KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeridhishwa na teknolojia ya tabaka gumu la mawe iliyotumika katika ujenzi wa Barabara ya Seneto hadi Kreta katika Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro.
Mwenyekiti wa
Kamati ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Timotheo Mnzava (Mb)
ametoa kauli hiyo leo wakati wa ziara ya kukagua mradi wa ujenzi wa barabara katika
Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, mkoani Arusha
“Kwa kweli tumefurahishwa sana na aina
hii ya teknolojia iliyotumika katika ujenzi wa barabara na sisi kama Kamati
tutaendelea kuishauri Serikali kuitumia katika maeneo mengine yanayohitaji
teknolojia ya aina hii” Mnzava
amesisitiza.
Amefafanua kuwa
awali barabara hiyo ilikua changamoto kwa watalii wanaoingia katika eneo la
Kreta lakini kwa kazi iliyofanyika itaendelea kuwavutia wageni na kuhakikisha
usalama wa wageni wanaotembelea Kreta ya Ngorongoro.
Mnzava
ameipongeza Serikali kwa kutoa fedha zilizotumika katika ujenzi wa barabara
hiyo na pia ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka ya Hifadhi ya
Eneo la Ngorongoro kwa kuisimamia kazi ya ujenzi.
Ametoa wito kwa
Serikali kuongeza juhudi na kasi katika kumalizia kipande cha barabara
kilichobakia lakini pia kuangalia uwezekano wa kukarabati barabara nyingine za
Ngorongoro ili kukuza utalii na kuongeza usalama wa watalii wanaotembelea eneo
hilo.
Naye, Naibu Waziri
wa Maliasili nanUtalii, Mary Masanja (Mb) amesema barabara hiyo ni hazina
katika hifadhi kwa sababu imejengwa kwa kuokoa gharama ambapo awali zilipangwa
kutumika kiasi cha shilingi bilioni 1.9 lakini imetumia kiasi cha shilingi
bilioni 1.7.
Amesema mfumo wa
barabara za mawe ni bora zaidi kwa sababu ni rafiki wa uhifadhi na gharama
nafuu ukilinganisha na barabara za lami.
Ameongeza kuwa
maelekezo yote ya Kamati ya kumalizia eneo la barabara lenye urefu wa kilomita
1.2 na kuangalia uwezekano wa kutumia teknolojia ya mawe katika maeneo mengine
uhifadhi yatafanyiwa kazi.
Ametumia fursa
hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa kuwa kinara katika uhifadhi na uendelezaji wa utalii ambapo moja ya
mikakati yake ni kuhakikisha miundombinu katika maeneo yote yaliyohifadhiwa iwe
rafiki kwa watalii ili iwezeshe kuongeza idadi ya watalii.
No comments:
Post a Comment