Na Fredy Mgunda,Iringa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa chama cha akiba na mikopo cha ‘Machinga Saccos’ mkoa wa Dar es Salaam, Februari 20, mwaka huu.
Uzinduzi wa Machinga Saccos unakuja ikiwa ni maelekezo ya Rais Samia alipokutana na viongozi wa Machinga mkoa wa Dar es Salaam, Januari 25, 2022.
Akizungumza na waandishi wa habari, Naibu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Machinga Taifa, Joseph Mwanakijiji alisema kuwa Saccos hiyo itakuwa ni suluhisho kwa wafanyabishara hao watakapopata majanga mbalimbali.
Mwanakijiji alisema kuwa swala la mitaji kwa machinga limekuwa kikwazo kikubwa katika kukuza biashara wanazozifanya hivyo kuwepo kwa chombo hicho kutasaidia kukuza mitaji yao.
“Tumekuwa tukipata tabu namna gani ya kukopeshwa, pamoja na mikopo yenye gharama kubwa, kwa hiyo kupitia Saccos hii sisi machinga tutakuwa tumepata suluhisho.
“Saccos imebeba kila kitu, mitaji tutapata hapa, bima pamoja na vitu mbalimbali hivyo natoa wito kwa wamachinga mkoa wa Dar es Salaam waweze kujiunga kwa wingi,” amesema Lusinde.
Alisema kuwa kuzinduliwa kwa SACCOS hiyo kutakuwa na faida ya wafanyabishara hao kuanza kukopa kwa riba nafuu tofauti ilivyo hivi sasa ambavyo wanahangaika kupata mitaji ya kukuza biashara zao.
Mwanakijiji alisema kuwa wafanyabiashara wadogo wadogo (MACHINGA) wanaungana na wafanyabiashara hao nchi nzima kukifanya chombo hicho kuwa imara zaidi kwa kuwasaidia mitaji machinga wote.
alisema kuwa wanampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suhulu Hassan kwa kuamua kuanzisha SACCOS ya machinga nchi nzima kwa kuwa itasaidia kukuza mitaji ya wafanyabiasha hao.
Mwanakijiji alisema kuwa amekuwa Rais wa kwanza kuweka historia ya kukutana kundi hilo la wafanyabiashara wadogo wadogo na kutambua mchango wao katika kukuza uchumi wan chi.
Alisema katika siku hiyo ya uzinduzi pia watazindua kitabu kitakachoelezea historia ya Machinga ambacho wamekipa jina la ‘Mama wa Taifa’.
“Pamoja na kuelezea historia ya machinga pia itamuelezea Rais wetu ambaye ni Rais wa kwanza mwanamke hapa nchini. Tunawakaribisha wamachinga wahudhurie kwa wingi siku hiyo,” amesema Mwanakijiji.
Mwanakijiji alisema wataendelea kuhamasishana ili na mikoa mingine iweze kuanzisha Saccos.
No comments:
Post a Comment