Na Mathias Canal, WEST-Dodoma
Serikali
imetangaza timu ya watu watano kwa ajili ya kufanya Utafiti wa ufuatiliaji wa
wahitimu wa mafunzo ya ufundi kutoka vyuo vya VETA nchini.
Timu
hiyo itaongozwa na Dkt. Hamisi H. Mwinyimvua ambaye ni Mhadhiri kutoka Chuo
Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) na wajumbe wanne ambao ni Prof. Deograsias P.
Mushi Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM), Dkt. John Chegere
Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM), Dkt. Claude Maeda Mhadhiri
kukota Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Dkt. Ibrahim Kadigi Mhadhiri
kukota Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).
Akitangaza
timu hiyo ya Wataalamu hao leo tarehe 16 Agosti 2022 Waziri wa Elimu, Sayansi
na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa tafiti hizo zitalenga Kutathmini
athari chanya au hasi za muda mrefu za programu mbalimbali za elimu; Kuboresha
mitaala na mazingira ya elimu na mafunzo; Kujua vikwazo wanavyopambana navyo wahitimu
wanapoenda kwenye soko la ajira ili kuboresha; na Kujua kama elimu au ujuzi
unaohitajika kwenye soko la ajira au mahali pa kazi unaendana na elimu au
mafunzo yanayotolewa na vyuo husika.
Amesema
kuwa malengo hayo yanaonyesha kuwa tafiti za ufuatiliaji zinatoa taarifa muhimu
kwa wadau wanaohusika na Utoaji wa Elimu na Mafunzo – Kuandaa Sera ya Elimu na
Mafunzo; Kuandaa Mitaala ya Elimu na Mafunzo; n.k. ili kuhakikisha wale wote
wanaohitaji elimu na mafunzo au ujuzi wa aina fulani wanapata fursa hiyo.
Pia
malengo hayo yanaonyesha Ajira na Uandaaji wa Sera za Ajira – Kuandaa Sera na
Miongozo ya Ajira ili kuhakikisha wataalamu wa aina mbalimbali wanaohitajika
wanakuwepo ili kutoathiri uwekezaji na ukuaji wa uchumi; pamoja na Ufanyaji
Maamuzi ya kifamilia au binafsi - Kuhusu aina gani ya elimu au mafunzo ya
ujuzi mtoto au mtu asomee ili kukubalika kwenye soko la ajira au kuanzisha
biashara binafsi.
Waziri
Mkenda amesema kuwa kwa sababu ya msukumo mkubwa uliowekwa kwenye ujuzi wadau
wote wa elimu nchini wanapewa fursa ili waweze kutoa ushirikiano kwa kutoa
maoni yao ili kuboresha elimu ujuzi.
Amesema
kuwa Utafiti wa Ufuatiliaji au tracer study ni utafiti unaofanywa kufuatilia
masuala mbalimbali ya wahitimu wa mafunzo mbalimbali kwa kutumia dodoso maalumu
la mahojiano (questionnaire) kutegemeana na malengo ya utafiti huo.
Waziri
Mkenda amesema kwa kuelewa kuwa wahitimu wa mafunzo ya VETA wameongezeka kutoka
179,930 mwaka 2016 hadi 295,446 mwaka 2020, na utafiti wa mwisho wa aina hii
ulifanyika mwaka 2018 kwa waajiriwa wa 2010 – 2015, malengo ya Utafiti wa
Ufuatiliaji unaofanywa na Timu hiyo itakuwa ni Kujua walipo na wanafanya
shughuli gani wahitimu wa mafunzo ya VETA baada ya kuhitimu masomo yao
(waliohitimu 2017 – 2021).
Malengo
mengine ni Kulinganisha mahitaji ya soko la ajira na uzalishaji wa wahitimu wa
VETA (demand vs supply of graduates in the labour market), Kujua kama ujuzi
unaohitajika kwenye soko la ajira unaendana na ujuzi unaofundishwa na vyuo
husika, na Kujua kama kuna waajiri wasioajiri wahitimu wa VETA na sababu zake.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt Fransis
Michael amesema kuwa timu hiyo ina kazi kubwa kuhakikisha kuwa inapokea maoni
kutoka maeneo mbalimbali ili kuakisi uwajibikaji na ufanisi wa elimu ujuzi.
Amesema
kuwa lengo kubwa katika ukusanyaji huo wa maoni ni kuhakikisha kuwa wanafunzi
wanapomaliza elimu ujuzi waweze kuajirika kirahisi katika maeneo mbalimbali
waliyosomea.
Naye
Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) ambaye ni kiongozi wa timu
hiyo Dkt. Hamisi H. Mwinyimvua amesema kuwa utafiti wa aina ya ufuatiliaji
unaweza kufanyika kujua walipo wahitimu wa kada au ujuzi fulani
(graduates) au wahitimu kutoka chuo fulani (alumni).
Dkt
Mwinyimvua ameongeza kuwa lengo la ufuatiliaji linaweza kuwa kujua
ajira/shughuli wanayofanya baada ya kuhitimu, jinsi wanavyotumia ujuzi
walioupata na changamoto wanazopambana nazo.
MWISHO
No comments:
Post a Comment