Sunday, February 27, 2022

MBUNGE CHEREHANI ATAKA WOTE WANAOHUSIKA KWENYE MNYORORO WA TUMBAKU KUENDELEA KUWATENDEA HAKI WAKULIMA

Mbunge wa Ushetu Mhe. Emanuel Cherehani akizungumza  na wadau  na wa chama katika Mkutano Mkuu wa nne wa Chama Kikuu cha Ushirika Milambo kilichopo Mkoani Tabora  Ulipofanyika February 26 , 2022.
Mbunge Mhe.Emanuel Cherehani Akishusha Nondo Kwenye Mkutano wa chama cha Ushirika Milambo

Na Mwandishi Wetu, Tabora

MBUNGE wa Jimbo la Ushetu Wilayani Kahama Mhe. Emmanuel Cherehani ameshiriki mkutano mkuu wa nne wa Chama Kikuu cha Ushirika Milambo kilichopo Mkoani Tabora akimuwakilisha Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe.

Amesema katika kipindi hichi cha kuelekea kwenye manunuzi ni muhimu wote wanaohusika na mnyororo wa zao la tumbaku kuhakikisha bei inakuwa nzuri, kuteua  madaraja kwa usahihi wa sokoni na kutatua changamoto zinazowakabili wakulima ili mkulima aweze kurejesha mikopo na kuinuka kiuchumi.

Cherahani ametoa rai hiyo wakati wa mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika mkoani Tabora leo tarehe 26 Februari 2022 na kuhudhuriwa na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Tumbaku Tanzania, wanunuzi wa Tumbaku, Taasisi za Fedha pamoja na wawakilishi wa vyama vikuu vinavyolima Tumbaku.

Mbunge Cherehani amewataka viongozi kuhakikisha wanasimamia malipo ya wakulima ili waweze kulipwa kwa wakati jambo litakalowafanya waweze kufanya maandalizi ya mashamba kwa ajili ya msimu unaofuata kwa wakati.

Katika hatua nyingine Mhe Cherehani amempongeza Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutatua changamoto za wakulima.

MWISHO

No comments:

Post a Comment