Monday, March 21, 2022

KAMATI YA BUNGE YARIDHIKA NA HATUA ZA UJENZI DARAJA LA KITENGULE

Muonekano wa Daraja jipya la Kitengule lenye urefu wa Mita 140 linalojengwa pamoja na barabara unganishi (Km 18). Daraja hili linaunganisha barabara kuu ya Kyaka-Bugene-Benako na barabara ya Kagera Sugar Junction-Kakunyu, katika Wilaya za Misenyi, Karagwe na Ngara mkoani Kagera.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso (kushoto), akisikiliza maelezo ya mradi wa ujenzi wa Daraja la Kitengule kutoka kwa Mhandisi Mshauri wa daraja hilo Lukas Nyaki, lenye urefu wa Mita 140, ambalo linajengwa na barabara unganishi Km 18. kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya. Daraja hilo linaunganisha Wilaya za Misenyi, Karagwe na Ngara mkoani Kagera.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso, akitoa maelekezo kwa Mhandisi Mshauri wa mradi wa ujenzi wa Daraja jipya la Kitengule, wakati kamati yake ikikagua hatua za ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa Mita 140 linalojengwa na barabara unganishi Km 18. Daraja hilo linaziunganisha barabara kuu ya Kyaka-Bugene-Benako na barabara ya Kagera Sugar Junction- Kakunyu, katika Wilaya za Misenyi, Karagwe na Ngara mkoani Kagera.

 

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu wakikagua sehemu ya juu ya Daraja jipya la Kitengule, lenye urefu wa Meta 140 linalojengwa pamoja na barabara unganishi Km 18. Daraja hilo linaunganisha barabara kuu ya Kyaka-Bugene-Benako na barabara ya Kagera Sugar Junction-Kakunyu, katika Wilaya za Misenyi, Karagwe na Ngara mkoani Kagera.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu wakitoka sehemu ya chini ya daraja jipya la Kitengule, baada ya kujiridhisha na hatua za ujenzi wa daraja hilo. Daraja la Kitengule lina urefu wa Mita 140, linajengwa pamoja na barabara unganishi Km 18 na linaunganisha barabara kuu ya Kyaka-Bugene-Benako na barabara ya Kagera Sugar Junction-Kakunyu, katika Wilaya za Misenyi, Karagwe na Ngara mkoani Kagera.

Picha na WUU

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeridhika na hatua za ujenzi wa Daraja jipya la Kitengule linalojengwa mkoani Kagera, lenye urefu wa Mita 140 pamoja na barabara unganishi Km 18, ambapo hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 77.

Akizungumza kwenye kikao cha majumuisho baada ya kukagua ujenzi wa daraja hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso, amesema kuwa kamati yake imeridhika na maendeleo ya hatua za ujenzi wa daraja hilo, akashauri ni vyema daraja hilo litakapokamilika lijengewe misingi ya uhifadhi wa mazingira, na kwamba katika kipindi cha matazamio kingo za mto huo zipandwe miti ili kuzuia maporomoko pamoja na kuimarishwa kwa ulinzi katika eneo la daraja hilo ili kuepuka uhujumu wa miundombinu ya daraja utakaoweza kufanywa na wananchi wasio na uzalendo.

“Kamati yangu imeridhishwa na maendeleo ya mradi wa ujenzi wa daraja hili ambalo ni mradi wa kimkakati, wenye lengo la kukuza uchumi hasa kutokana na shughuli zinazofanywa za uzalishaji wa sukari katika Kiwanda cha Sukari cha Kagera lakini vilevile kufunguka kwa barabara kati ya wilaya za Misenyi, Karagwe na Ngara kutachochea biashara kati ya mkoa huu na nchi jirani za Rwanda na Burundi kupitia barabara ya Kyaka, Bugene hadi Benako inayoanzia Rusumo na Kabanga wilayani Ngara kwenye mipaka ya Rwanda na Burundi,” amesema Kakoso.

Mwenyekiti huyo amekipongeza Kiwanda cha Sukari cha Kagera kwa kuunga mkono jitihada za Serikali katika ujenzi wa daraja hilo na kuwataka wazalishe sukari kwa wingi zaidi ili thamani ya fedha iliyowekezwa kwenye mradi wa ujenzi wa Daraja la Kitengule isipotee bure kwa kuhakikisha kuwa sukari inayozalishwa kiwandani hapo inasambaa nchi nzima.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Ujenzi), Mhandisi Godfrey Kasekenya amewaambia wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuwa daraja hilo tayari limeanza kutumika na kwamba Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa, amemuagiza Mhandisi Mshauri kusanifu sehemu ya barabara kutoka Daraja la Kitengule kuunganisha na Kakuyu hadi Bunazi (km 25) itakayounganishwa na barabara ya Mutukula, ili iingizwe kwenye bajeti kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami.

Awali, akisoma taarifa yake kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Yudas Msangi, ameiambia Kamati hiyo kuwa Daraja la Kitengule limejengwa kwa lengo la kuziunganisha barabara kuu ya Kyaka-Bugene-Benako na barabara ya Kagera Sugar Junction-Kakunyu, katika Wilaya za Misenyi, Karagwe na Ngara, na kwamba daraja hilo linajengwa na Kampuni ya China International Cooperation Group kwa gharama ya Shilingi Bilioni 25 na ujenzi wake unatarajia kukamilika ifikapo mwezi Mei, 2022.

Nae mwakilishi kutoka Menejimenti ya Kiwanda cha Sukari cha Kagera  amesema kuwa kiwanda hicho kimetumia takriban Shilingi Bilioni 5 katika kuchangia ujenzi wa daraja hilo ikiwa ni mchango kwa ajili ya  ujenzi wa Taifa. Ameongeza kuwa ujenzi wa daraja hilo utawezesha kiwanda hicho kuongeza idadi ya ajira kiwandani hapo kutoka elfu kumi hadi elfu kumi na tano na hivyo kuongeza uzalishaji wa sukari kiwandani hapo kutokana na kuongezeka kwa uvunaji wa miwa kutoka upande wa pili wa Mto Kagera.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ipo mkoani Kagera kwa ziara ya kikazi ya siku moja, kwa ajili ya kukagua hatua za ujenzi wa miundombinu ya Daraja la Kitengule linalojengwa kwenye mto Kagera pamoja na barabara unganishi.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

No comments:

Post a Comment