Na Fredy Mgunda,Iringa.
Wakala wa huduma za misitu Tanzania TFS kupitia shamba la miti
la Sao Hill Mkoani Iringa limegawa miche milioni moja (1,000,000) kwa wananchi
wa vijiji vinavyolizunguka shamba la Miti SaoHill na wadau taasisi mbalimbali
za serikali mkoani Iringa na nje ya Iringa katika msimu wa mwaka wa 2021/2022
kwa lengo la kuimalisha ujirani mwema ambao umekuwa umedumu kwa miaka mingi.
Akizungumza wakati wa ugawaji wa miti hiyo Mhifadhi mkuu wa shamba la miti Sao
HillLucas Sabida alisema kuwa zoezi la ugawaji miche ya miti kwa ajili ya
ujirani mwema hufanyika kila mwaka kipindi cha masika kwa lengo la kuhakikisha
wanapanda miti hiyo na inakuwa kwa wakati,hasa kipindi hiki kizuri cha mvua za
msimu.
alisema kuwa hatua ya ugawaji wa miche ya miti husaidia kwa kiasi kikubwa
kuwakumbusha wananchi juu ya uhifadhi wa misitu katika maeneo yao kwani
wanapochukua miche hiyo huelekezwa namna na ya kuipanda na tunzaji wake.
Sabida aliwataka wananchi kuendelea kuhimizwa juu ya utunzaji wa miti
wanayoipanda ili iwe na manufaa kwao na vizazi vijavyo.
Alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2016/2017 mpaka 2020/2021 wamezalisha na kugawa jumla ya miti milioni tano yenye thamani ya kiasi cha bilioni moja na milioni mia tano (1,500,000,000/=).
Sabida alisema kuwa mwaka huu wamegawa miche milioni moja yenye thamani ya shilingi milioni mia tatu (300,000,000/=) kwa wananchi wanaolizunguka shamba hilo pamoja na taasisi mbalimbali za serikali.
Kwa upande wake mgeni rasmi wa zoezi la ugawaji wa miche hiyo mkuu wa wilaya ya Mufindi Saad Mtambule alisema kuwa anaupongeza uongozi wa shamba la miti la Sao Hill kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa kutunza miti na mazingira kwa ujumla.
Alisema kuwa uwepo wa shamba hilo katika wilaya ya Mufindi kunachangia kwa asilimia kubwa kukuza uchumi wa wananchi ambao kwa asilimia kubwa pia wanategemea uchumi wa misitu kuendesha maisha yao.
Mtambule alisema kuwa zaidi ya wananchi elfu sita wameajiriwa kwenye viwanda ambavyo vinazalisha bidhaa za misitu hivyo uwepo wa shamba hilo kunachochea kukuza uchumi wa wananchi kwa kiasi kikubwa.
Alisema kuwa wananchi wanatakiwa kuacha mara moja tabia ya kuchoma moto bila kupata kibali kutoka kwa mamlaka husika na kuwahimiza kuendelea kupanda miti kwa wingi.
Shamba la Miti SaoHill ni miongoni mwa mashamba 23 ya miti ya kupandwa ya
serikali yanayosimamiwa na Wakala wa Huduma wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)
lenye ukubwa wa hekta 135,903 ambazo zimehifadhiwa kwaajili ya upandaji miti
kibiashara na hifadhi ya mazingira na vyanzo vya maji,makazi ya watumishi na
uwekezaji.
No comments:
Post a Comment