Na SAIDA ISSA,DODOMA.
SERIKALI kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), limezindua Programu ya Mpango wa miaka minne wa jinsia wenye lengo la kutatua changamoto za wanawake katika maeneo yao ikiwemo vitendo vya unyanyasaji.
Akizugumza wakati wa uzinduzi wa program hiyo Naibu Waziri wa Nishati Stephen Byabato alisema mradi huo unalenga kutengeneza sera za shirika na kujenga uwezo kuhusu masuala ya unyanyasaji wa kijinsia.
Alisema mradi huo, utasaidia kuwepo kwa taarifa sahihi za unyanyasaji wa kijinsia katika shirika, kuruhusu fursa ya ukuzaji taaluma kwa wafanyakazi wanawake na kuongeza mafunzo kwa vitendo kwa wafanyakazi wanawake waliopo kazini.
“Mradi huu unatekelezwa na TANESCO lengo ni kuhakikisha watumishi wanaofanya kazi katika taasisi hiyo wanapata haki sawa,lengo ni kuhakikisha nafasi mbalimbali zinazojitokeza zinahusisha jinsia zote bila ubaguzi na kujenga usawa.
"Katika mradi huo tumekubaliana kuunda kitengo maalumu ambacho kitakuwa na bajeti na kujengewa uwezo kuhusu masuala ya jinsia ili mtu anapopata changamoto awe na sehemu ya kwenda kusema na kupata msaada.
Byabato alisema kuwepo kwa kitengo hicho ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020 hadi 2025 ambayo imeeleza serikali mambo mbalimbali ikiwemo uanzishwaji wa dawati ya jinsia.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO Mwanaidi Maajar alisema maendeleo hayawezi kuwepo kama hakutakuwa na usawa wa kijinsia.
Alisema wanawake wamekuwa hawapewi kipaumbele katika nafasi kubwa za uongozi na ukizingatia sensa ya watu na makazi ya mwaka jana inaonyesha idadi ya wanawake ni wengi kuliko wanaume.
“Tunataka wanawake wa TANESCO wawe na haki na wajibusawa na wanaume kusiwepo na vitendo vya vitisho akashindwa kufanya maamuzi mbalimbali,pia katika meza ya maamuzi na wanawake nao washirikishwe ili kujenga usawa mahali pa kazi.
Awali akitoa salamu za taasisi yake Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Maharage Chande alisema mradi huo ni ajenda ambayo ipo katika taasisi hiyo.
Alisema TANESCO wamebahatika kupatia mradi wa TAZA ambao ni wa kusafirisha umeme mkubwa kutoka Tanzania kwenda Zambia na unafadhiliwa na serikali na wadau wengine.
“Katika mradi huu kuna kiapo cha kuangalia masuala ya usawa wa kijinsia, na lengo la kuzindua mradi huu ni kuongeza chachu ya uwepo wa usawa katika masuala yote katika taasisi yetu,”alisema
No comments:
Post a Comment