivyofungiwa ni Kituo cha Kipenda Roho Investment pamoja na Oilcom vilivyopo Soya, Wilaya ya Chemba Mkoani Dodoma.
Bw. Kaguo amesema kuwa uamuzi huo umekuja baada ya kikao cha Bodi ya Wakurugenzi ya EWURA kilichofanyika Oktoba 9, 2023 na kujiridhisha vituo hivyo vilitenda kosa la kuhodhi mafuta kati ya mwezi Julai na Agosti mwaka huu.
Amesema kuwa uamuzi wa Bodi ya Wakurugenzi hadi sasa utakuwa umegusa vituo tisa, huku akieleza kuwa uchunguzi unaendelea katika vituo vingine.
“EWURA inapenda kuwakumbusha wafanyakazi wote wa biashara ya mafuta nchini kuhakikisha wanaendesha biashara zao kwa mujibu wa sheria, kanuni, na miongozo inayosimamia biashara ya mafuta nchini” amesema Bw. Kaguo.
Bw. Kaguo ametoa onyo kwa OMCs na wamiliki wa vituo vya mafuta kuwa serikali inafuatilia suala hilo kwa ukaribu kupitia vyombo vyake na ikithibitika kuna uvunjaji wa sheria na kanuni umetendeka hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ikiwemo kuwafutia leseni za biashara.
Kwa mujibu wa Sheria ya Petroli, sura Na 392 EWURA ina jukumu la kuhakikisha upatikanaji wa mafuta wakati wote katika maeneo yote nchini.
Hata hivyo kuanzia mwezi Julai mwaka huu kumekuwepo na matukio kwa baadhi ya maeneo hasa pembezoni mwa nchi kukosa mafuta hasa kipindi bei zinapoelekea kubadilishwa na kusababisha kuwa na usumbufu makubwa kwa wananchi na madhara ya Kiuchumi.
Ili kufikia malengo EWURA inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kisheria ikiwemo kuvifungia baadhi ya vituo vilivyothibitika kufichua mafuta kinyume na kanuni na miongozo inayosimamia biashara ya mafuta nchini.
No comments:
Post a Comment