Tuesday, March 7, 2023

"Wataalamu wa TPHPA shirikini kikamilifu kutekeleza Mashirikiano na AVRDC"Kaimu Mkurugenzi wa TPHPA Prof Joseph Ndunguru

 


Pichani: Kulia Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) Prof. Joseph Ndunguru akisalimiana na Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika ya World Vegetable Centre Ndg. Gabriel Rugalema











Na Innocent Natai

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) Prof. Joseph Ndunguru amewataka wataalamu wa mamlaka hiyo kushiriki kikamilifu katika utekelezaji ya makubaliano ya mashirikiano na kituo cha  Africa World Vegetable Center  (AVRDC) ili kuhakikisha nasaba za mimea zinakusanywa na kuhifadhiwa kwa wingi.

Prof. Ndunguru ameyasema hayo leo March 7,2023 baada ya kufanya ziara ya kutembelea ofisi za kituo hicho kinachojihusisha na utafiti,ukusanyaji na uboreshaji wa nasaba za mbegu za mboga mboga  kilichopo Wilaya ya Arumeru Mkoani Arusha.

Aidha alisema kuwa katika mazungumzo waliyofanya wameweka makubaliano ya kushirikiana katika maeneo matatu na miongoni mwa makubaliano hayo ikiwa ni pamoja na kukusanya zaidi nasaba katika Genebank na kuchambua kwa pamoja nasaba za mbegu ambazo zimekwisha kukusanywa kwakutumia teknolojia za kisasa,

Pia kushirikiana katika Mafunzo kwa wataalamu ya kujengeana uwezo katika miundombinu ya uhifadhi wa nasaba na Afya ya mimea ambapo wamekusudia kuandaa kwa pamoja mafunzo kwa wataalamu ya kutambua visumbufu vya mimea kwa maana ya magonjwa, wadudu na pia teknolojia za kisasa za kugundua na kudhibiti visumbufu 

Na eneo la tatu ( 3) ikiwa ni kuwa na miradi ya pamoja ambapo Prof Ndunguru amebainisha kuwa miradi hiyo itawezesha kutafuta fedha kwaajili ya kutekeleza malengo ya taasisi zote mbili

Pia amebainisha kupitia mashirikiano hayo taasisi hizo mbili zitaweza kufanya mambo makubwa ikiwemo kuwashawishi wadau wa maendeleo wakawapatia fedha kwaajili ya kuendelea kutekeleza majukumu yao 

Kupitia hayo ametoa wito kwa timu ya wataalamu watakaochaguliwa na Mamlaka na kituo hicho kwaajili ya kushughulikia makubaliano hayo kufanya kazi kwa bidii wakijua kuwa hayo yanafanyika kwa manufaa ya Watanzania wote.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa  kituo hicho kanda ya Afrika ya World Vegetable Centre Ndg. Gabriel Rugalema amesema kuwa amefarijika kutokana uwepo wa makubaliano hayo mapya ya Mashirikiano kwani kama taasisi ya utafiti wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali ambazo kupitia mashirikiano hayo wanaimani zitatatuliwa kikamilifu

“Kama Mheshimiwa rais wetu anavyosema tukienda pamoja tutafika mbali, tukienda mmoja mmoja hatutofika kwa wakati na ushirikiano wetu utatusaidia kuweka rasilimali zetu kama watu,fedha na vifaa Pamoja na kuzitumia vyema” alisema Ndg. Rugalema

Aidha amemalizia kwa kusema kuwa kwasasa Dunia ipo katika mapambano ya janga la mabadiliko ya tabia ya nchi na TPHPA wanalojukumu la Kitaifa la kutunza nasaba ya mazao tofauti tofauti kwaajili ya kuyakinga na mabadiliko ya tabia ya nchi na AVRDC inayo jukumu la kidunia katika kutunza,kuchakata na kuboresha nasaba ya mazao ya mboga mboga kwa matumizi ya dunia nzima, kwahiyo kwa mashirikiano hayo wataweza kuweka nguvu za pamoja.

Katika ziara hiyo iliyolenga kufanya mazungumzo ya kuweka mashirikiano kati ya Taasisi hizo mbili Prof. Ndunguru aliambatana na wataalamu kutoka Mamlaka hiyo.

No comments:

Post a Comment