Na. John Mapepele
Naibu Waziri wa Kilimo na Mbunge wa Dodoma Mjini Mhe. Antony Peter Mavunde ameipongeza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mkakati kabambe wa kuratibu tamasha kubwa la kihistoria la Muziki la Serengeti litakalowakutanisha zaidi ya wasanii mia moja wa miuziki litakalofanyika Dodoma Machi 12-13 Mjini Dodoma
Aidha Mhe. Mavunde amepongeza kwa ubunifu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo wa kuongeza siku ambapo sasa litafanyika kwa siku mbili badala ya moja kama ilivyopangwa awali kutokana na mahitaji makubwa ya tamasha hilo kwa wasanii na wananchi.
“Hii ni kazi nzuri na kubwa inayofanywa na Wizara hii, wasanii zaidi ya mia moja wamekutanishwa katika jukwaa moja kutoa burudani na kutangaza vivutio vya utalii vilivyomo katika nchi yetu kupitia mbuga yetu ya Serengeni, nitoe wito kwa wananchi wote wa Dodoma kutumia fursa hii adimu kushiriki kwenye tamasha hili la kihistoria”. Amefafanua Mhe Mavunde
Akizungumza leo Machi 3, 2022 jijini Dodoma amewataka pia Wasanii wa Dodoma kujitokeza kwa wingi ili kujifunza na kupata uzoefu kutoka kwa wanamuziki na wasanii wakongwe watakaotumbuiza kwenye tamasha hilo.
Aidha, Dkt. Abbasi amesema kuwa Tamasha hili ndiyo tamasha pekee kubwa linalowaleta pamoja wasanii mbalimbali, wachanga na wakongwe, pia bendi za muziki kujumuika pamoja bila kujali lebo zao.
Ameeleza kuwa nia ya Serikali ni kuhakikisha wasanii wanabadilishana uzoefu kwenye fani ya muziki ili kukuza vipaji vyao huku wakitumia tamasha hilo kutangaza utalii na vivutio mbalimbali vya Tanzania sasa inakwenda kufikiwa kwa ukamilifu.
Mwenyekiti wa Kamati ya kuratibu tamasha hili, Dkt. Emmanuel Ishengoma ambaye pia Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa nchini amesema maandalizi yote muhimu yamekamilika kitu kilichobaki kwa sasa ni wananchi kutoka sehemu mbalimbali nchini kuja kushiriki tamasha hilo ambalo limesheheni burudaki kali kutoka kwa wasanii wenye vipaji.
Kwa upande wake Msanii Mkongwe wa Muziki nchini Mlisho Mpoto amesema tamasha hilo linakwenda kukata kiu ya watanzania ya kupata burudani ya wasanii wa nyumbani.
No comments:
Post a Comment