Thursday, May 4, 2023

KONDOA WATAKIWA KUKAMILISHA UJENZI JUNI 15 ,2023


Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bw. Ally Gugu akikagua ujenzi wa jengo la wazazi linalojengwa katika Hospitali ya Mji Kondoa ambaloliko katika hatua za umaliziaji. Ujenzi huo unaenda sambamba na majengo mengine mawili ya upasuaji na chumba cha kuhifadhi maiti. Serikali imetoa kiasi cha Shilingi milioni 900 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa Hospitali kongwe nchini.

Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bw. Ally Gugu akipata maelezo kutoka Mwalimu Anthony Dihemba wa Shule ya Sekondari Bicha kuhusu vyumba viwili vya maabara vilivyokamika na kugharimu kiasi cha shilingi Milioni 30

Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bw. Ally Gugu akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bicha iliyopo katika Halmashauri ya Kondoa Mji. Pamoja na mambo mengine Gugu amewasisitiza kusoma kwa bidii na kutunza miundombinu inayojengwa na Serikali ikiwa ni pamoja na madarasa na maabara.

Katibu Mkoa Tawala Mkoa wa Dodoma Bw. Ally Gugu amewataka Watendaji katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa kuhakikisha miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri hiyo inakamilika  ndani ya muda uliopangwa ili kuweka rekodi ya kukamilisha miradi ndani ya muda uliowekwa bila kuathiri viwango vya ubora unaokubalika.

Rai hiyo imetolewa Wilayani Kondoa katika kikao kazi baina yake na watumishi wa Halmashauri ya Mji Kondoa huku akihimiza weledi, uzalendo na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma kwa kufuata Sheria, Taratibu na Kanuni za Utumishi wa Umma.

“Suala la maadili na weledi katika taaluma zetu ni muhimu sana na nitoe rai kwenu mjitume zaidi, tumieni fursa za uwekezaji na kuendelea kuwaelimisha wengineni ili Mkoa wa Dodoma uendelee kuwa fahari ya watanzania wote” Gugu amefafanua.

Amesema watumishi wana jukumu la kusimamia agenda ya Serikali ya kuhakikisha mipango iliyowekwa inatekelezwa kwa ufanisi katika ngazi zote huku akiangazia suala la hifadhi na usimamizi wa mazingira na kuwataka kuzingatia maelekezo ya Serikali na kutekeleza kwa vitendo Kampeni ya kukijanisha Dodoma.

“Simameni katika nafasi zenu, ili kwa pamoja mtimize malengo mliyojiwekea ya kujiletea maendeleo binafsi na taifa kwa ujumla. Natoa rai kila mmoja kusimama katika  nafasi yake katika kutimiza malengo na majukumu ya msingi. Wekeni utaratibu wa kutatua changamoto zenu kwa njia ya mazungumzo, ikiwa ni pamoja na kukwamua utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wakati, hatutakubali miradi kutokamilika na kuvuka mwaka ifikapo tarehe 30 Juni 2023. 

Halmashauri ya Mji Kondoa ni moja kati ya Halmashauri 8 zilizopo katika Mkoa wa Dodoma na ilianzishwa mwaka 2015 ikiwa ni ukubwa wa kilometa za mraba 703 na ipo katika Kata ya Chemchem, Mtaa wa Kwapakacha.

No comments:

Post a Comment