Na WyEST, DODOMA
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda (Mb) amesema Wizara itatenga bajeti kwa ajili ya mtu yeyote mwenye muswada wa kuandika riwaya ambazo zitashindanishwa na muswada ambao utashinda utagharamiwa uchapishaji wake na Wizara.
Amesema hayo Jijini Dodoma alipokutana na wawakilishi wa Mwandishi wa Kitabu cha Hesabu kilichoandikwa kwa kutumia mitaala ya Kenya, Uganda na Tanzania, David Inzofu ambapo amesema lengo ni kuona kunakuwa na Watanzania wengi wanaojitokeza kuandika vitabu.
Waziri Mkenda amemuagiza Kamishna wa Elimu kuhakikisha kitabu hicho kinapitiwa na wataalamu kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) ili kama kuna sehemu ya kuboresha iweze kuboreshwa kwa lengo la kumsaidia mwandishi huyo ili kuongeza hamasa kwa Watanzania wengi zaidi kuandika vitabu na kuhamasisha usomaji.
“Tunataka kusaidia waandishi ambao wanataka kuandika riwaya. Tunaposema elimu yetu tunataka iakisi mahitaji ya nchi yetu na utamaduni wetu tungependa pamoja na wanafunzi kusoma vitabu vya nje wasome pia vilivyoandikwa na Watanzania,” amesema Prof. Mkenda.
Amesema kumekuwepo na maoni ya kutumia Kiswahili kufundishia katika siku zijazo, hivyo kunahitaji maandalizi ili kuweza kufika huko, Watanzania wenyewe waandike vitabu wawe tayari, uwezo na uzoefu wa kutafsiri vitabu vya Kiingereza kuwa vya Kiswahili.
“Tungependa kukuza Kiswahili na hii inahitaji maandalizi, hivyo lazima kuwe na vitabu vingi vya Kiswahili, huwezi kuanza kutumia lugha ya Kiswahili huku vitabu vikiwa vya Kiingereza. Huyu mwalimu David Inzofu nafurahi kwamba ametafsiri hiki kitabu kwa Kiswahili itabidi tumsaidie ili Baraza la Kiswahili lihakiki kitabu hicho,” ameongeza Waziri Mkenda.
Kwa upande wao, mmoja wa wawakilishi wa mwandishi wa kitabu hicho, Novatus Makunga amemshukuru Waziri Mkenda kwa kukubali kupokea nakala hizo kwa ajili ya kuvipitia, akisema hiyo inaonyesha nia njema ya Serikali iliyo nayo kushirikiana na wadau wengine wa elimu katika kuendelea kuboreaha elimu nchini.
No comments:
Post a Comment