Na Mathias Canal, Dodoma
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa Mwaka huu 2021/22, Wizara hiyo imetenga kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuendeleza watakaoibuliwa katika MAKISATU 2022.
Akizunguzma na waandishi wa Habari Ofisini kwake Jijini Dodoma leo tarehe 16 Februari 2022 amesema kuwa Wiki ya Kitaifa ya Ubunifu ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuongeza hamasa ya matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu kama nyenzo ya kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii.
Amesema kuwa Wiki ya Ubunifu inaandaliwa kwa kushirikiana na programu ya FUNGUO ya UNDP inatarajiwa kufanyika katika mikoa 17 nchini ambayo ni: Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya, Arusha, Iringa, Mwanza, Zanzibar, Tanga, Kilimanjaro, Morogoro, Njombe, Kagera, Mtwara, Kigoma, Mara, Ruvuma. Aidha, kitaifa Wiki ya Ubunifu 2022 itaadhimishwa tarehe 15-20 Mei, 2022, jijini Dodoma sambamba na kilele cha MAKISATU.
Vilevile, Waziri Mkenda ameeeleza kuwa katika kilele hicho tutakuwa na maonesho ya teknolojia na bunifu mbalimbali, bidhaa na huduma zinazotolewa na taasisi zitakazoshiriki zikiwemo taasisi za kitafiti na maendeleo, Vyuo Vikuu, kumbi za ubunifu, taasisi za kibiashara, wakala za Serikali, Wizara na Taasisi Binafsi.
Maadhimisho ya Wiki ya Ubunifu yatahusisha pia majukwaa na majadiliano kuhusu maendeleo ya Sayansi, teknolojia na ubunifu Nchini, mafunzo na semina kwa wabunifi ikiwemo limu ya ujasiriamali. Aidha, mijadala hiyo itawahusisha wabunifu, wadau mbalimbali wa ubunifu na Serikali, kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja ya kuhamasisha matumizi ya teknolojia na ubunifu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
MWISHO
No comments:
Post a Comment