Tuesday, May 16, 2023

SERIKALI KUSHIRIKISHA WANANCHI KUHUSU KUONDOLEWA KWA KIJIJI CHA NGARESERO KWENYE PORI TENGEFU LA POLOLET, NGORONGORO


Serikali imesema kuwa itashirikisha wananchi kuhusu utekelezaji wa Maamuzi ya Baraza la Mawaziri ya kukiondoa Kijiji cha Ngaresero katika Pori Tengefu la Ziwa Natron kutokana na sababu kwamba Pori hilo ni moja kati ya maeneo yaliyotolewa maelekezo na Baraza la Mawaziri kuwa lipandishwe hadhi.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro, Mhe. Emmanuel Lekishon Shangai, lililoulizwa na Mhe. Zaytun Swai kuhusu lini Serikali itaondoa Kijiji cha Ngaresero kwenye eneo la Pori Tengefu la Pololet baada ya kujumuishwa kimakosa.

Amefafanua kuwa kulingana na Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999 na marekebisho yake ya mwaka 2019, ardhi ya Pori Tengefu Ziwa Natron ipo kwenye kundi la ardhi ya Hifadhi.

Aidha, Mhe.Masanja ameweka bayana kuwa Serikali itaenda kushughulikia mgogoro huo kwa kukutana na wananchi ili kufikia muafaka na hatimaye pori hilo liwe na hadhi iliyotarajiwa.

No comments:

Post a Comment