KATIBU Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda, Biashara Prof. Godius Kahyarara ameitembelea kamati maalumu iliyoundwa ikishirikisha taasisi mbalimbali za Serikali kwa lengo la kutengeneza mfumo wa kielektroniki wa huduma za pamoja kwa wawekezaji unaojulikana kama Tanzania Electronic Investment Window – TeIW.
Prof. Kahyarara amesema kuwa utengenezwaji wa
mfumo huu ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Samia Suluhu Hassan alilolitoa akihitaji Wizara kuanzisha mfumo wa utoaji
huduma kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kuwa na dirisha moja la
huduma.
Prof. Kahyarara alieleza kuwa timu hii imeanza
kazi hii tangu tarehe 7 Desemba, 2021 ambapo walianza kutengeneza mfumo huu
katika awamu ya kwanza na upo katika hatua ya mwisho kukamilika na kuanza
majaribio na kwa awamu ya kwanza mfumo umeziweka pamoja taasisi saba ikiwemo
NIDA, TRA, BRELA, ARDHI, KAZI, UHAMIAJI na TIC.
Alisema kuwa awamu ya pili ya utengenezwaji wa
mfumo huu utahusisha taasisi tano zilizosalia ambazo ni TMDA, OSHA, TANESCO,
TBS na NEMC.
“Faida za
mfumo huu ni kuwa utasaidia upatikanaji wa vibali vyote vinavyotolewa nchini
kupatikana kwa urais na kwa haraka kwani huduma zote zitapatikana kupitia
dirisha moja na mwekezaji ataweza kuomba vibali husika mahali popote alipo, pia
utasaidia kufuatilia hatua za maombi ya uwekezaji”. Alisema Prof.
Kahyarara.
Aliongeza kwa kusema kuwa kuanza kutumika kwa
mfumo huu utasaidia kupunguza urasimu, gharama na muda kwani mwekezaji atapata
huduma zote kupitia mfumo huu na sio kukutana na watoa huduma na hii itasaidia
hata kupunguza rushwa na udanganyifu.
Prof. Kahyarara akatumia fursa hiyo kuwashukuru
wabia wa maendeleo Trade Mark East Afrika (TMEA) ambao wamefadhili kuwaweka
pamoja wataalamu wa kuandaa mfumo huu na sasa nchi yetu inaenda kunufaika kwani
wawekezaji watazidi kuja kwa wingi kwani urasimu utapungua kwa kiasi kikubwa.
Kwa upande wake Mratibu wa mradi wa uaandaaji
wa mfumo wa dirisha moja kwa wawekezaji (One Stop Centre) Robert John
Mtendamema alisema kuwa kituo cha uwekezaji nchini kilianzishwa mwaka 1997
kikiwa na lengo la kuwahudumia wawekezaji kwa haraka chini ya mwamvuli wa
dirisha moja (One stop shop) ambapo taasisi mbalimbali za Serikali zinahudumia
wawekezaji zimeweka maafisa ambao wana uwezo wa kutoa maamuzi ya kutoa vibali
hivyo.
Mtendamema alisema kuwa kupitia mfumo huu
unaoundwa sasa utawezesha kuondoa kero mbalimbali kwa wawekezaji hasa zile za
kumlazimisha mwekezaji kuingia katika mifumo mbalimbali kutafuta vibali na sasa
ataingia katika dirisha moja na kukuta taasisi zote na kufanya maombi kwa
wakati mmoja, pia kupitia mfumo huu utawarahisishia wawekezaji kufanya maombi
ya vibali na hii itapelekea kuongezeka kwa wawekezaji nchini kwa sababu ya
urahisi wa kufanya maombi ya vibali mbalimbali.
Mtendamema aliongeza
kwa kusema kuwa kutokana na kukua kwa maendeleo ya sayansi na teknolojia ya
TEHAMA kila taasisi ndani ya One Stop Centre wameweza kuwa na mfumo wa kutoa
kutoa huduma mbalimbali ambapo mwekezaji anapofika TIC inamuhitaji kuingia
katika mifumo isiyopungua 12 ya kila taasisi yenye nywila tofauti kwa ajili ya
kufanya maombi.
No comments:
Post a Comment