Wakristo nchini wametakiwa kuendelea kuhubiri kweli ya
Mungu ambayo ni Neno la Mungu , huku wakiyazingatia maelekezo yote yanayopatikana
katika Maandiko Matakatifu yanayotolewa na watumishi wake na kuyashika kikamilifu.
Agizo hilo limetolewa na Askofu Mstaafu wa Kanisa la
Anglikana Tanzania Dayosisi ya Mpwapwa Dinare ya Kongwa Dkt. Jacob Erasto
Chimeledya wakati akitoa ujumbe wa Neno la Mungu katika ibada ya kipaimara
iliyofanyika Agosti 14, 2022 kanisani
hapo.
Katika ibada hiyo iliyoambatana na uzinduzi wa Jengo
la kuabudia, Askofu Chimeledya alisema kanisa la sasa linatakiwa kuzingatia
maelekezo yote yaliyofundishwa na mitume kupitia maandiko matakatifu ili waweze
kutoyafuata mafundisho ya uongo, kama ambavyo waumini wa kanisa la kwanza
walivyokengeuka na kufuata mafundisho ya uongo.
“ Kuna tatizo lilitokea katika kanisa la kwanza pale
Efeso waumini wake walifuata walimu wa uongo na kwa makundi makundi wakaanza kuiamini ile imani na Timotheo
alikuwa peke yake, na kundi kubwa la watu walijitenga na kweli ya Mungu
wakiamini mafundisho ya uongo na kuzifuata roho zidanganyazo.” Alisema Askofu
Alisema kanisa linaweza kufa endapo tu waumini hawatozingatia
maagizo ya Mungu kama ambavyo Paulo alimwambia Timotheo akitolea mfano wa
Mataifa ya Uingereza, Marekani, Australia ambapo baadhi ya Majengo hayatumiki tena kama
sehemu za kuabudia yamegeuka kuwa
Migahawa baada ya waumini kusikiliza
mafundisho ya Duniani, wakayazingatia, wakayaamini na kuyafuata hayo na kuacha kweli ya Mungu.
“ Ndugu zangu tunaambiwa na sisi kuwa utafika wakati
watu wataikataa hiyo kweli ya Mungu, Watakupinga, watakwambia wewe muongo nenda zako,
unatudanganya kila siku, kwanza unatuchelewesha, Mtume Paulo anamwandikia Timotheo anasema itafika
wakati watu watayakataa mafundisho yenye uzima ila watazifuata nia zao wenyewe
watajipatia walimu makundi makundi kwa kuwa wana masikio ya utafiti
watajiepusha wasisikie yaliyo kweli watageukia hadithi za uongo.” Aliongeza Askofu
Aliwataka Wakristo kuzingatia mambo matatu muhimu
katika utumishi wao akiwahimiza kuwa watoaji iwe ni kwa mali, maisha au miili yao lakini pia wasiache kumwamini
Yesu Krito , kuwa na matumaini nae na kusimama katika kweli kwenye maisha yao yote wawapo hapa Duniani.
Katika Risala yao kwa Askofu Chimeledya waumini wa
kanisa hilo walimpongeza kwa kazi nzuri aliyoianzisha katika kipindi chake cha
Uaskofu zikiwemo kuhimiza Semina na Mikutano ya Kiroho, kuwatunza viongozi
wastaafu, Kuanzisha Ibada za Jumuia, Ujenzi wa Makanisa na nyumba za watumishi.
Ibada hiyo ilienda sambamba na kuwekewa mikono wana Kipaimara wa Dinare ya Kongwa wapatao 143, ambapo viongozi mbalimbali wa Serikali na Chama cha Mapinduzi walihudhuria akiwemo Spika Mstaafu na Mbunge wa Kongwa Mhe. Job Ndugai, Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. White Zuberi Mwanzalila na Katibu wa CCM Wilaya hiyo Joyce Mkaugala.
No comments:
Post a Comment