Friday, September 29, 2023

MBUNGE TAUHIDA ATOA MISAADA KWA WANAFUNZI KIDATO CHA NNE WALIOKO KAMBINI, AWAASA KUSHIRIKIANA

Zikiwa zimesalia siku chache kuelekea Mitihani  ya Kidato cha Nne Wanafunzi wa Kidato hicho wameaswa kutumia muda ambao wako Kambini kushirikiana na kuelekezana katika Masomo jambo ambalo litawapelekea kufanya vizuri katika mitihani yao.
   
 Wito huo umetolewa na Mbunge wa Viti Maalum-Zanzibar Mhe. Tauhida Gallos wakati alipofanya Ziara katika Kambi za maandalizi ya Mitihani ya Kidato cha Nne Mkoa wa Magharibi Visiwani Zanzibar ambapo pia ametoa misaada ya mahitaji mbalimbali itakayosaidia wanafunzi hao kujikimu kwa kipindi ambacho watakuwa kambini.
     
Mbunge Tauhida amewasisitiza wanafunzi hao kutokuwa na tabia ya choyo na badala yake watumie muda huo walioko kambini kuelekezana, kufundishana, na kusaidiana katika masomo yao ili kwa pamoja watimize ndoto zao.

"jipimeni sasa ,mkiwa na choyo,  jiulize mwenzio asipofahamu ikiwa wewe unakosa kumfahamisha siyo roho mbaya? kama una roho mbaya, una choyo unafaa kuwa Rais?, unafaa kuwa Daktari? huna huruma unawezaje kuwa Kiongozi? utaishia kutamani tu kwa kuhofia mwenzio atashika namba moja wewe utakuwa wa pili"

Amesema Divisheni wanazozitafuta ni kwaajili ya kuleta mafanikio mwisho wa siku kila mmoja ataenda upande wake, mwingine atakuwa Daktari na mwingine atakuwa Rais kisha mtakutana huko juu miaka ya mbele na wasioneane choyo na badala yake wahakikishe wanasaidiana
"Hakikisheni kwenye kambi hii kwa muda ambao Waalimu hawapo mnachukua madawati mnajipanga kwa makundi na kuelekezana wapi hujafahamu na wapi uelekezwe, furaha yenu muende mkakutane juu" Amesisitiza Tauhida

Kwa upande wao Uongozi umeeleza kuwa matarajio yao kwa wanafunzi hao ni kupata matokeo mazuri katika mitihani yao huku Wanafunzi wakimshukuru Mbunge huyo kwa kuwatembelea na kuwapelekea msaada huo na kuahidi kuwa kupitia hilo itakuwa ni chachu kwa wao kufanya Vizuri.

"Tunashukuru kwa misaada ambayo umetupa itatusaidia kwa siku ambazo zimesalia hapa kambini na tunakuahidi kwamba tutakuletea matokeo mazuri kwani jasho lako kubwa limetoka kwaajili yetu."Alishukuru Mwanafunzi kwa niaba ya wenzake

No comments:

Post a Comment