OR-TAMISEMI
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe.Denis Londo amezitaka Halmashauri zote nchini kuimarisha usimamizi katika ukusanyaji na matumizi ya fedha zitokanazo na mapato ya ndani ili fedha hizo zitumike kutekeleza miradi ya maendeleo na sio kusubiri fedha kutoka Serikali Kuu.
" Utakuta Halmashauri mapato yake ya ndani ni Bil. 2 au 3 na katika hali yoyote ile haiwezi kufikiria kujenga vituo vya afya au shule jukumu hili limebeba Serikali Kuu" Amesema Mhe. Londo
Mhe. Londo ametoa agizo hilo 16 Machi 2023 wakati akihitimisha ziara ya Kamati ya kudumu ya Bunge Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mkoa wa Simiyu.
Amebainisha kuwa kuna baadhi ya Halmashauri hazioni kwamba zina jukumu la kutekeleza miradi ya maendeleo katika Halmashauri zao hali inayopelekea kutosimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa umakini.
Aidha amewataka watoa huduma katika vituo vya kutolea huduma za AfyaMsingi nchini kuhakikisha wanatoa huduma bora zinazoendana na uwekezaji ambao unafanywa na Serikali wenye lengo la kuimarisha utoaji wa huduma bora za afya nchini.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Deogratius Ndejembi ( MB) amemuelekeza Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii, Ofisi ya Rais TAMISEMI kuhakikisha ifikapo tarehe 20 Machi 2023 wataalamu wa kutoa mafunzo ya vifaa tiba wawe wamefika katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya Bariadi ili kutoa mafunzo kwa watoa huduma wa hospitali hiyo.
Aidha amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi kutenga fedha kwaajili ya kujenga njia za watembea kwa miguu ( walkways) katika Hospitali ya Halmashauri Bariadi pamoja na kuhakikisha anafanya mawasiliano na Bohari Kuu ya Dawa ( MSD) kuhakikisha generata linafika katika Hospitali ya Halmashauri ya Bariadi na kuanza kufanya kazi.
No comments:
Post a Comment