Monday, May 15, 2023

WAZAZI NA WALEZI WATAKIWA KUJENGA TABIA YA KUWALINDA WATOTO DHIDI YA VITENDO VYA UKATILI WA KIJINSIA-WAZIRI GWAJIMA


TANZANIA imeungana na Mataifa mengine Duniani kuadhimisha siku ya kimataifa ya familia huku wazazi na Walezi wakitakiwa kujenga tabia ya kuwalinda watoto wao dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia ambavyo kwa asilimia 60 vinatokea ndani ya nyumba zao.
 
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima, katika maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya familia iliyofanyika kwenye viwanja vya Nyerere squre jijini Dodoma 
 
Alisema kutokana na kukithiri kwa matukio ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto nchini wazazi wanapaswa kuwalinda watoto wao kuliko hata wanavyolinda mali zao.
 
“Wazazi lazima tubadilike ili kulinda watoto wetu kuliko tunavyolinda mali zetu leo hii wazazi wamekuwa wepesi sana kulinda nyumba, shamba unakuta mbuzi akiibiwa tuu kwa mjumbe hakukaliki lakini watoto wetu hatuwalindi matokeo yake unakuta mtoto kafanyiwa vitendo vya ulawiti sisi hatuna hata habari”alisema Dk. Gwajima
 
Kadhalika, alisema wazazi wanaowajibu huo kutokana na vitendo hivyo kwa asilimia kubwa kutokea ndani ya nyumba zao na kufanya na watu wa karibu wa familia.
 
“Kwenye aibu yetu ndipo shetani alipojificha mzazi unajifanya wewe unahuruma umekaribisha ndugu zako lakini hao ndiyo wanakuwa wa kwanza kuharibu watoto wako sisemi kuwa mkawafukuze lakini mnapaswa kulinda watoto wenu kuliko mnavyolinda mali zenu”alisema Dk. Gwajima
 
Pia, alisema moja ya sababu ya kuongezeka kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia nchini ni mmomonyoko wa maadili ni kuiga mila na desturi za mataifa mengine.
 
“Kuna watu wao hivi sasa wanataka kutengeneza kizazi ambacho hakimtegemei Mungu na kuleta tamaduni ambazo ni kunyume na agizo la Mungu kama ndoa za jinsia moja ambazo kimsingi siyo tafsiri halisi ya familia ambayo baba,mama na watoto”alisema
 
Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii Fatma Tofiq, alisema wamekutana katika siku hiyo ya kimataifa ya familia kujadilina nini kifanyike na kipi kisifanyike ili kuimarisha familia.
 
“Maadili yakiwepo katika familia zetu hakutakuwepo na watoto wa mitaani lakini pia tunapaswa kumrudia Mungu kuna mambo yanatendeka hivi sasa yanaumiza sana lakini wajibu wa kila familia kuwa na upendo na kila mtu baba au mama kuwa na wajibu wa kulinda familia yake”alisisitiza
 
Mwakilishi wa mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Mrakibu msaidizi wa Polisi Dk. Ezekieli Kyogo, alisema kama familia zitakuwa sawa mzigo wa matukio ya uharifu yatapungua nchini.
 
Naye, Prof. Palamagamba Kabudi, ambaye alikua mtoa mada katika maadhimisho hayo, alisema Watanzania wanapaswa kwa pamoja kupinga mambo ambayo ni kinyume na mila na destruri zao.
 
“Hizi ndoa za mume na mume mwingine kuwa mke hatupaswi kuzivumilia kwani kama tutazikalia kimya hivi sasa kizazi chetu cha baadaye kitaona ni jambo la kaiwa wao kufanya, na hivi sasa wanatakuwa kuwa na haki hata ya kuwa na watoto wa kuasili”alisema Prof. Kabudi
 
Mwisho

No comments:

Post a Comment