KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imelipongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kuridhishwa kwa kutekeleza vizuri mradi wa Backbone Transmission Investment Project (BTIP) awamu ya pili unaofanywa katika mikoa ya Iringa, Dodoma, Shinyanga na Singida.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kudumu wa Bunge wa kamati hiyo Naghenjwa Kaboyoka wakati kamati hiyo ilipotembelea kukagua mradi huo mkoani Singida jana.
“ Tumefika leo kutembelea mradi huu wa kimkakati ambao serikali imetumia fedha nyingi kwa kufadhiliwa kwa fedha za mkopo kutoka kwa wahisani wa maendeleo ya sekta ya Nishati na kuridhishwa na utekelezaji wake” alisema Kaboyoka.
Kaboyoka alisema changamoto walizoambiwa na watekelezaji wa mradi huo wamezichukua na watazifanyia kazi kwa kuziwasilisha kunakohusika.
Mratibu wa mradi huo Mhandisi Emmanuel Manirabona akitoa taarifa mbele ya kamati hiyo alisema Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango na wahisani wa maendeleo wa sekta ya Nishati walikubaliana kutumia akiba iliyopatikana kwa awamu ya isaidie kutekeleza awamu ya pili ya mradi.
“Awamu hii ya pili inafadhiliwa kwa fedha za mkopo kutoka kwa wahisani wa maendeleo ya sekta ya Nishati ambao ni Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ,Shirika la Kimataifa la Kimataifa la Japan (JICA) pamoja na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) kwa jumla ya kiasi cha Dola za Marekani 120 Milioni” alisema Manirabona.
Alisema katika kuhakikisha kuwa mradi huo unatekelezwa kulingana na mahitaji yaliyotolewa kwa wakandarasi kwa ubora unaotakiwa na kuhakikisha kuwa TANESCO inapata mradi wenye thamani ya fedha itakazotoa ilifanya manunuzi ya Mkandarasi Mshauri kusimamia mradi huo kwa niaba ya uongozi wa shirika.
Mhandisi Manirabona aliongeza kuwa shirika hilo limeweka timu ya mradi inayoundwa na Mratibu, mameneja wa miradi na wahandisi wa mradi watakaosimamia kila siku shughuli za mradi.
Alisema faida za mradi huo kwa nchi yetu mara utakapokamilika utaongeza uwezo wa kusafirisha umeme kwa wingi kwenda kwenye mikoa yenye mahitaji makubwa ya umeme, kuunganishwa kwa gridi ya taifa kwenye kanda ya Afrika Mashariki (EAPP) kupitia mradi wa Kenya, Tanzania na Kusini (SAPP) kupitia mradi wa Tanzania, Zambia na kuweza kufanya biashara ya kuuziana nishati ya umeme hivyo kukuza uchumi na pato la taifa kwa ujumla.
Alitaja faida nyingine kuwa ni kupunguza upotevu wa umeme na kulisaidia Shirika kukwepa gharama nyingi zinazotokana na upotevu huo.
,Mkaguzi Mkuu wa Nje kutoka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Priscus Ngowi alitaja baadhi ya changamoto walizoziona baada ya matokeo ya ukaguzi ya mwaka wa fedha ulioishia Juni 2021 ya utekelezaji wa mradi huo kuwa ni Mabadiliko ya sheria za kodi kwa miradi ambayo imekwishaanza kutekelezwa, Mabadiliko ya viwango vya malipo kwa Wakala wa Barabara (TANRODS) kwa kuzidisha uzito wa mizigo, Ucheleweshaji wa malipo kwa mkandarasi kwa miradi inayopokea malipo moja kwa moja kutoka kwa mfadhili na kushindwa kukamilika kwa vituo vya Iringa na Shinyanga.
No comments:
Post a Comment