Wednesday, March 2, 2022

RC MAHENGE ATEMBELEA MASOKO YA MANISPAA YA SINGIDA ATOA MAAGIZO “NITASIMAMIA MWENYEWE”

 



Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Binilith Mahenge (wa kwanza kulia ) akiongea na wafanyabiashara hivi karibuni  katika soko la kilambida Kata ya Kindai  manispaa ya Singida ikiwa ni ziara yake ya kuangalia hali ya mazingira ya usafi na miundombinu mbalimbali ya masoko.




Wafanyabiashara wa soko la Kilambida wakisikiliza viongozi wakati wakihutubia namna ya utekelezaji mbalimbali wa shughuli za maendeleo katika Manispaa 

Kaimu Mkurugenzi manispaa ya singida Dk. Adrianus Kalekizi( wa kwanza kulia ) akitoa ufafanuzi katika baadhi ya hoja zilizotolewa na Mkuu wa Mkoa katika ziara yake ya hivi karibuni katika masoko ya manispaa hiyo.)

Na Bashiri Salum -Singida

 

MKUU wa Mkoa wa Singida Dk. Binilith Mahenge leo Machi 2,  2022 ametembelea masoko ya Kilambida, Mitunduruni na Mahembe yaliyopo katika Manispaa  hiyo lengo likiwa ni kukagua mazingira ya usafi pamoja na maeneo waliyokwisha pangiwa kufanyia biashara ya mazao ya chakula.

Akiwa katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa huyo alimuagiza Mkurungezi wa Manispaa ya Singida kutafuta fedha kwa ajili ya kulipa  fidia kwa wamiliki wa makaburi yaliyopo soko la mahembe ili kupisha wafanyabiashara pamoja na  kufanya marekebisho ya miundombinu  katika baadhi ya maeneo hayo.

Dk. Mahenge alisisitiza juu ya  ujenzi wa maegesho ya magari na sehemu za kushushia mizigo pamoja na kulifanya soko la Mahembe kama sehemu ya kushushia ndizi na viazi kutokana na maeneo mengine kuwa yameshajaa

Hata hivyo Dk. Mahenge aliitaka Manispaa kuhakikisha wananchi wanapata taarifa ya kila kinachoendelea  kuhusu fidia za makaburi na baadhi ya wamiliki wa nyumba ambazo zinatakiwa kupisha eneo la soko na kuwataka kuweka utaratibu ambao hautachelewesha utekelezaji wa shughuli hizo.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Singida Mhandisi Paskasi Muragili akawataka wafanyabiashara hao kuhakikisha kwamba wanabaki katika maeneo yao waliyopangiwa wakati serikali ikiendelea kupambana na changamoto zinazojitokeza.

Mhandisi  Muragili aliwataka viongozi wa masoko kuelimishana ili kutoa ushirikiano wakati wa ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya masoko ikiwa ni pamoja na kukubali kufanya maendeleo wakati taratibu za malipo ya fidia yakiendelea.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Dk. Adrianus Kalekizi amemueleza Mkuu wa Mkoa kwamba Manispaa imejipanga kuhakikisha zoezi  litakamilika ifikapo mwezi Mei 2022 ambapo  kwa sasa tayari bajeti yake imeshapangwa.

Ziara hiyo ya Mkuu wa Mkoa iliwahusisha Viongozi wote wa Manispaa kamati ya ulinzi na usalama pamoja na wataalamu mbalimbali wa mazingira.

 

No comments:

Post a Comment