Wednesday, May 11, 2022

MHE MAVUNDE AMPA MKANDARASI SIKU 14

Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe Anthony Mavunde amempa siku 14 mkandarasi anayetakiwa kujenga mradi wa umwagiliaji wa Kilida uliopo katika Kijiji cha Kilida, kilichopo Jimbo la Kavuu, Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe mkoani Katavi.

Mhe Mavunde ametoa maelekezo hayo alipotembelea mradi huo kujionea uharibifu uliotokana na mvua kubwa zilizonyesha na kuharibu baadhi ya mashamba ya wakulima katika kijiji hicho.

“Nimewaelekeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kuhakikisha mkandarasi anayetakiwa kujenga mradi huu awe amefika hapa ndani ya siku 14.

Awali mkandarasi alikuwa anasema anashindwa kuja sababu ya mvua ila nimefika mwenyewe mpaka hapa na nimejionea barabara zinapitika na hamna kisingizo nampa siku 14 aje aanze kazi tuwasaidie wananchi wetu,” amesema Mhe Mavunde.

Awali Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe Geophrey Pinda amesema kuwa mradi huo wa umwagiliaji utakapojengwa na kukamilika licha tuu ya kutoa ajira utasaidia pia kuzalisha mbegu.

“Tunataka hapa pawe na mradi mkubwa wa umwagiliaji utakaosaidia uzalishaji mkubwa wa mbegu. Wananchi wa huku wanaumizwa sana na bei ya mbegu ila zikizalishwa hapa maisha ya wananchi wengi hapa yatabadilika,” amesema Mhe. Mbunge huyo.

No comments:

Post a Comment