Saturday, May 28, 2022

MIUNDOMBINU BORA YA MICHEZO YAVUTIA MASHINDANO YA KIMATAIFA NCHINI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) Mei 28, 2022 jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa za michezo mbalimbali inayoendelea ndani na nje ya nchi.

Waandishi wa habari wakitekeleza majukumu yao wakati Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi (hayupo pichani) akitoa taarifa za michezo mbalimbali inayoendelea ndani na nje ya nchi Mei 28, 2022 jijini Dar es Salaam.

Na Eleuteri Mangi-WUSM, Dar es Salaam

Tanzania inaendelea kupata heshima ya kuwa mwenyeji wa mshindano mbalimbali ya Kanda, Afrika na Dunia kwa ujumla katika michezo mbalimbali kutokana na mazingira mazuri yanayowekwa na Serikali katika sekta hiyo.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi katika mkutano na waandishi wa habari Mei 28, 2022 jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa za michezo mbalimbali inayoendelea ndani na nje ya nchi.

“Maboresho yanayofanywa na Serikali kwenye miundombinu bora na rafiki katika michezo, utulivu na amani iliyopo nchini vinaleta hamasa kwa mataifa mengine kuleta mashindano hapa nchini” amesema Dkt. Abbasi.

Dkt. Abbasi ameongeza kuwa, uwanja wa ndani wa Benjamin Mkapa unaendelea kuwa kivutio  baada ya kufanyiwa maboresho kwa fedha zilizotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan,  ambapo ulianza kutumika Desemba 2021, na nchi nyingi zinapenda kuutumia.

Baadhi ya mashindano ya kimataifa ambayo yamefanyika katika uwanja huo ni pamoja na mchezo wa wa riadha Afrika Mashariki ambapo nchi saba zimeshiriki Tanzania ikiwa ni mwenyeji wa mashindano hayo, pamoja na Kenya, Ethiopia, Eritrea, Sudani Kusini na Somalia.

Mashindano mengine ambayo yamefanyika kwenye uwanja huo ni pamoja na mchezo wa Ngumi za Ridhaa, nchi za Tanzania, Zambia, Burundi, Zimbabwe na Uganda zinashiriki ambapo mchezo mwingine uliochezwa hapo ni mchezo wa Baseball ambao ulishirikisha nchi za Tanzania, Zambia, Zimbabwe, Tunisia, Ghana, Bukina Faso na Misri.

Aidha, Katibu Mkuu Dkt. Abbasi amesema kuwa Serikali inaendelea kuzisimamia timu za Taifa ikiwemo ambazo zinashiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola ambayo itafanyika Birmingham nchini Uingereza.

“Timu za kuogelea, riadha, judo, na mchezo wa kunyanyua vitu vizito zipo kambini tangu mwezi wa Februari, 2022, tumeachana na tabia ya kuweka timu kambini kwa muda mfupi, Serikali inagharimia maandalizi hayo kwa asilimia 100” amesema Dkt. Abbasi. 

Ameongeza kuwa Wizara hiyo,  inaendelea kusimamia kimkakati suala la michezo nchini ikiwemo maandalizi ya Timu ya Tembo Worriors ambayo inashiriki fainali za kombe la Dunia kwa watu wenye ulemavu zitakazofanyika Oktoba mwaka huu nchini Uturuki.

Timu ya Taifa ya Serengeti Girls pia inasimamiwa na Serikali ili wafuzu kushiriki fainali za dunia kwa wasichana wenye umri wa miaka 17  na kuliwakilisha vyema taifa nchini katika fainali za dunia katika mchezo huo itakayofanyika nchini India.

Timu hiyo imewafunga timu ya taifa ya Cameroon kwa jumla ya magoli 4-0 mchezo uliochezwa nchini Cameroon na mchezo wa marudiano utachezwa Juni 5, 2022 katika uwanja wa Amani Zanzibar.

No comments:

Post a Comment