Na Saida Issa, DODOMA
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi Benedict Ndomba amesema kuwa Mfumo rasmi wa ukusanyaji fedha za umma (GePG), umesaidia kuongeza mapato ya serikali na kudhibiti mianya yote iliyokuwepo awali wakati wa matumizi ya vitabu.
Mkurugenzi huyo aliyasema hayo jana jijini Dodoma alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji wa shunghuli mbalimbali za mamlaka hiyo kwa waandishi wa habari.
Mkurugenzi Ndomba alisema mfumo huo umekuwa msaada mkubwa kwa serikali katika kuongeza kiwango cha ukusanyaji wa mapato na kuondoa mianya yote ya watu kukwepa kufanya malipo ya serikali.
“Mfumo huu umeisadia serikali kuongeza mapato lakini pia kuona kiasi cha fedha ambacho kinakusanywa kila siku kupitia mfumo huu hata muda huu ukitaka kuangalia ni kiasi gani kimeingia unaona moja kwa moja tofauti na ilivyokuwa hapo awali wakati tunatumia vitabu vya stakabadhi,”alisema Mhandisi Ndomba.
Kadhalika alisema kuwa mfumo huo pia unaisadia serikali kutambua ni taasisi gani ambazo zimekuwa zikiongoza kwa ukusanyaji mapato nchini.
“Lakini pia mfumo huu unaisaidia serikali kupata takwimu za kila halmashauri,taasisi na kutambua kuwa ni eneo gani ambalo limekuwa linachangia kwa kiasi kikubwa kwenye pato la taifa,"alieleza.
Pia alisema kuwa Mamlaka hiyo imeendelea kusanifu, kujenga na kusimamia uendeshaji wa mifumo tumizi inayotumiwa katika taasisi za umma kwa pamoja.
“Baadhi ya mifumo hiyo ni pamoja mfumo wa baruapepe serikalini (GMS) ambao unaziwezesha taasisi za umma kuwasiliana na kubadilishana taarifa kwa usalama, haraka na kwa gharama nafuu ambapo jumla ya taasisi 616 zinatumia mfumo huu”alisema
Alisema mfumo mwingine ni wa Ofisi Mtandao (e-Office) ambapo jumla ya taasisi 200 zinautumia hadi sasa.
Mkurugenzi huyo alisema mfumo wa Ofisi Mtandao mbali na kurahisisha utendaji kazi katika taasisi za umma pia umesaidia kupunguza matumizi ya karatasi na kutunza mazingira na kuokoa fedha za serikali.
“Mfumo wa Utoaji Huduma za Serikali kwa Simu za Mkononi (MGov) Mfumo wa mGOV umeunganishwa na watoa huduma wote wa simu za mikononi nchini Tanzania,hadi sasa, taasisi zaidi ya 275 zimeunganishwa na kuutumia mfumo wa mGOV kutoa huduma”alisema
Hata hivyo, alisema baadhi ya huduma hizo ni jumbe fupi yaani SMS za ununuzi wa umeme (LUKU), SMS za huduma za malipo ya serikali.
Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) ni Taasisi ya Umma iliyoanzishwa kwa Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya mwaka 2019, ikiwa na majukumu ya kuratibu, kusimamia na kukuza jitihada za Serikali Mtandao, pamoja na kusimamia uzingatiaji wa Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao katika Taasisi za Umma na utoaji wa huduma kwa wananchi yenye Lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika Taasisi za Umma pamoja na kuboresha utoaji wa huduma kwa Umma ili huduma hizo zipatikane kwa urahisi, haraka na kwa gharama nafuu kupitia TEHAMA.
Mwisho
No comments:
Post a Comment