Friday, March 25, 2022

MKOA WA MWANZA WAELEZEA MAFANIKIO KATIKA KUPAMBANA NA UGONJWA WA KIFUA KIFUU

Dkt Nangi William Mratibu wa kifua kikuu na ukoma Mkoani Mwanza


Dkt Clement Morabu kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Mganga Mkuu Hospitali ya Wilaya ya Misungwi


wananchi

Mgeni rasmi akipata maelezo kutoka kwa mtaalamu wa afya

Na Maganga James Gwensaga - Mwanza

Katika kukabiliana na tatizo la ugonjwa wa kifua kikuu mkoa wa Mwanza umefanikiwa kwa kiwango kikubwa kupitia  Mikakati mbalimbali iliyoiweka  ikiwemo kuanzishwa kwa  wilaya za kimkakati za kifua kikuu zipatazo tisa  za Buchosa , Kwimba , Magu, Misungwi, Mwanza East, Mwanza North, Mwanza south, Sengerema na Ukerewe kwa lengo la kuibua wagonjwa 4745 ili kufikia asilimia moja ya lengo la Mkoa.

Mafanikio mengine ni  kila Wilaya ya kifua kikuu kuwa na mratibu wa kifua kikuu ambaye atashirikiana na Mratibu wa Kifua kikuu na Ukimwi, uwepo wa Muuguzi wa kutoa dawa za kifua kikuu (DOT Nurse) kila kituo cha tiba, ongezeko la vituo vya kupimia kifua kikuu 88 pamoja na uwepo wa gari maalumu la kliniki Tembezi ya kifua kikuu, gari ambalo linatoa huduma Kanda ya Ziwa.

Hayo yameelezwa na Dkt Nangi William Mratibu wa kifua kikuu na ukoma Mkoani Mwanza,  March 24, 2022 wakati akitoa taarifa ya hali ya kifua kikuu Mkoani Mwanza   kwa Mgeni Rasmi Dkt Clement Morabu kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ambaye pia ni Mganga Mkuu Hospitali ya Wilaya ya Misungwi kwenye maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu nchini ambayo kiMkoa yaliyofanyika Wilayani Misungwi.

“ Leo March 24, 2022 tunaadhimisha siku ya kifua kikuu Duniani ikiwa ni kumbukumbu ya matokeo makubwa ya ugunduzi wa vimelea vinavyosababisha ugonjwa wa kifua kikuu vinavyojulikana kwa jina la Mycobacterium tuberculosis ambapo mtafiti na Mwana Mikrobailojia Daktari Robert Koch aliitangazia dunia matokeo ya utafiti wake katika Jiji la Berlin mwaka 1882.” Alisema Dkt Nangi

Aidha aliyataja mafaniko mengine ni uwepo wa  vituo 275 vya kutolea dawa za kifua kikuu, mashine za x-ray 17 ambazo pamoja na kupima magonjwa mengine hutumika pia kupima kifua kikuu pamoja na uwepo wa kituo maalum cha huduma za wagonjwa wa kifua kikuu sugu(MDR-TB) Kilichopo Bugando.

Alisema hadi  kufikia Disemba 2021, Mkoa wa Mwanza ulikuwa na jumla ya wagonjwa wa kifua kikuu 4409 na wenye kifua kikuu sugu 17 huku katiki yao waliopima vvu ni 4248 na waliopatikana na maambukizi ni 991.

Aidha aliwapongeza wadau wa maendeleo katika seksheni ya Afya ambao ni Amref anayetekeleza mradi wa afya shirikishi kwa ushirikiano na shirika la SHDEPHA+ Kahama katika kutoa huduma za kifua kikuu katika ngazi ya Jamii ambapo katika mradi huo wahudumu wapatao 99 pamoja na waendesha bopdaboda hukusanya sampuli na kusafirisha kwenye vituo vya upimaji.

“ Pia tunashukuru shirika la ICAP kupitia mradi wao wa FIKIA+ pia kwa kushirikiana  na shirika la SHDEPHA + la Kahama anayetekeleza huduma za kifua kikuu na Ukimwi ngazi ya Jamii.

Alizitaja changamoto mbalimbali zinazaowakabili katika utekelezaji wa mapambano dhidi ya kifua kikuu kuwa  ni uhaba wa mara kwa mara   wa upatikanaji wa makopo ya kukusanyia sampuli za makohozi pamoja na kuharibika mara kwa mara kwa mashine za Gene x-pert hali inayorudisha nyuma jitihada za kuibua wagonjwa wa kifua kikuu.

Kwa upande wake Dkt Clement Morabu kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Mganga Mkuu Hospitali ya Wilaya ya Misungwi amefurahishwa sana kwa namna ya mkoa ulivyojipanga katika mapambano ya kifua kikuu.

“ Niwapongeze sana Mkoa wa Mwanza kupitia taarifa ya mratibu ikiwemo kuanzisha wilaya za kimkakati katika kukabiliana na ugonjwa huu na nimefurahi sana kuona hata kwenye maadhimisho haya kuna banda la uchunguzi wa kifua kikuu haya ni mafanikio makubwa sana hongereni.”  Alisema Dkt Clement

Kitaifa Siku ya Kifua kikuu Duniani uadhimishwa kila tarehe 24 mwezi Machi na kwa mwaka huu,  iliadhimishwa Kitaifa Mkoani Tanga ambapo mgeni rasmi alikuwa Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu Waziri wa Afya na Kauli Mbiu ya Mwaka huu ni OKOA MAISHA, WEKEZA KATIKA KUTOKOMEZA KIFUA KIKUU NCHINI.

No comments:

Post a Comment